· Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Simiyu, DPP, DCI washuhudia.
Emmanuel
Oguda - Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma amewatunuku vyeti vya pongezi Mahakimu watano
walioshiriki katika zoezi maalum la kumaliza mashauri ya mlundikano katika
Mahakama za Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama za Wilaya Bariadi na Maswa.
Vyeti hivyo vya pongezi vimetolewa jana tarehe 26
Agosti, 2022 katika halfa fupi ya kuwapongeza Mahakimu hao iliyofanyika katika
viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga. Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Matuma
aliwapongeza Mahakimu hao kwa moyo wao wa kujitolea pasipo malalamiko ya aina yoyote
na kufanikiwa kumaliza mashauri ya mlundikano 54 kwa muda wa majuma mawili.
“Kazi hiyo ni ya kizalendo na ya kujitolea sana’’
alisema Jaji Mfawidhi huyo. Alisema Kikosi kazi cha tatu ambacho kiliundwa kwa
ajili ya kumaliza mashauri kama hayo kwenye Mahakama za Mwanzo hakijaanza kazi
kwa kuwa hadi sasa hakuna mashauri ya mlundikano katika Mahakama za Mwanzo.
Alibainisha pia kuwa Kikosi kazi cha Mahakama Kuu
ambacho kinajumuisha Majaji watatu na Mahakimu wenye mamlaka ya ziada
kimefanikiwa kuondoa mashauri ya mlundikano 46 kati ya 56 yaliyokuwepo, hivyo
kubakiwa na mashauri 10 ambayo yanaendelea kuondolewa.
Aidha, Jaji Matuma amewataka wadau wa Mahakama, wakiwemo
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka (DPP) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI) kushirikiana bega kwa bega na Mahakama ya Tanzania katika
kumaliza mashauri kwa wakati. Akashauri changamoto ambazo zipo ziendelee
kutatuliwa ili wananchi waweze kupata haki zao kwa wakati.
Akitoa taarifa ya kikosi kazi hicho, Hakimu Mkazi
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Meatu, Mhe. Mohamed Siliti amesema wamefanikiwa
kumaliza mashauri hayo 54 kwa ushirikiano mkubwa kutoka ofisi ya Taifa ya Mashtaka
Simiyu pamoja na wadau wengine licha ya changamoto ndogondogo zilizojitokeza.
Alisema kuwa wakati wa usikilizwaji wa mashauri hayo
kikosi kazi pia kilitumia TEHAMA kwa kusikiliza jumla ya mashauri saba (7) kwa
njia ya ‘video conferencing’ ambapo jumla ya vielelezo 77 viliwasilishwa kwa
njia hiyo huku shahidi akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam.
Hakimu huyo alisema hatua hiyo iliweza kupunguza muda
na kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipa shahidi huyo iwapo angesafiri hadi
Maswa. “Kikosi kazi hiki kipo tayari muda wowote kitakapohitajika,” aliongeza
Mhe. Siliti.
Awali akiongea katika Hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema alimpongeza Jaji Matuma kwa ubunifu alioufanya ili
kumaliza mashauri ya mlundikano na akawapongeza watumishi wanaojituma na
kujitolea bila kujali stahiki za kiutumishi wala malipo kwani kujitolea huko
pia kumepunguza malalamiko katika ofisi yake.
“Nakupongeza sana Jaji Mfawidhi wa Kanda yetu ya
Shinyanga, jitihada zako za kumaliza mlundikano wa mashauri kumepunguza kabisa
yale malalamiko ya mara kwa mara katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa,’’ alisema Mhe.
Mjema. Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Dkt.
Yahaya Nawanda ambaye ameshiriki pia katika zoezi hilo. Kwa upande wake, Mkuu wa
Mkoa wa Simiyu aliwapongeza ubunifu uliofanywa Shinyanga na ameahidi kufanya
hayo katika Mkoa wake wa Simiyu.
Katika Salamu zake kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa
Mashtaka Nchini (DPP) Bw. Anthony Mwakitalu aliahidi kuendeleza ushirikiano
uliopo baina ya Mahakama na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ili
kuharakisha usikilizaji wa mashauri, hivyo kuchochea utoaji wa haki kwa haraka
kwa wananchi. Alisema atafanya kazi kwa kasi na kuleta mashataka mahakamani
huku upelelezi ukiwa umekamilika.
Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini
(DCI) Ramadhani Kingai alipongeza jitihada kubwa zilizofanywa Kanda ya
Shinyanga pamoja na mikakati iliyowekwa kumaliza mashauri ya mlundikano. Aliahidi
kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika kuhakikisha mashauri yanamalizika
kwa wakati kwa kukamilisha upeleleze kwa muda.
Tarehe 7 Februari, 2022, Mahakama Kuu Kanda ya
Shinyanga iliunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kuondoa mashauri ya mlundikano
katika Kanda hiyo na Mahakimu hao walijitolea kufanya kazi hiyo bila kujali
stahiki zao za kiutumishi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga
Mkuu wa Mashata Mkoa wa Simiyu, Mhe. Chema Maswi
akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mwanzo Isungang’holo,
Kishapu Mhe. Sayi Mabondo akipokea cheti cha pongezi wakati wa Hafla hiyo.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Maswa Mhe. Enos Misana
akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Shinyanga Mhe.
Catherine Langau akipokea cheti cha pongezi wakati wa hafla hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Sophia Mjema akiwasilisha salamu katika hafla hiyo.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Sehemu ya Mawakili wa Serikali na Mahakimu waliohudhuria hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni