Jumatano, 17 Agosti 2022

SHAMRA SHAMRA ZATAWALA MAPOKEZI YA BASI JIPYA MAHAKAMANI MOROGORO

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro.

Watumishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro hawakuamini macho yao walipofika asubuhi na mapema katika viwanja vya Mahakama na kukuta basi jipya na la kisasa likiwa limepaki pembeni, tukio lililopokelewa kwa shamra shamra za kila aina.

Basi hilo lililetwa na Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bi. Dativa Michael ambaye alikabidhiwa jijini Dar es Salaam. 

Bi Michael naye hakuamini macho yake alipofika ndani ya basi hilo baada ya kukabidhiwa. “Kwa kweli ni basi jipya na la kisasa kabisa, tunashukuru sana kwa neema hii iliyofunuliwa kwetu leo,” alisisika Bi Michael akisema.  

Ilikuwa majira ya asubuhi wakati watumishi walipobaini kuwa ndoto yao imegeuka kuwa kweli pale Bi Michael alipokabidhi basi hilo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe ili lianze kutumika kurahisisha usafiri kwa watumishi wa Mahakama hiyo.

Baada ya kuingia ndani ya basi hilo, Jaji Mfawidhi huyo hakusita kuonesha furaha yake kutokana na uzuri aliojionea wa basi hilo. Baadaye alizindua matumizi ya basi hilo na kuwaeleza watumishi wote kuwa kuwahi kufika kazini pia ni njia mojawapo ya kurahisisha utoaji huduma kwa wateja. Aliwasihi kulitunza vyema ili litumike kwa muda mrefu na kuwahakikishia mambo mazuri zaidi yataendelea kufanywa na Mahakama.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi kwa njia ya mtandao, Mtendaji wa Mahakama katika Kanda hiyo, Bw. Ahmed Ng’eni ambaye yupo rikizo aliipongeza menejimenti na uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kusikiliza kilio chao kutatua changamoto ya usafiri. Alisema hapo awali baadhi ya watumishi walilazimika kupanda zaidi ya magari mawili ili kufika kazini.

Naye mnufaika wa usafiri huo, Msaidizi wa kumbukumbu, Bi. Herieth Mwingira alisema kuwa kwa sasa makali ya maisha yatapungua kwani basi hilo limeokoa kiwango kikubwa cha nauli alichokuwa akitumia ili kufika kazini kwa vile awali alilazimika kupanda magari mawili wakati wa kwenda na kurudi kutoka ofisini.

Basi hilo ni miongoni mwa mabasi mnne ambayo Serikali ilitoa fedha yaweze kununuliwa ili kurahisisha na kuboresha huduma za usafiri kwa watumishi wa Mahakama, Morogoro ikiwa ni miongoni mwa Kanda zilizonufaika na magari hayo.

Hivi karibuni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabliel alipokea magari manne toka kwa Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Mahakama ambaye aliyanunua baada ya kupatiwa fedha na Serikali.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel alinukuu jitihada zinazofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma za kuboresha huduma za Mahakama kwa jamii na hata kwa watumishi wake.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe akionesha ufunguo wa basi lililokabidhiwa kwake kwa ajili ya kuboresha usafiri wa watumishi katika Mahakama hiyo.

Basi likiwa limepaki nje ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

 

Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bi. Dativa Michael akiwa ndani ya basi wakati alipoenda kulipokea.

Watumishi wa Kituo hicho wakiingia ndani ya basi ili kulizindua.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Paul Ngwembe akiongoza watumishi wa Mahakama kuteremka ndani ya basi baada ya uzinduzi. Anayemfuatia nyuma (picha ya juu) na wa pili kushoto (picha ya chini) ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe Sylivester Kainda.  Walio ndani ya basi (picha ya juu na chini) ni watumishi wa Mahakama.


Shamra shamra za uzinduzi wa basi jipya (picha juu na chini) zikiwa zimepamba moto.















 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni