Na Francisca Swai- Mahakama, Musoma.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Musoma wameushukuru uongozi wa Mahakama kwa kutatua changamoto ya
usafiri baada ya kupatiwa basi jipya na la kisasa, tukio lililoibua furaha na
kupokelewa kwa nderemo na vifijo.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na watumishi
hao mara baada ya kupokea basi hilo lililonunuliwa na Mahakama ya Tanzania.
Wamesema basi hilo litatatua changamoto waliyokuwa nayo ya muda mrefu ya
ukosefu wa usafiri wa uhakikia.
Kwa mujibu wa watumishi hao, kumekuwepo na
changamoto ya usafiri hasa baada ya kuhamia katika Jengo la Mahakama Kuu Musoma
tangu Desemba 2019 ambalo lipo umbali wa kilomita nane kutoka Musoma mjini.
Akiongea na watumishi hao katika ghafla
hiyo fupi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amewaasa watumishi kushirikiana kulitunza
basi hilo ili liweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia katika usafiri kufika
kazini kwa wakati.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Musoma,
Bw. Festo Chonya amesisitiza utumiaji na utunzaji mzuri wa basi hilo ambalo
limetatua kilio cha muda mrefu kwa watumishi hao. Alisema uwepo wa basi hilo
litakalowezesha watumishi kufika kazini kwa wakati uwe ni chachu ya kujituma
ili kuongeza tija katika shughuli za utoaji haki kwa wakati.
Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa
fedha za kununua magari manne kwa ajili ya usafiri kwa watumishi wake.
Prof. Ole Gabriel alitoa pongezi hizo jijini
Dar es salaam wakati akipokea magari hayo kutoka kwa Mkurugenzi wa Ununuzi na
Ugavi wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Charles Chale. Mtendaji Mkuu huyo alisema magari
hayo yatapelekwa katika Kanda nne za Mahakama ambazo ni Morogoro, Shinyanga,
Mwanza na Musoma.
Alisema upatikanaji wa magari hayo ni jitihada za Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma kuona watanzania wanapata haki kwa wakati, hivyo kama watumishi wakiwa na usafiri wa uhakika itasaidia kutekeleza azima hiyo.
Prof Ole Gabriel aliwataka watumishi na madereva watakaokabidhiwa magari hayo kuyatunza ili yaweze kufanya kazi kwa muda mrefu na kusaidia katika uendelezaji wa mnyororo wa utoaji haki kwa wakati.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni