Na Emmanuel Oguda - Shinyanga
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi,
Mhe Katarina Mteule hivi karibuni alikutana na wadau wa Mahakama hiyo Kanda ya Shinyanga
na kusisitiza ushirikiano ili kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Mhe. Revokati alieleza lengo kuu la kukutana na wadau
wa Mahakama ya Kazi ili kupata maoni yao pamoja na kushirikiana katika
usimamizi wa Sheria za Kazi na Haki Kazi kwa ujumla.
“Zamani Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi ilisikiliza
mashauri ya kazi ambapo Jaji alikuwa akitoka Makao Makuu Dar es Salaam, lakini kwa
sasa Mahakama Kuu zote katika ngazi ya Kanda zinaendesha mashauri hayo kwa
kutumia Majaji wa Mahakama hizo,” alisema.
Jaji Mteule alieleza katika kikao hicho kilichofanyika
katika ukumbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya
Kazi imeamua kukutana na wadau kama hatua ya Mahakama ya Tanzania kutekeleza
Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano (2022/2021 – 2024-2025) unaosisitiza
kurudisha imani kwa wananchi na ushirikishwaji wa Wadau.
“Zipo changamoto nyingi kwenye mashauri ya kazi,
kupitia kwenu wadau wetu yapo mambo ambayo tutashirikishana kwa pamoja ili
tuendelee kuongeza ufanisi katika usikilizwaji wa mashauri hayo,” alisema.
Awali akifungua kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athumani Matuma alipongeza jitihada za
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa kuona umuhimu wa kushirikisha wadau katika
usikilizaji wa mashauri ya kazi. “Tukitatua migogoro ya kazi kwa haraka na kwa
haki tutakuza uchumi wa Nchi,” alisema.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Mhe. Elizabeth Nyembele alisisitiza utunzaji mzuri wa majalada, hasa kwenye ofisi
za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), kwa kuainisha mwaka shauri
lilipomalizika ili kuondoa usumbufu pale linapohitajika Mahakama Kuu, hatua
itakayosaidia kumaliza shauri husika kwa wakati.
Kwa upande wao, wadau walipongeza hatua ya Mahakama hiyo
kuwashirikisha katika kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali yanayohusu
changamoto katika usikilizaji wa mashauri ya kazi. Wadao hao wameshauri iangaliwe
namna ya kurasimisha na kutoa mwongozo au kanuni zitakazodhibiti wawakilishi binafsi
katika mashauri ya kazi ili yamalizike kwa wakati.
Wadau walioshiriki katika kikao hicho walitoka katika Ofisi
ya Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Makatibu wa Vyama vya Wafanyakazi Mkoa na
Chama cha Mawakili Shinyanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni