Na. Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza.
Rais wa Chama cha Majaji
na Mahakimu Tanzania (JMAT), Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza amewahimiza viongozi wa chama hicho, Tawi la Mwanza
waliochaguliwa hivi karibuni kudumisha ushirikiano miongoni mwa wanachama katika
Mkoa huo.
Mhe. Kahyoza alitoa wito
huo hivi karibuni alipokuwa anafungua kikao cha JMAT katika tawi hilo kilichohudhuriwa
na Majaji wote wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza pamoja na Mahakimu wote katika Mkoa.
Aliwapongeza viongozi wapya walioteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika
chama hicho.
Rais huyo alisisitiza
kuwa ili kuweza kuweka imani kwa wanachama wake, viongozi wawe wawazi na
kuwashirikisha katika uamuzi wanaotoa. Alibainisha kuwa kwa upande wa JMAT
Taifa wamejipanga kuhakikisha chama kinawafikia wanachama wote pale walipo ili
waweze kuelewa zaidi kazi zake.
“Tukiwa kama viongozi wa
JMAT Taifa na mimi nikiwa kama Rais nitahakikisha tunakuwa wawazi kwenu ili
muwe huru na chama hiki maana chama chetu ndio jukwaa lenu la kuwasilisha maoni
yenu mbalimbali mliyonayo ili kuweza kuboresha maeneo yenye changamoto katika
utendaji kazi,” alisema Jaji Kahyoza.
Kadhalika, aliwasihi
wanachama kuangalia jinsi gani michango yao ya kila mwaka inakidhi mahitaji na
utekelezaji wa JMAT Taifa na pia kuweza kurudisha ruzuku kwenye matawi.
“Nawaomba muangalia
kiwango mnachochangia ni namna gani tunaweza kuepuka kutegemea zaidi mwajili. Tuna
michango tunayotakiwa kutuma katika chama cha Afrika Mashariki ambacho JMAT pia
ni mwanachama, kuna michango kwa ajili ya chama cha Afrika ambacho JMAT ni
mwanachama na huko pia tunatakiwa kutuma wawakilishi wetu, yote haya yanategemea
michago kutoka kwa wanachama katika matawi mbalimbali,” alisema.
Katika kikao hicho,
kulikuwa na mada za kitaaluma zilizowasilishwa kwa wanachama, ikiwemo uendesheji
wa mashauri ya mirathi katika ngazi zote za Mahakama iliyotolewa na Jaji wa
Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mhe, Wilfred Ndyasobera.
Mhe. Ndyasobera aliwakumbusha
sheria mbalimbali zinazotumika kuendesha mashauri ya mirathi mahakamani ikiwa
ni pamoja na nyaraka na fomu zinazotakiwa kujazwa na kuwasilishwa kabla na
wakati wa uendeshaji wa mashauri hayo.
“Natambua kuwa wenzangu Majaji
na Mahakimu mnafanya vizuri. Lengo la mada hii siyo kwamba hamuwezi kuyaendesha
mashauri hayo, bali ni kukumbushana tu juu ya taratibu na sheria mbalimbali
ambazo mara nyingi zinakuwa hazitumiki sana katika kuendesha mashauri ya
mirathi, mfano sheria ya The Indian
Succession Act ya mwaka 1865 na nyinginezo, hivyo naamini kupitia mada hii
tutapata kufamu au kukumbuka baadhi ya mambo,” alisema.
Mada nyingine ilihusu usimamizi
na uendeshaji wa mashauri ya madai iliyotolewa na Mhe. Kahyoza, ambaye aliwakumbusha
Mahakimu umuhimu wa kuzingatia taratibu zote za kuendesha mashauri hayo kwa
kuzingatia sheria ya utaratibu wa madai sura ya 20 na marejeo yake.
Alisema, “Ndugu zangu
nawasihi sana tunapoendesha mashauri haya tufuate sheria inavyotaka, tujiepushe
na hizi amri za kuahirisha mashauri kwa kuyataja (mention), kwani ukiangalia
sheria nzima hakuna sehemu ambayo inaonyesha kuwa unaweza kupanga shauri kwa
ajili ya mention. Na hii mention, mention ndio inapelekea
kuchelewa kumaliza mashauri kwa wakati na hivyo kukuta mnachelewesha haki za
watu pasipo sababu za msingi. Tubadilike na tuanze kufuata sheria inavoelekeza.”
Kadhalika, Mhe. Kahyoza aliwakumbusha
namna bora ya kudhibiti na kuendesha mashauri kwa kupanga ratiba ambayo itakuwa
ni halisi kwa Mahakimu kuwepo mahakamani na hivyo kuhakikisha mashauri
yanamalizika kwa wakati.
Katika kikao hicho, Mwenyekiti
wa JMAT Mkoa kwa kushirikiana na Katibu wake walipitisha maazimio mbalimbali
yaliyokubaliwa na wanachama wote ikiwemo kuunda kamati mbalimbali kwa ajili kuendesha
shughuli za chama mkoani Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni