Jumatatu, 15 Agosti 2022

MADALALI WASAMBAZA NYARAKA ZA MAHAKAMA WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO YA KAZI

 Na Mary Gwera, Mahakama

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ametoa rai kwa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama nchini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa kwa Mahakama kutokana na ukiukwaji wa taratibu na kanuni za utendaji kazi wao.

Akizungumza wakati akifungua Mafunzo kwa kundi la tisa (9) la wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama leo tarehe 15 Julai, 2022 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa, baadhi ya Maafisa hao wamekuwa wakikiuka taratibu za kazi hali inayosababisha tuhuma kurudishwa kwa Mahakama ili hali Mhimili huo ukiwa umeshatekeleza kazi yake ya kutoa uamuzi/amri za mashauri mbalimbali.

“Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mahakama ndio wanaotekeleza amri za Mahakama, baada ya Mahakama kutoa amri wao ndio wana wajibu wa kuitekeleza hiyo amri kama ni kubomoa nyuma, kukamata mali na kuuza na kadhalika, hivyo ni muhimu waelewe na kuzingatia sheria na taratibu za utendaji kazi wao ili Mahakama iondokane na malalamiko mbalimbali yanayotolewa,” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.

Ameeleza kuwa, kuanzishwa kwa mafunzo hayo ni moja kati ya sehemu ya uboreshaji wa huduma unaoendelea katika mhimili wa Mahakama lengo likiwa ni kuleta taswira chanya ya Mhimili huo kwa wananchi.

Mafunzo haya yanaondoa malalamiko mengi yaliyokuwepo kutoka kwa wananchi ambapo kwa kufanya hivi inawawezesha Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kufanya kazi kwa kufuata kanuni zilizopo,” amesisitiza.

Kwa upande mwingine; Mkuu huo wa Chuo amewasisitiza Maafisa hao kuhusu kuzingatia matumizi ya TEHAMA kwa kuwa Mahakama imetoa kipaumbele katika eneo hilo na hususani kipindi hiki inapoendelea na mchakato wa kuelekea kuwa Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.

Lengo kuu la mafunzo haya ni kuboresha utoaji huduma kwa jamii kwa weledi na kuhakikisha kuwa Mahakama inakuwa na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wenye weledi, mbinu bora na nyenzo za kufanyia kazi. Aidha, ili kupata nafasi ya kusoma mafunzo haya mwombaji ni lazima pamoja na sifa nyingine awe angalau na cheti halali cha kumaliza elimu ya kidato cha nne.

Kwa mujibu wa Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama, za mwaka 2017, mwombaji wa kazi za Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama anapaswa kuwa na cheti cha Umahiri cha mafunzo ya Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama kinachotolewa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Kwa mujibu wa Jaji Dkt. Kihwelo, tangu mafunzo haya yameanza kutolewa Julai 2018 utendaji kazi wa Madalali wa Mahakama pamoja na Wasambaza Nyaraka za Mahakama umeboreka na malalamiko yamepungua.

Aidha mpaka kufikia sasa Chuo kimeweza kutoa mafunzo kwa makundi nane tofauti na hili likiwa ni kundi la tisa na hivyo Chuo kimeweza kuwajengea uwezo Madalali wa Mahakama 240 na Wasambaza Nyaraka za Mahakama 131.

Mara baada ya kukamilika kwa utoaji wa mafunzo, Washiriki watafanya mitihani ya kupima umahiri wao na wakifaulu wanapatiwa cheti cha umahiri ambacho ni moja ya kigezo cha kuomba kazi ya udalali pamoja na usambaza nyaraka za Mahakama.

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambaza Nyaraka za Mahakama (waliosimama). Mhe. Dkt. Kihwelo amefungua Mafunzo hayo leo tarehe 15 Julai, 2022 katika Ukumbi wa Shule ya Sheria (Law School of Tanzania) jijini Dar es Salaam. Aliyeketi kulia ni Mhe. Victoria Nongwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na aliyeketi kushoto ni Mhe. Eliah Baha, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo kutoka IJA.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (aliyesimama) akizungumza na Washiriki wa Mafunzo (hawapo katika picha) alipokuwa akifungua Mafunzo hayo.  Aliyeketi kulia ni Mhe. Victoria Nongwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na aliyeketi kushoto ni Mhe. Eliah Baha, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo kutoka IJA.
Washiriki wa Mafunzo wenye nia ya kufanya kazi ya Udalali na Usambaza Nyaraka mza Mahakama wakimsikiliza Mgeni rasmi Mhe. Dkt. Kihwelo alipokuwa akitoa hotuba yake wakati akifungua mafunzo hayo.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya mafunzo hayo (Sekretarieti). Aliyeketi kulia ni Mhe. Victoria Nongwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na aliyeketi kushoto ni Mhe. Eliah Baha, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo kutoka IJA.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni