Ijumaa, 12 Agosti 2022

JAJI SHABAN LILA AWA MWENYEKITI WA JMAT TAWI LA MAHAKAMA YA RUFANI

 

Magreth Kinabo – Mahakama

Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Mahakama ya Rufani, Mhe. Shaban Lila amewataka wanachama wa tawi hilo kuendelea kuwa na ushirikiano na viongozi wapya waliochaguliwa ili kuwezesha chama hicho kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza mara baada ya kuibuka mshindi kuwa Mwenyekiti wa JMAT wa tawi hilo katika uchaguzi uliofanyika leo tarehe 12 Agosti, mwaka 2022 kwenye ukumbi  namba moja wa Mahakama ya Rufani Tanzania,uliopo Jijini  Dar es Salaam kwa ajili ya kujaza nafasi tano zilizo kuwa wazi  Jaji  Lila aliwashukuru wanachama JMAT   kwa kumpa kura.

‘‘Ninaombeni ushirikiano ili kuweza kutekeleza majukumu yetu ipasavyo na kulifanya tawi hili kuendelea kuwa hai,” amesema Jaji Lila, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Viongozi wengine walioibuka kuwa washindi katika nafasi nyingine zilizokuwa wazi ni Makamu Mwenyekiti chama hicho ni Mhe. Charles Magesa ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama hiyo.  Nafasi ya Katibu ilijazwa na Mhe. Kifungo Mrisho, nyingine ni Mweka Hazina ambapo ilijazwa na Mhe. Lukengelo Deda na Mwanachama Mwakilishi Mhe. Jonas Lyakundi aliibuka mshindi wa kiti hicho.

Awali Jaji Lila akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya tawi hilo, amesema limeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 18 (a) (i) ya Katiba ya JMAT ya 2017. Ambapo mwaka 2018 tawi hilo lilikuwa na wanachama 59, idadi hiyo ya wanachama   iliundwa na Majaji wa Mahakama hiyo, Msajili Mkuu pamoja na Katibu wake, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji, Mahakimu na Wasajili waliokuwa  katika Kurugenzi ya Maadili(DJSIE) Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri(DCM) na Kitengo cha Uboreshaji wa Mahakama(JDU).

Ameongeza kuwa hadi kufikia  tarehe 1 Agosti, mwaka 2022 tawi hilo lilikuwa na wanachama 91, lakini kutokana na uteuzi na uhamisho wa wanachama wengine  idadi ya wanachama hadi kufikia tarehe 12 Agosti mwaka 2022 limekuwa na wanachama 86. Hivyo ongezeko la  wanachama kutoka 59 mpaka 91 limechangiwa na kuongezeka kwa Majaji, Wasaidizi wa  Sheria wa Majaji, Wasajili wa Mahakama ya Rufaa na kuongezeka kwa baadhi ya vitengo.

Amevitaja vitengo hivyo kuwa ni Kituo cha Huduma kwa Mteja, Maktaba na Baraza la Rufaa za Kodi. Hivyo idadi ya wanachama imeongezeka kwa asilimia 35 kwa kipindi cha miaka mine kuanzia mwaka 2018.

Jaji Lila ameongeza kwamba tawi hilo la JMAT limekuwa likishiriki katika hafla mbalimbali, ikiwemo vikao, warsha, makongamano na mikutano. Mathalan ,baadhi ya vikao ambavyo tawi hilo limeshiriki ni kikao cha Baraza Tendaji la JMAT cha tarehe 22Septemba , mwaka 2018 kilichofanyika kwa njia ya whatApp.

Tawi hilo pia limeshiriki katika Mkutano Mkuu wa Majaji na Mahakimu wa Afrika Mashariki( EAMJA) uliofanyika Mombasa nchini Kenya mwaka 2018.Mwaka 2021 lilitoa wanachama 10 kuhudhuria mkutano mkuu wa JMAT uliofanyika Jjini Dodoma na  Julai mwaka  2022 lilitoa mwakilishi kuhudhuria kikao cha Baraza Tendaji la JMAT kilichofanyika Jijini Dodoma.


Baadhi ya wanachama wa JMAT wa tawi hilo walifuatilia kikao hicho.

Mwenyekiti wa JMAT tawi la Mahakama hiyo aliyemaliza muda wake, akitoa taarifa ya maendeleo ya tawi hilo.


Baadhi ya wanachama wa JMAT wa tawi hilo walifuatilia taarifa hiyo.

Mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jaji Augustine Mwarija (katikati) akifungua kikao hicho leo tarehe 12 Agosti mwaka 2022. (Kushoto) ni Mwenyekiti wa JMAT wa tawi hilo aliyemaliza muda wake, Mhe. Jaji wa Mahakama hiyo, Shaban Lila na kulia ni Makamu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Rehema Mkuye.

Makamu Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Jaji wa Mahakama hiyo Mhe. Rehema Mkuye akitoa neon la shukurani.


Mwenyekiti wa JMAT wa tawi hilo, Mhe. Jaji wa Mahakama hiyo Mhe, Jaji Shaban Lila akizungumza jambo mara baada kuchaguliwa.

Baadhi ya wanachama wa  JMAT wa tawi hilo wakichambua kura.

Picha ya pamoja ya viongozi waliochaguliwa katikati ni Mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) tawi la Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jaji Augustine Mwarija, wa (tatu kushoto)ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Mahakama ya Rufani, Mhe. Shaban Lila na wa pili kushoto ni wakala wa uchaguzi huo na wa kwanza kushoto ni Katibu wa JMAT tawi hilo, Mhe. Kifungo Mrisho. (Wa tatu kulia  wa Makamu Mwenyekiti chama hicho ni Mhe. Charles Magesa, wapili kulia Mwanachama Mwakilishi Mhe. Jonas  Lyakundi na wa kwanza kulia ni Mweka Hazina wa JMAT tawi hilo Mhe. Lukengelo Deda.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni