Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza jana tarehe 16 Agosti, 2022
amewakabidhi watumishi basi jipya aina ya TATA lililonunuliwa na Mahakama ya
Tanzania ili kutatua changamoto ya usafiri iliyokuwa inawakabili.
Makabidhiano ya basi hilo
jipya na la kisasa yalifanyika katika viwanja vilivyopo katika Kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki mara baada ya kukutana na watumishi wa Mahakama hiyo kwenye
majadiliano yaliyolenga kutambua majukumu ya kila kada na kuboresha utendaji
kazi za kimahakama kwa wananchi.
Bus hilo ambalo tayari
limeanza kutoa huduma, hivyo kuwaondolea watumishi hao adha ya usafiri ya
kuwahi ofisini na pia kurudi nyumbani ni miongoni mwa magari ya aina hiyo manne
yaliyonunuliwa na Mahakama ya Tanzania hivi karibuni.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa
fedha za kununua magari manne kwa ajili ya usafiri kwa watumishi wake.
Prof. Ole Gabriel alitoa
pongezi hizo jijini Dar es salaam hivi karibuni wakati akipokea magari hayo
kutoka kwa Mkurugenzi wa Ununuzi na Ugavi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles
Chale. Mtendaji Mkuu huyo alisema magari hayo yatapelekwa katika Kanda nne za
Mahakama ambazo ni Morogoro, Shinyanga, Mwanza na Musoma.
Kabla ya makabidhiano ya
basi hilo, Jaji Mfawidhi huyo aliendesha majadiliano na watumishi wote wanaohudumu
katika Kituo hicho ambapo amewakumbusha kuzielewa hadidu rejea za kila kada ili
kuweza kutoa huduma za kimahakama na kiutawala kwa viwango vinavyokubalika.
“Ni vizuri kwa kila mmoja
wetu kujua majukumu yake kulingana na hadidu rejea za kufanya kazi ndani ya
jengo hili. Pia tunatakiwa kutimiza matarajio ya wananchi ili tuweze kupimwa, kwani
mwisho wa siku kila mmoja humu atapimwa utendaji kazi wake kwa kupitia kadi
maalumu. Tuwe tayari kubadili utamaduni wetu wa utendaji kazi kutoka ule tuliokuwa
nao hapo zamani,” alisema.
Akichangia katika
majadiliano hayo, Msaidizi wa Sheria wa Jaji, Mhe. Geofrey Ndege alisema moja
ya vitendo vinavyoweza kuondoa imani kwa jamii ni kuvujisha uamuzi na ushauri
wa kisheria unaotolewa kwa Majaji kwa watu wasio stahili, hivyo akashauri watumishi
kujiepusha na mambo kama hayo.
Majadiliano hayo
yaliwawezesha watumishi kutambua kile ambacho wanatakiwa kutimiza na kile kinachotarajiwa
kutoka kwao katika kuwahudumia wateja wote wa ndani na nje ya taasisi.
Aidha majadiliano hayo
yameweza watumishi kuwa na mwanga jinsi ambavyo wanastahili kufanya kazi katika
jengo hilo, hivyo kuwajengea uelewa wa pamoja wa nini cha kufanya na kuacha
tamaduni gani.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza (katikati) akiwa na baadhi
ya watumishi mara baada ya kuwakabidhi basi hilo jipya.
Baadhi ya madereva wakiwa
katika picha ya pamoja mbele ya basi hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni