Na Ibrahim Mgallah, Mahakama Kuu-Mbeya
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dkt. Lillian Mongella amewasihi
watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo kutoa huduma bora kwa wateja ili
kufikia maono ya taasisi ya upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati.
Mhe.
Jaji Mongella, ambaye alimwakilisha Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda hiyo, Mhe. Rose Ebrahim alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anafungua mafunzo elekezi
yaliyowaleta pamoja watumishi wa kada mbalimbali waliwemo walinzi, madereva,
wasaidizi wa kumbukumbu, wahudumu wa ofisi, makatibu mahsusi na Maafisa
Utumishi au Tawala.
Aliwakumbusha
watumishi hao kuwa sifa ya taasisi inaweza kuharibiwa na mtu mmoja asiyetoa
huduma nzuri kwa wateja, hiuvyo kila mtumishi anatakiwa kutoa huduma bora kwa
wateja ili kuendeleza sifa nzuri ya Mahakama. Kadhalika, aliwaomba watumishi hao
kusikiliza kwa makini yote yatakayofundishwa na kuyafanyia kazi mara baada ya
mafunzo.
Mafunzo
hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Mbeya yenye mada kuu
inayohusu Huduma kwa Mteja ni mwendelezo wa mafunzo yanayofanywa na Mahakama
ili kuwajengea uwezo watumishi wake.
Akiwasilisha
mada katika mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. David Ngunyale amesema
kila mtumishi anatakiwa kutoa huduma bora kwa namna ambayo mteja ataridhika. “Nawasihi
mtoe huduma bora kwa namna ambayo wewe utaridhika na mteja ataridhika kwenye huduma
aliyoipata,” Jaji Ngunyale aliwambia watumishi hao.
Vile
vile akawataka watumishi hao kufanya kazi kwa amani na upendo na kuwasihi kuridhika
na kile wanachikipata na kwamba wanatakiwa kutoa huduma kwa usawa na kuzingatia
hali ya mtu. Aidha, Mhe. Ngunyale aliwakumbusha watumishi kutunza siri wanapotekeleza
majukumu yao.
Akihitimisha mafunzo hayo, Kaimu Mtendeji wa Mahakama Kuu Mbeya, Bw. Moses Luwoga aliishukuru kamati ya mafunzo kwa kuandaa mafunzo hayo. “Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yataongeza ufanisi katika kuwahudumia wateja wanaofika kupata huduma mahakamani,” alisema. Pia aliwashukuru watumishi na mkufunzi kwa utayari wao wa kuhudhuria mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni