Na Tiganya Vincent-Mahakama, Chamwino
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea
na uteuzi wa Majaji wanawake ili katika kuelekea kwenye usawa wa Kijinsia
katika Mhimili huo wa utoaji wa haki nchini.
Amesema
lengo lake ni kutaka kuwepo hamsini kwa hamsini kwa upande wa Majaji katika
Mahakama ya Tanzania.
Mhe.
Samia ametoa kauli hiyo leo Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma mara baada ya
kumaliza kuwaapisha Majaji 22 wa Mahakama Kuu aliowateua mapema Mwezi huu.
Amesema
Majaji wanawake licha kusoma na wanaume lakini wao ni waadilifu, wachapakazi na
wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao wanazingatia mila na desturi na utamaduni
wa Kitanzania.
“Pamoja
na kusoma wote wanawake na wanaume, lakini wanawake ni waadilifu na wanapohukumu
wanazingatia mila na desturi za Kitanzania…wanawake niliwateua nendeni
mkachape kazi msiniangushe,”amesisitiza.
Aidha
Rais Samia amesema kuwa alipokea mapendekezo ya majina 71 ambapo kati yao
walitakiwa kuteuliwa Majaji 47 lakini kutokana
na ufinyu wa bajeti ameanza na uteuzi wa Majaji 22 na waliobaki wataendelea
kuwa katika kanzidata wakati ukifika nao watateuliwa.
Kwa
upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia kwa kuongeza idadi ya Majaji hao ambao
watasaidia kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.
Amesema
Rais Samia tangu alipoingia madarakani mwaka jana aliteua 21 wa Mahakama Kuu na
kuteua jumla ya Majaji 9 wa Mahakama ya Rufani na kufikisha idadi ya Majaji wa
Rufani 25.
Amesema
idadi hii kubwa imeiwezesha Mahakama kuweza kuunda majopo nane (8) ambao ni
hatua kubwa ya kupunguza muda ambao rufani zinadumu kabla ya kukamilika.
Mhe.
Prof. Juma amesema uteuzi wa hivi karibuni na baadaye kuapishwa kwa Majaji
wapya 22 umefanya kwa kipindi cha miezi 15 ya uongozi wa Rais Samia kufikisha jumla
ya Majaji 52 ambao amewateua ikiwa wa
Mahakama ya Rufani 9 na Mahakama Kuu 43.
Amesema
ongezeko la Majaji hao 22 litasaidia kupunguza wastani wa mzigo wa mrundikano
wa mashauri mahakamani ambapo idadi ya Majaji Mahakama Kuu imeongezeka kutoka
78 hadi 100 pamoja na Jaji Kiongozi.
Prof.
Juma amesema kufikisha idadi hiyo ya Majaji 100 kutapunguza wastani wa mzigo wa
mashauri anayobeba kila Jaji kutoka mashauri 340 hadi 265.
Jaji
Mkuu huyo ameongeza kuwa uteuzi uliofanywa na Rais umezingatia usawa wa kijinsia
ambapo kabla ya uteuzi, Mahakama Kuu
ilikuwa na Majaji wanawake 27 kati ya 78 ambao walikuwa sawa na asilimia 35
Amesema
baada ya uapisho wa Majaji 22, idadi ya wanawake na kuwa sawa na asilimia 37 ambayo
ni hatua kubwa sana katika kuzingatia usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa wote.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa neno wakati wa hafla fupi ya kuwaapisha Majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 29 Agosti, 2022 Ikulu Chamwino Jijini Dodoma, kulia kwake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania mara baada ya kuapishwa Ikulu Chamwino Jijini Dodoma, wengine ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa tatu kushoto), Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kulia), Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro (wa pili kushoto), Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (wa pili kulia), Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Kattanga (wa kwanza kulia) na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Kamishna wa Tume ya Maadili, Mhe. Sivangelilwa Mwangesi (wa kwanza kushoto)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni