Na. Faustine Kapama na Magreth Kinabo-Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Mamlaka ya Usimamizi
wa Bima Tanzania (TIRA) kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho kwenye sheria
inayoendesha taasisi hiyo ili kuwezesha mashauri ya bima kutatuliwa kwanza kwa
njia ya usuluhishi kabla ya kupelekwa mahakamani.
Mhe.
Prof. Juma ametoa ushauri huo leo tarehe 21 Julai, 2022 alipokutana na viongozi
waandamizi wa TIRA ambao walimtembelea ofisini kwake katika jengo la Mahakama
ya Rufani jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha (Curtesy Call),
kukuza na kuendeleza mahusiano na ushirikiano bora kati ya Mamlaka na Mhimili
wa Mahakama ya Tanzania.
“Huu ni wakati wenu wa kuangalia sheria zenu
upya hasa hizi sehemu ambazo mnasema
kuna uwiano wa kufuata taratibu lakini watu bado wanakimbilia mahakamani kwa
sababu tangu mwaka 2020 sheria mpya ya usuluhishi imetungwa kwa lengo la
kupunguza kujaza mashauri katika Mahakama hizi za kawaida,” amesema.
Jaji
Mkuu amebainisha kuwa katika Mahakama hizo za kawaida kuna kanuni nyingi ambazo
wengine huzitumia vibaya aidha kuchelewesha au kupata ujanjaujanja fulani, jambo
ambalo kwenye usuluhishi sheria siku hizi inaruhusu mchakato wa kutatua madai kufanyika.
“Hili
ni eneo ambalo linaweza kubadilishwa kwamba kabla ya kwenda mahakamani tumalize
masuala ya usuluhishi na sisi tutafurahi sana kama mtatupunguzia mzigo wa
mashauri kwa watu kuelewana nje ya Mahakama. Sheria imebadilika, kanuni hata
siku hizi zimeshatangazwa kwa wale ambao wanaruhusiwa kufanya suluhisho,”
amesema.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao ambao ni Kamishina wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware, Mkurugenzi wa Sheria Emily Kiria, Kaimu Meneja Usimamizi wa vihatarishi na Ubora, Dkt Emanuel Lupilya, Meneja Mawasiliano Eliezer Rweikiza ambao waliambatana na Mwenyekiti wa wa Umoja wa Kampuni za Bima, Bw. Khamis Suleiman, waliwasilisha maombi mbalimbali, ikiwemo uwezekano wa Mahakama kutoa kipaumbele cha kusikiliza kwa haraka mashauri ya bima.
Jaji
Mkuu amesema kuwa mashauri ya bima ni ya kiuchumi, hivyo akipata orodha kutoka
kwa viongozi hao atayapeleka kwa Jaji Kiongozi ili kuona uwezekano wa kuyafanya
yawe baadhi ya mashauri ambayo yanaweza kupewa kipaumbele katika kusikiliza na
kukamilika kwa haraka. “Hivyo, kesi kupewa kipaumbele haina shida kwa sababu
sisi tuna maeneo asmbayo tunatoa kipaumbele,” Mhe. Prof. Juma amewahakikishia
viongozi hao wa TIRA.
Akiwasilisha
taarifa yake mbele ya Jaji Mkuu, Dkt. Saqware amesema kuwa hadi sasa Mamlaka
imesajili makampuni 33, madalali 91, mawakala 958, wadhamini na wakadiriaji
hasara 45 na wachunguzi 2. Amesema kuwa kwa mwaka 2021, kampuni za bima
zilifanya biashara yenye jumla ya shilingi billioni 991.5 za Kitanzania, kiasi ambacho ni
ongezeko la zaidi ya asilimia 10.6% ukilinganisha na mwaka 2020 ambapo kilikuwa
ni shillingi billioni 824.35.
Kamishina
huyo amesema kuwa sekta ya bima kwa ujumla inakua kwa kasi na ili kuikuza zaidi
wanahitajika kama Taifa kutatua changamoto inazokabiliana nazo ikiwemo kuandaa
na kuitekeleza Sera ya Taifa ya Bima (NIP) na kuongeza mitaji ya makampuni ya
bima ili kuwa na uwezo wa kuchukua na kuhimili biashara zote zinazojitokeza
kama fursa kwenye sekta ya umeme, gesi, mafuta na usafiri wa anga.
Amestaja
changamoto nyingine ambayo inahitajika kutatuliwa ni kuondoa udanganyifu na
kupunguza ongezeko la kesi za Madai. Amesema Mamlaka yake ina taarifa za kuwepo
kwa kesi za madai 118 ambazo zipo katika Mahakama mbalimbali nchini zenye
thamani zaidi ya shillingi billioni 90 za Kitanzania ambazo zimekaa mahakamani
kwa muda mrefu.
“Katika
muktadha huu na kwa kutambua umuhimu wa Mahakama katika kuamua haki za watu,
wakiwepo wadau wa bima, basi, Mamlaka
inaomba kesi za bima zipewe kipau mbele ili kusaidia kuwarudisha wadai
katika hali zao kabla ya janga kama kanuni za bima zinavyoelekeza,” Dkt. Saqware
alipendekeza kwa Jaji Mkuu.
Kadhalika,
ameomba Mahakama kuwa na ushirikiano na Mamlaka katika maeneo na matukio
mbalimbali yatakaojitokeza na kutazama kesi za bima kwa jicho la huruma ili
zifuate mtiririko uliopo wa kusuluhisha
kibima ili kupunguza madai ambayo yanatishia uhai wa sekta ya bima,
fedha na uchumi kwa ujumla.
Mamlaka
ya Usimamizi wa Bima ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha na
Mipango. Imeanzishwa kwa Sheria ya Bima Na.394, kama ilivyorekebishwa mwaka
2019.
Kazi
za Mamlaka ni pamoja na kusimamia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya
uendeshaji wa shughuli za bima nchini, ikiwemo kufanya kazi ya kusajili, kutoa
leseni (kwa makampuni ya bima na watoa huduma za bima madalali, mawakala,
wakadiriaji na watathmini hasara, wachungzi) na kusimamia uhai na ustahimilivu
wa sekta ya bima, kusimamia uweledi na maadili ya watoa huduma za bima nchini.
Kazi
nyingine ni kukuza na kuendeleza biashara ya bima kwa kuwa bima ni kati ya
vichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kulinda maisha, Afya za
watu na mali zaokwa kuwarudisha katika hali zao kabla ya kupata majanga
yanayowezakuwarudisha nyuma katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii
Kamishina
huyo ametaja kazi zingine za Mamlaka ni kutoa elimu kwa umma na kulinda haki za
wateja wa bima ili kupanua na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za bima
nchini na pia kuishauri Serikali kuhusu mambo yanayohusiana na Bima ya Mali,
Maisha na Afya kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania.
Kamishina wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishina wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware (kulia) na Mwenyekiti wa wa Umoja wa Kampuni za Bima, Bw. Khamis Suleiman (kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni