Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania-Lushoto
Waajiriwa wapya wa Mahakama ya Tanzania wameaswa kutokubali hisia zao kutawala uamuzi wanaotoa katika utekelezaji wa majukumu ya utoaji haki kwa wananchi.
Akizungumza alipokuwa akitoa mada kuhusu masuala ya Saikolojia leo tarehe 20 Julai, 2022 wilayani Lushoto, Mshauri wa Saikolojia ya Familia, Bibi. Sadaka Gandi amesema kuwa Mahakimu wanapaswa kutotoa uamuzi kwa kufuata hisia zao wanapokuwa wanaendesha mashauri na hata wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao mengine ya kila siku wawapo kazini au hata sehemu nyingine.
Bibi Sadaka amesema, Hakimu anapokuwa kazini mambo ambayo yaliyompata siku za nyuma na kumsababishia huzuni asiyachukue wakati anapokuwa amekumbana na tukio linalofanana nayo kama msingi wa kuchukua uamuzi tofauti.
Amesema ni muhimu kudhibiti hisia na kuangalia mazingira yaliyopo katika shauri lilipo mbele ya Hakimu na kutumia busara ili kufikia uamuzi sahihi usioongozwa na mihemuko.
“Mahakama ni sehemu ambayo inahitaji mtu ambaye ni ‘grown-up and mature’ ambaye uamuzi wake lazima ulenge kuisaidia jamii kwa kupata haki na kuridhika na huduma anayopata kutoka kwa Mtumishi wa Mahakama” amesisitiza.
Bibi Sadaka ameongeza ni vema wao kama watumishi wa Mahakama ambayo ina jukumu la kuhakikisha inatoa huduma ya utoaji haki kwa wananchi wakajenga tabia ya kudhibiti hisia na mihemuko yao ili kutoa huduma nzuri kwa jamii wanayoitumikia.
Amesema wasipodhibiti hisia na mihemuko yao wanaweza kuchukua mambo yaliyowapata katika siku na miaka ya nyuma kutoa uamuzi ambao wakati mwingine matokeo yake yanaweza kuwaathiri watu wasio na hatia.
Aidha Mwanasaikolojia huyo amewaasa watumishi hao wapya kuwa makini na matendo yao katika jamii, lugha wanayotumia na watu wanashirikiana nao ili kuhakikisha kuwa wanalinda heshima yao na ya Mahakama.
Baadhi ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu wakifuatilia mada inayohusu kuvumilia sehemu za utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Mafunzo hayo yanaendelea katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama cha Lushoto.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama -Lushoto)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni