Ijumaa, 19 Agosti 2022

MAHAKAMA MKOANI MOROGORO YATOA ADHABU MBADALA KWA WAFUNGWA 125

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro.

Mahakama mkoani Morogoro imetoa adhabu mbadala kwa wafungwa 125, jambo linalochangia kupunguza mrundikano magerezani.

Hayo yamebainishwa na Kiongozi wa Huduma za Uangalizi (Probation Officer) wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Yusuf Ponera alipokuwa anaongea na Mwandishi wetu kwenye mahojiano maalumu aliyoyafanya ofisini kwake leo tarehe 19 Agosti, 2022.

 “Ofisi yangu imekabidhiwa jumla ya wafungwa 125 wa adhabu mbadala kuanzia mwezi Januari 2022 mpaka Agosti mwaka huu ambao kati yao wafungwa 93 ni wenye jinsia ya kiume huku wafungwa 32 wakiwa ni jinsia ya kike,” amesema.

Alifafanua kuwa idadi hiyo imegawanyika katika makundi mawili ambapo wafungwa wanne (4) wamewekwa kwenye malezi na uangalizi ambao ni wazee na wanafunzi.

Amesema wafungwa 121 wanatumikia adhabu zao kwa kufanya shughuli za kijamii ikiwemo usafi na kutunza mazingira katika ofisi za umma walizopangiwa, kazi ambazo wanafanya bila malipo kwa muda wa saa nne mpaka vifungo vyao vitakapoisha.

“Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama nisipotoa shukurani kwa Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri tunaoupata. Uwepo wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro umerahisisha utendaji kazi wa ofisi yangu,” Bw .Ponera amesema.

Amebainisha kuwa uwepo wa Kituo hicho umeambatana na utoaji elimu kwa umma, jambo ambalo linawarahisishia kazi hata wanapoenda kufanya utafiti wa mfungwa anayekidhi vigezo vya adhabu mbadala wanakuta jamii ina uelewa na hutoa ushirikiano mzuri.

Naye Miraji Hasani ambaye alianza kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kuanzia tarehe 5 Juni, 2022 ambaye amekuwa akifanya usafi katika Zahanati ya Vikenge Wilayani Mvomero Morogoro amesema kupitia adhabu hiyo amejifunza jinsi ya kushirikiana na jamii.

Kadhalika, mfungwa huyo amesema kifungo hicho kimemuadabisha kwani wakati mwingine hujisikia aibu pale ndugu na jamaa zake wanapomkuta maeneo yale akitumikia, hivyo amejifunza na kuahidi kuwa raia mwema mara atakapomaliza kutumikia adhabu yake.

Sheria ya huduma kwa jamii kifungu cha 6 ya mwaka 2002 inamtaka mfungwa kufanya kazi za kijamii bila malipo. Mkoani Morogoro wafungwa wanaotumikia adhabu mbadala wamekuwa wakifanya usafi katika taasisi za umma huku wenye taaluma wakitumikia taaluma zao katika ofisi za umma.

Ikumbukwe kuwa mara baada ya kufunguliwa kwa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro mwishoni mwa mwezi Novemba 2021, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Paul Ngwembe alikutana na kuzungumza na wadau wa Mahakama ambapo miongoni mwa ajenda ilikuwa namna walivyojipanga kupunguza mrundikano magerezani mkoani hapa.

Mhe. Ngwembe alibainisha kuwa Mahakama itatoa elimu ya sheria kwa wananchi na kutumia adhabu mbadala kwa mujibu wa sheria kwa vile Serikali inatumia fedha nyingi kuhudumia wafungwa gerezani na hupoteza mapato mengi kwani wakati mwingine mfungwa awapo gerezani hazalishi na kuingizia Serikali kipato.

Kiongozi wa Huduma za Uangalizi wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Yusuf Ponera akifafanua jambo wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wetu.
Kiongozi wa Huduma za Uangalizi wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Yusuf Ponera (kushoto) akifanya mahojiano na wanafamilia wa mtuhumiwa ili kujua kama anastahili adhabu mbadala.
Afisa wa Huduma za Uangalizi Mkoa wa Morogoro, Bi. Imelda Aloyce (aliyesimama) akitoa elimu kwa wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.
Mti uliopandwa na kuhudumiwa na mfungwa wa kifungo cha nje miaka ya nyuma.
Mti wa matunda uliopandwa na kutunzwa na mfungwa wa kifungo cha nje.
Bustani ya mbogaboga iliyopandwa na mfungwa wa kifungo cha nje. Mboga hizo hugawiwa pasipo na malipo kwa watu wenye uhitaji.
Eneo la mbele ya  Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ambalo limepandwa miti ambayo inahudumiwa na wafungwa wa adhabu mbadala.

Muonekano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ambako pia ofisi za huduma za uangalizi zinapatikana.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Mhe. Paul Ngwembe akiwa katika moja ya mikutano na wadau mbalimbali wa Mahakama na wananchi kuzungumzia walivyojipanga kupunguza mrundikano magerezani.

Sehemu ya wadau wa Mahakama Kanda ya Morogoro wakiwa kwenye kikao kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni