Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto
Naibu Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Prof. Fatihiya Massawe leo tarehe 13 Agosti,
2022 amehitimisha mafunzo ya siku tano yaliyowaleta pamoja Makatibu Mahsusi 56
kutoka Mahakama mbalimbali nchini kwa kuwahimiza watumishi hao wa Mahakama kufanyakazi
kwa bidii na kuzingatia mema na yanayokubalika katika jamii kwa vile Taifa
linawahitaji na kuwategemea.
Ametoa rai kwa Makatibu
Mahsusi hao kuwa kuzingatia mafunzo na maelekezo yote waliyoyapata na kisha kuyatafsiri
kwa kufanya kazi kwa weledi na kwa kiwango cha hali ya juu kwenye vituo vyenu
vya kazi. “Ninawahimiza mkafanye kazi kwa bidi kubwa na kwa kuzingatia yaliyo mema na yanayokubalika katika jamii. Napenda
mfahamu kuwa Taifa linawahitaji na kuwategemea sana,” amesema.
Naibu Mkuu wa Chuo huyo
amewaambia watumishi hao wa Mahakama ya Tanzania kuwa wanapaswa kutambua kuwa
kwa kupitia majukumu yao wanashiriki kutoa huduma kwa wateja moja kwa moja na
kupitia huduma hizo hujenga imani za wananchi katika Mahakama kwa ujumla.
“Ninaamini mafunzo haya
yamewajenga vizuri sana, ni imani yangu kuwa mtazingatia mafunzo haya katika
kuboresha utoaji wa huduma kwa mteja kwa kufanya kazi kwa bidi, ufanisi,
maarifa na kumjali mteja kila mnapotoa huduma kwake, kwa kuwa mteja ndiye mlipa
kodi na ndiye mwajiri,” amesema.
Amewakumbusha pia kutambua
kuwa mafunzo waliyoyapata endapo watayazingatia kwa ufasaha yatawatambulisha
vema kwa wananchi kwa kuwa wamepewa dozi nzuri ya utendaji wa kazi mzuri, hivyo
wataweza kushiriki na kuchangia katika kutekeleza malengo yaliyopo kwenye mpango
mkakati na vipaumbele vya Mahakama.
Prof. Massawe anaamini
mambo ambayo wananchi wanayoyalalamikia kama vile ucheleweshaji wa huduma,
uwepo wa rushwa, huduma kuwa duni, kauli zisizoridhisha, majivuno, matumizi
mabaya ya vyeo au jina la Mahakama wataenda kuyaondoa na kusaidia kurejesha imani
na mtazamo chanya kwa jamii.
“Nimatumaini yangu kuwa
mtakwenda kufanya kazi kwa nguvu moja na ari kubwa kwa lengo la kuleta
mabadiliko chanya vituoni. Mwende mkatimize wajibu wenu kwa weledi, ustadi,
uaminifu, maadili na nidhamu ya hali ya juu. Ni matarajio yetu kuwa mtaijenga na kuilinda
taswira nzuri ya Mahakama pamoja na viongozi wake. Uongozi wa Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto unawatakia utekelezaji mzuri wa majukumu yenu,” amewaasa Makatibu
Mahsusi hao.
Akitoa neno la shukurani
kwa niaba ya washiriki, Mwenyekiti wa Makatibu Mahsusi hao, Bi Dianess
Mwakatundu alieleza kuwa kwa moyo wa dhati wanaupongeza uongozi wa Mahakama ya
Tanzania kwa kuwapa fursa hiyo adhimu ya mafunzo na wameahidi kutekeleza yale
yote waliyojifunza na kuleta mabadiliko makubwa na yenye tija katika vituo vyao
vya kazi.
Kabla ya mafunzo hayo
kuhitimishwa, Makatibu Mahsusi hao
walipitishwa kwenye mada kadhaa, ikiwemo 'Kuthibiti Msongo wa Mawazo na Jinsi
ya kuwa na Hasira kama Mtumishi wa Umma' iliyowasilishwa na Mshauri Mwelekezi,
Bw. Geofrey Wawa na kuhusu 'Ujuzi wa Kifedha na Maisha ya Ujasiliamali'
iliyowasilishwa na Mkurugenzi na Mshauri Mwelekezi, Bw. James Rhombo.
Jana tarehe 12 Agosti,
2022, washiriki hao wa mafunzo walipitishwa kwenye mada mbalimbali na
wawezeshaji mahiri, ikiwemo ‘Huduma kwa Mteja’ iliyowasilishwa na Mhadhiri
kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Yustin Bangi na baadaye mada
kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi Patricia
Ngungulu kuhusu ‘Stahiki na Wajibu wa Mwajiri na Mtumishi katika Utumishi wa
Umma.’
Akiwasilisha mada yake,
Dkt. Bangi amewaeleza Makatibu Mahsusi hao kuwa tendo la huduma kwa mteja ni
endelevu, hivyo huduma wanayotoa inatakiwa iwe rafiki. “Kuna watu wengi
wanaogopa kuja mahakamani. Ikitokea nimekuja halafu unanifokea unanipotezea
mwelekeo. Ona huruma kwa mwenzio na uvae viatu vya huyo unayemhudumia. Usiwe na
upendeleo na kumbuka siyo kila mtu anaweza kuwa Katibu Mahsusi, nyinyi ni watu
muhimu sana, nawaomba mzingatie weledi mnapowahudumia wateja wenu,” amesema.
Amewasisitiza kuwa na
maarifa ya kutatua matatizo ya wateja wanaofika kupata huduma na kila mteja
anayefika mbele yao anatakiwa kutambuliwa, kusikilizwa, kuheshimiwa, kujaliwa
na kuhudumiwa.
“Kuna mambo muhimu sana
ya kujiuliza hapa. Usafi wako binafsi ukoje; sura zenu ninaonekanaje
mnapokutana na wateja. Sura zenu ziwe za
kumkaribisha mteja na akija mteja mbele yako anatakiwa apate kile
anachotarajia,” Dkt. Bangi aliwaambia watumishi hao wa Mahakama.
Kwa upande wake Bi
Ngungulu amewaeleza washiriki hao wa mafunzo kuwa kila mwajiri au mtumishi
anazo stahiki au haki kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali
inayosimamia utumishi wa mahakama au umma na kila upande unapaswa kuhakikisha
kwamba unazingatia utoaji wa haki au stahiki kwa upande mwingine.
Alizitaja baadhi ya
stahiki au haki za mtumishi wa umma kama kupewa nyaraka muhimu zinazohusiana na
utumishi wake, kulipwa mshahara au ujira kama ujira wa kazi aliyofanya na kupata
likizo na nauli ya likizo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Zingine ni kupata mafao
ya hitimisho ya kazi au ajira, kupewa mafunzo ya kujengewa uwezo na kuendelezwa
kitaaluma, kupata usalama wa afya na maisha yake katika sehemu za kazi, kupata
usalama wa afya na maisha yake katika sehemu za kazi na kulipwa fidia kwa
kuumia kazini.
“Hata hivyo ili mtumishi
au mwajiri aweze kupewa stahiki au haki anazopaswa kupewa ni lazima atimize
wajibu wake kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wake wa ajira. Wajibu ni
lazima utekelezwe kwanza ndio stahiki/haki zitatekelezeka,” alisema.
Ametaja sehemu ya wajibu
wa mtumishi kama kutekeleza majukumu yake ya kikazi kila siku kulingana na
taaluma, fani na kazi aliyoajiriwa nayo; kutimiza malengo ya mwajiri kwa mujibu
wa makubaliano na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo
mahali pa kazi na kama inavyotolewa na mamlaka mbalimbali za Serikali, kuwa na
utii na nidhamu.
Wajibu mwingine ni kufanya
kazi kwa kushirikiana na kuaminiana, kujenga na kuimarisha mahusiano mema
mahali pa kazi; kuheshimu mipaka ya kazi na miiko; kutoa huduma bora, kufanya
kazi kwa bidii, umakini na kwa ufanisi; kutoa huduma bila upendeleo na kuwa
mwadilifu katika kazi.
Akataja pia baadhi ya
majukumu ya mwajiri ikiwemo kuchukua hatua za kinidhamu kwa makosa ya mtumishi
akiwa kazini, kumpa mtumishi majukumu ya kufanya na mpango kazi na kuandaa au
kutengeneza na kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo
mbalimbali ya utumishi.
Majukumu mengine ni kumlipa
mtumishi ujira wake kwa kadri ya makubaliano baada ya kutimiza wajibu wake na
kwa muda uliokubaliwa; kumjengea mtumishi mazingira wezeshi ili aweze
kutekeleza majukumu yake kwa utulivu na ufanisi; kusimamia na kufuatilia
utendaji kazi wa mtumishi siku hadi siku na kumuendeleza mtumishi kwenye kada
(career) yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni