Emmanuel Oguda – Mahakama, Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma, amewapongeza Maafisa Tawala kwa kusimamia
vizuri rasilimali chache wanazopewa na Mahakama.
Mhe. Matuma ametoa pongezi hizo jana tarehe 26 Agosti,
2022 katika hafla ya kuwakabidhi vyeti Mahakimu wakazi walioshiriki zoezi la kumaliza
mlundikano wa mashauri.
“Nilipofanya ukaguzi hivi karibuni kuzunguka Mahakama
za Mwanzo 70 Kanda ya Shinyanga, kuna maeneo nimepita na kujionea mwenyewe kazi
nzuri zilizofanywa na Maafisa hawa, zikiwemo kujenga vyoo vya kisasa, kuweka
madirisha maarufu kama Aluminium, kuweka vigae na kupaka rangi kwenye baadhi ya
Mahakama za Mwanzo kwa kutumia rasilimali chache wanazopewa,” alisema.
Jaji Mfawidhi huyo alisema usimamizi mzuri wa
rasilimali hizo umeleta tija ya kazi kubwa iliyofanyika, akamtaja Hakimu wa
Mahakama ya Mwanzo Isungang’holo, Kishapu ambaye pia ni miongoni mwa watumishi
waliosimamia rasilimali vizuri. “Najivunia sana kuwa na maafisa hawa katika
Kanda ya Shinyanga,’’ alisema.
Miongoni mwa maafisa waliopokea pongezi hizo na kisha
kutunukiwa vyeti maalum walikuwa Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kahama, Bw.
Boniface Fumbe, Afisa Tawala wa Mahakama ya Wilaya Kishapu, Bi. Dotto Mabula na
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Isungang’holo Kishapu, Mhe. Sayi Mabondo.
Jaji Matuma amewataka Maafisa Tawala na Utumishi
wengine kuiga mfano kwa maafisa hao kwa kusimamia vyema rasilimali chache
wanazopewa kufanikisha Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni