Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 17 Agosti, 2022 ametembelewa na kufanya mazungumzo na Rais wa Jumuiya ya Majaji wanaojihusisha na Sheria za Ukimbizi na Uhamiaji Kanda ya Afrika, Mhe. Dunstan Mlambo.
Mhe. Mlambo ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Jimbo la Gauteng, Africa ya Kusini amekutana na Jaji Mkuu ofisini kwake jijini Dar es Salaam lengo mojawapo likiwa ni kujadili kuhusu Mkutano wa Jumuiya hiyo unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha mnamo Novemba mwaka huu.
Katika mazungumzo yao, Jaji Mlambo amemueleza Mhe. Prof. Juma kuwa, Mkutano wa Jumuiya hiyo (International Association of Refugee and Migration Judges (IARMJ) unatarajiwa kufanyika tarehe 14 hadi 18 Novemba mwaka huu katika Hoteli ya Gran Mellia jijini Arusha huku akimuomba Jaji Mkuu ushiriki wake pamoja na wa Majaji wa Mahakama ya Tanzania katika Mkutano huo.
“Napenda kukushukuru Mhe.kwa kukubali kuonana na wewe siku ya leo, moja ya malengo ya kukuonana nawe ni pamoja na kukujulisha kuhusu mkutano wetu unaotarajia kufanyika Novemba mwaka huu; hivyo naomba ushiriki nasi pamoja na Majaji wa Mahakama ya Tanzania ili tuweze kubadilishana uzoefu kwa kushiriki katika mijadala mbalimbali itakayojiri katika mkutano huo,” amesema Mhe. Mlambo.
Naye Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amemuhakikishia Jaji Mlambo kuwa, atashiriki katika Mkutano huo pamoja na Majaji wengine wapatao 30 kutoka Mahakama ya Tanzania.
“Naomba nikuhakikishie kuwa, nitashiriki katika mkutano huo pamoja na Majaji wengine kutoka Mahakama ya Tanzania ili kubadilishana uwezo na kufahamu zaidi mnafanya nini,” amesema Jaji Mkuu.
Mkutano huu utahudhuriwa na Majaji wapatao 30 kutoka Tanzania pamoja na Majaji mbalimbali kutoka katika nchi za Afrika na nje ya Bara la Afrika na unalenga katika kubadilishana uzoefu kuhusu namna ambavyo Mahakama zinavyoshughulikia mashauri ya Uhamiaji na watu na wale wanaoomba kupewa hifadhi.
Mbali na hilo, Mhe. Prof. Juma amemueleza Jaji Mlambo kuhusu utaratibu uliopo ndani ya Mahakama ya Tanzania wa kupandisha hukumu mbalimbali zinazotolewa na Majaji katika Mfumo wa kutunza uamuzi/hukumu wa Mahakama ujulikanao kama ‘TanzLII’ na kuongeza kuwa, ni vyema kuangalia uwezekano wa kufahamu zaidi jinsi Jumuiya hiyo inavyohifadhi hukumu zake kupitia mfumo wa ‘Africa LII’ kama alivyodokeza Jaji Mlambo katika mazungumzo na Jaji Mkuu.
Awali, katika mazungumzo ya Viongozi hao, Jaji Mlambo amemueleza Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma kuwa,
Jumuiya hiyo ya kimataifa ambayo inahusika katika kuwajengea uwezo Majaji
katika kusikiliza mashauri ya maombi ya watu kupewa hadhi ya ukimbizi ina miaka
20 sasa tangu kuanzishwa kwake na ina matawi manne (chapters) ambayo ni Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Rais wa Jumuiya ya Majaji wanaojihusisha na Sheria za Ukimbizi na Uhamiaji Kanda ya Afrika, Mhe. Dunstan Mlambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni