· Benki ya Dunia haiamini kinachotokea
·Kasi usikilizaji mashauri inatisha
Na.
Faustine Kapama-Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wa
Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke kinachojishughulisha na
masuala ya familia kwa huduma nzuri wanazotoa kwa wananchi, hatua iliyoifanya
Benki ya Dunia kutoamini kinachotokea.
Mhe.
Prof. Juma ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Julai, 2022 alipotembelea Kituo
hicho kama sehemu ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama kukagua shughuli
mbalimbali za kiutendaji, kuangalia utoaji wa haki na kuzungumza na watumishi.
Jaji
Mkuu huyo amebainisha kuwa mara nyingi huwa anapata pongezi kwa niaba ya
watumishi kutoka katika makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo Benki ya
Dunia, ambayo Mkurugenzi wake aliitembelea Mahakama ya Tanzania hivi karibuni
kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini kwa ufadhiri wa Benki
hiyo ya kimataifa.
“Mkurugenzi
wa Benki ya Dunia amewasifu sana alipotembelea hapa tarehe 17 Novemba, 2022,
hakuwa na hakika kwamba yale ambayo Benki ya Dunia ilikuwa imeota, yale ambayo
yameandikwa kwenye makabrasha kuwa Kituo Jumuishi, alipofika hapa
akakuta ni kweli.....
“.....aliniandikia
barua kwamba niwapongeze na vile vile alituma ujumbe wa twitter kwa watumishi
wote wa Benki ya Dunia kuwa watakuwa wanakuja mara kwa mara kujifunza hapa
kwenu,” Mhe. Prof. Juma amewaambia watumishi hao wa Mahakama Temeke.
Amesema
kuwa sifa nzuri anazozipokea hazitoki nje ya nchi tu bali pia kwa Watanzania ambao
wameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi mzuri na uliotukuka kutoka kwa
watumishi wa Kituo hicho cha aina yake katika Bara la Afrika.
Jaji
Mkuu alinukuuu ujumbe uliotolewa na Mtanzania mmoja ambaye amewataja kwa majina
ambao ni Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe Ilvin Mugeta na Naibu Msajili Mary
Moyo kwa kumwonyesha utendaji uliotukuka, upendo na moyo wa huruma, hatua
iliyochagiza shauri lake la mirathi kumalizika kwa wakati.
Akizungumza
na watumishi katika Kituo hicho, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa mafanikio
waliyonayo ni mafanikio ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kwa ujumla
huku Mahakama ya Tanzania ikiwachukulia wao kuwa ndiyo chanzo cha mafanikio
hayo makubwa.
“Hivyo
ninawashukuru sana kwa kuweza kubeba mafanikio (haya kwa) Benki ya Dunia,
Serikali na Mahakama kwa ujumla. Kwa kweli mmefanya kazi kwa mafanikio makubwa
sana, hasa katika maeneo ambayo Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania inaona
yanahitaji msukumo wa utoaji haki kama kesi zinazohusu talaka, mirathi na
watoto zinazogusa jamii ambayo ni wanyonge zaidi,” amesema.
Kabla
ya kuongea na watumishi hao, Jaji Mkuu alipata nafasi ya kutembelea maeneo
mbalimbali, ikiwemo chumba maalumu ambacho kimetengwa kwa ajili ya akina mama kuwawezesha
kunyonyesha watoto wao wachanga wanapofika katika Kituo hicho kupata huduma za
utoaji haki.
“Hiki
ni chumba ambacho Mtendaji Mkuu wa Mahakama alikuwa anasema ni nchi ya Ufaransa
tu ndiyo wanachumba cha kunyonyeshea watoto. Katika Bara la Afrika ni (Tanzania
pekee wanahuduma hii), hivyo ni sehemu muhimu na tutaendelea kuiboresha ili itoe
huduma bora zaidi,” amesema.
Akizungumza
katika kikao hicho, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani, ambaye aliambatana na Jaji Mkuu katika ziara hiyo alishindwa kuficha
furaha yake kufuatia taarifa nzuri iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Kituo
hicho kuelezea shughuli mbalimbali za kiutendaji ambazo zimefanikiwa kwa kiasi
kikubwa.
“Nina
neno moja kwa wote wanaohudumu katika Kituo hiki; hongera sana. Hapa kwa maoni
yangu, ile safari ambayo unaizungumzia na kuelekeza kuwa tuianze, Kituo hiki
hakijaanza kwa maneno. Safari ya kuelekea Mahakama Mtandao imeonekana na mimi
kwa mara ya kwanza nimepata matumaini makubwa sana. Nafahamu changamoto
mnazokabiliana nazo hasa katika kasi ya usikilizaji wa mashauri. Hali
ilivyokuwa kwa miezi miwili iliyopita ni tofauti na sasa,” alisema.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliyeambatana
na Jaji Mkuu kwenye ziara hiyo ameahidi kushughulikia changamoto ndogondogo
zinazokikabili Kituo hicho katika kutekeleza majukumu yake ili nyota yake ya
kiutendaji iendelee kung’aa sio Tanzania pekee bali pia katika Bara la Afrika
na Dunia nzima.
Awali
akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Kituo hicho, Mhe. Mugeta alimweleza Jaji
Mkuu kuwa tangu kilipoanzishwa tarehe 27 Agosti, 2021 hadi kufikia jana tarehe
19 Julai, 2022, mashauri 4,687 yamesajiliwa katika ngazi zote za Mahakama na
asilimia 68 yamesikilizwa na kuamuliwa.
Amesema
kati ya mashauri yote yaliyosajiliwa, asilimia 62, yaani mashauri 2,911 ni ya
mirathi ambapo asilimia 82 ya mashauri hayo tayari wasimamizi wa mirathi na
watekeleza wosia wameteuliwa na kuthibitishwa, mtawalia.
“Hadi
kufikia Julai 19, 2022 jumla ya mashauri 424 yalihusisha malipo ya fedha na 15,413,629,678/63
ziliwekwa katika akaunti ya mirathi ya Mahakama. Asilimia 91 ya kiasi hiki kimelipwa kwa
wanufaika kupitia mashauri 371. Bakaa iliyopo kwenye akaunti hadi tarehe ya
ripoti hii ni Tshs 1,321,830,690/22 ambayo ipo katika hatua za malipo,” amesema.
Mbali
na Jaji Kiongozi na Mtendaji Mkuu, viongozi wengine kutoka Makao Makuu
walioambatana na Mhe. Prof. Juma katika ziara yake ni Msajili wa Mahakama ya Rufani,
ambaye ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji
wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za
Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa
TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Mtendaji wa Mahakama Kuu
Masjala Kuu Bi. Maria Itala na Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey Mnemba.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno katika mkutano huo.
Afisa Tehama katika Kituo hicho cha Temeke, Bi Amina Said akifurahia jambo baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Viongozi waandamizi wa Mahakama kutoka Makao Makuu wakiongozwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, ambaye ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina (wa tatu kulia) na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi (wa kwanza kulia) wakifuatilia matukio mbalimbali katika mkutano huo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipokea kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta zawadi maalumu aliyotunukiwa na watumishi wa Kituo hicho.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni