Alhamisi, 18 Agosti 2022

MKUU WA MKOA WA DODOMA ATEMBELEA UJENZI WA MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA

•Aimwagifa sifa Mahakama uboreshaji miundombinu, Tehama

Na Arapha Rusheke, Mahakama-Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule leo tarehe 18 Agosti, 2022 ametembelea ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania na kupongeza juhudi zinazofanywa na Mhimili huo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya majengo na matumizi mazuri ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo yamerahisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi.

Amesema hatua hiyo pia inaondoa malalamiko yasiokuwa ya lazima na kujenga imani ya wananchi katika utoaji na uboreshaji wa huduma za haki. Akizungumzia ujenzi huo, Mhe. Senyamule amepongeza mapinduzi makubwa yanayofanyika kwani jengo hilo ni kitu cha fahari kwa Tanzania.

“Jengo hili ni la kihistoria sio katika nchi yetu tu bali hata nje ya nchi. Nchi yetu ina mihimili mitatu, nafurahi kuona Mhimili wa Mahakama umefanikiwa sana kuboresha huduma zake hasa katika matumizi ya TEHAMA. Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassani kwa juhudi hizi za kuwezesha Mhimili huu kutekeleza majukumu yake kikamilifu,” alisema.

Mkuu wa Mkoa huyo ambaye aliambatana na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ameahadi kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha jukumu kuu la utoaji haki kwa wananchi linafanyika kama inavyotakiwa. “Ofisi yangu ipo wazi muda wowote, tutashirikiana na Mahakama bega kwa bega muda wowote, saa yeyote mimi nipo, msisite kunishirikisha kama Mahakama inahitaji msaada wangu,” aliwaambia viongozi wa Mahakama walioambatana naye.

Viongozi walioambatana na Mkuu wa Mkoa katika ziara yake walikuwa Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Adam Mambi, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dodoma, Mhe. Sylvia Lushashi na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Dodoma, Bw. Sumera Manoti.

Akiwa katika eneo la ujenzi, Mhe. Senyamule alipokea taarifa zilizowasilishwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu inayoonyesha kuwa gharama mpaka kukamilika kwa jengo hilo itakuwa billioni   129 za Kitanzania.

Naye Mhandisi alimweleza Mkuu wa Mkoa huyo kuwa mpaka kufikia leo tarehe 18 Agosti, 2022 ujenzi umefkia asilimia 65 na mkandalasi anaendelea na kazi za umaliziaji (finishing). Kadhalika, alisema “lifti” zote 17 zilizopo katika jengo hilo zitaanza kuwekwa kuanzia wiki ijayo. Amemhakikishia kiongozi huyo wa Serikali kuwa ujenzi utakuwa katika sehemu nzuri ifikapo mwezi Desemba ili kukabidhi jengo hilo.

Kabla ya kutembelea ujenzi huo, Mkuu wa Mkoa huyo alifika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuonana na baadhi ya wadau wa Mahakama na kujionea sehumu maalumu zilizotengwa ikiwemo Mahakama ya Watoto na Chumba cha kunyonyeshea Watoto.

 Hali ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama kwa sasa (Picha juu na chini).

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha (picha juu na chini) akieleza jambo katika eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akionyeshwa muonekano wa jinsi jengo litakavyokuwa baada ya kumalizika.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akielekea kuona maendeleo ya ujenzi.
Mhandisi Queen akifafanua jambo kuhusu ujenzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akieleza jambo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mh. Rosemary Senyamule (katikati) na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt Adam Mambi (wapili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mahakama na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni