Jumanne, 30 Agosti 2022

UPATIKANAJI WA MAJAJI NI SHIRIKISHI: JAJI MKUU

Na Faustine Kapama, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 29 Agosti, 2022 alielezea kwa kina utaratibu shirikishi uliotumiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kupata majina ya Watanzania 22 walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akizungumza katika tukio la kihistoria la kuwaapisha Majaji 21 kati ya 22 liliofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Mhe. Prof. Juma alieleza kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama imejiwekea utaratibu wa muda mrefu wa kuwaomba wadau wa Mahakama na katika sekta za sheria kuwasilisha majina ya Watanzania wenye sifa za kikatiba, uwezo, uzoefu, maadili mema na tabia njema kuweza kujadiliwa na kisha kupendekezwa kwa Rais.

“Wadau wamepewa uhuru kuwasilisha majina kutoka ndani ya Taasisi zao, hata kutoka nje ya Taasisi zao, ilimradi wanaopendekezwa wana sifa za Kikatiba, uwezo, uzoefu, maadili mema na tabia njema, kuweza kujadiliwa na Tume, kisha kupendekezwa kwa Rais. Mantiki ya kuwashirikisha wadau ni kufanya zoezi la kuwapata Majaji kuwa shirikishi na kwa kutambua kuwa wadau wa Mahakama na wa sekta ya sheria ndio wanaowafahamu wanaostahili kupendekwa kwa uteuzi wa kuwa Jaji,” alisema.

Jaji Mkuu aliwaeleza Watanzania katika salamu zake za shukrani kwa Rais katika tukio hilo lililokuwa linarushwa bubashara na Televisheni ya Taifa kuwa katika zoezi la kuwapata Majaji 22, wadau wa Mahakama na wa sekta ya sheria waliwasilisha Tume jumla ya majina 232 yaliyojumuisha kutoka Mahakama 87, Mawakili wa Serikali 30, Vyuo 22, Mawakili wa Kujitegemea 53 na Wizara na Taasisi za Umma majina 40.

“Baada ya usaili wa ana-kwa-ana (oral interview) na usaili wa kuandika (written interview) na kukagua machapisho au hukumu (assessment of written works), idadi ikapungua hadi 57. Hawa walitoka katika Taasisi (mbalimbali) ikiwemo Mahakama 20, Mawakili wa Serikali 23, Vyuo wanne (4), Mawakili wa Kujitegemea watano (5) na Wizara na Taasisi za Umma watano (5), (hivyo) kamati iliwasilisha Tume majina 57 kwa ajili ya kuyajadili,” alisema.

Mhe. Prof. Juma alifafanua kuwa baada ya kuyajadili majina hayo 57 pamoja na majina yaliyokuwa ndani ya Kanzi-Data, Tume ilipitisha jumla ya majina 71 ambayo ilimshauri Rais ateue Majaji 47 au kadri atakavyoona inafaa ili kukidhi mahitaji ya Mahakama ya Tanzania na kutokana na vigezo alivyovitumia, Rais aliteua Majaji 22 kutoka katika orodha aliyoshauriwa na Tume.

Aliwahakikishia wateule wote 22 kuwa wanazo sifa za kikatiba za kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu, ambazo zimetajwa katika Ibara 109 (6) na (7), ikiwemo kuwa na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu kinachotambuliwa na Mamlaka ya Ihibati Tanzania, kuwa Hakimu, kufanya kazi katika Utumishi wa Umma ukiwa na sifa za kufanya kazi ya uwakili au ni Wakili wa Kujitegemea, kuwa na sifa za kusajiliwa kuwa Wakili na kuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usio pungua miaka kumi.

“Kwa niaba ya Tume ya Utumishi wa Mahakama napenda kuwapongeza kwa imani ambayo mamlaka ya uteuzi (Rais) imeonyesha kwenu kwa niaba ya Watanzania wote. Niwahakikishie kuwa kila mmoja wenu ana sifa zote za Kikatiba na pia mmekidhi vigezo vyote vya uteuzi. Mnao uwezo, mnayo maadili na tabia njema kuweza kuaminiwa kufanya kazi za Jaji wa Mahakama Kuu,” alisema Jaji Mkuu.

Uteuzi huo unaongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka 78 hadi 100 pamoja na Jaji Kiongozi. Kuongezeka kutoka 78 hadi 100 kutapunguza wastani wa mzigo wa mashauri anayobeba kila Jaji kutoka mashauri 340 hadi 265, hivyo kufanya mzigo kwa kila Jaji kupungua kwa mashauri 75.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uapisho huo ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (kulia aliyekaa) jana tarehe 29 Agosti, 2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Sehemu ya Majaji wapya (picha ya juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. 

Sehemu nyingine ya Majaji wapya (picha ya juu na chini) mara baada ya kuapishwa.

(Picha na Innocent Kansha- Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni