Na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto
Afisa Mawasiliano Mkuu kutoka Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Idara ya Usimamizi
wa Maadili Rocky Setembo amewaasa waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania kuepuka
matumizi ya mitandao ya kijamii kutuma taarifa mbalimbali za uendeshaji wa
shughuli za kiutumishi kwa kuwa bado njia hiyo sio rasmi na haijaidhinishwa.
Setembo amesema hayo leo tarehe 21
Julai, 2022 mjini hapa alipokuwa akitoa mada kuhusu misingi na kanuni za
maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwenye mafunzo elekezi kwa Mahakimu
na Wasaidizi wa Kumbukumbu yanayoendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama
Lushoto.
Amesema hadi sasa hakuna Waraka
ambao umetolewa kuruhusu mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp , Instragrum na
Twiter kutumika katika utumaji wa nyaraka muhimu za Serikali kama vile barua,
waraka na madokezo.
Setembo ameongeza kuwa hadi sasa
njia ambayo watumishi wa umma wanapaswa kutuma barua za kiutumishi ni kupitia
Posta na barua pepe ya Serikali ambayo ina jina la taasisi husika na kuendelea
ikiwa na maneno ya @go.tz na sio kwa
kutumia barua pepe nyingine ambayo wamiliki wa chombo cha kutunzia
kumbukumbu(Server) wako nje ya Tanzania.
Aidha, Setembo amewataka watumishi
hao wapya kutumia muda wa Serikali kwa ajili ya kutoa huduma nzuri kwa wananchi
badala ya kusoma na kujibu ujumbe katika
makundi mbalimbali ya mitandao ya kijamii ambayo hayana tija kwa umma.
“Utakuta mtumishi mmoja wa umma amejiunga na
makundi ya Whatsapp na twiter mbalimbali,
mfano anaweza kuwa na kundi la aliosoma nao Sekondari, Chuoni na katika makundi yote anataka kujibu kila
ujumbe unaoandikwa, hali hiyo wakati mwingine inasababisha kutumia muda wa
Serikali jambo ambalo ni makosa,”amesema.
Katika hatua nyingine, Afisa Mawasiliano
huyo Mkuu amewataka watumishi hao watakapokuwa katika vituo vyao vya kazi
kutumia lugha nzuri na yenye staha wanapotoa huduma kwa wateja wa ndani na wa
nje ili kuepuka kuwaathiri na kuchafua jina la taasisi ambayo watakuwa
wakiitumikia.
Afisa Mawasiliano Mkuu kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Idara ya Usimamizi wa Maadili Rocky Setembo akitoa mada kuhusu misingi na kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwenye mafunzo hayo.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama, Lushoto)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni