Na Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya mpira wa miguu ya Mahakama Sports, Kanda ya
Dar es Salaam jana tarehe 11 Agosti, 2022 imefanikiwa kuibuka mshindi kwa bao 1-0
dhidi ya timu ya TBS katika mechi nzuri ya kirafiki iliyochezwa
kwenye Viwanja vya Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law school) iliyoko Mikocheni
jijini Dar es Salaam.
Goli pekee hilo na la
ushindi lilifungwa na mshabuliaji hatari wa Mahakama Sports Ghulam Katwila baada
ya kupenyezewa pasi muruha kutoka kwa Winga machachari Charles Mwakapimba,
maarufu kwa jina la Mwaisa mtu MMBAD katika dakika ya 16 ya mchezo kipindi cha
kwanza.
Mchezo huo ulianza majira
ya saa kumi na nusu jioni kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na kulikuwepo na
kosa kosa za hapa na pale. Hata hivyo, Mahakama Sports waliweza kuitumia vizuri
nafasi waliyoipata katika dakika hiyo ya 16 ya mchezo na kufanikiwa kupachika
bao hilo.
Kupatikana kwa bao hilo
kuliamsha ari ya wachezaji wa pande zote mbili, huku vijana wa Mahakama Sports
wakitandaza kandanda safi. Isingekuwa umakini wa kolikipa wa Timu ya TBS,
Mahakama Sports ingeweza kujipatia magori mengi zaidi katika kipindi hicho.
Baada ya kosa kosa
nyingi, wachezaji wa Timu ya TBS wakacharuka kama nyuki na kuanza kulishambulia
lango la Mahakama Sports na kufanikiwa
kupata penati katika dakika ya 44 ya mchezo, baada ya beki wa Mahakama Sports Club
Joseph Nchimb, kwa jina maarufu Mjomba kuunawa mpira akiwa katika harakati za
kuuokoa ndani ya 18.
Hata hivyo, TBS
wakashindwa kuukwamisha mpira kwenye nyavu baada ya penati hiyo kuokolewa na
golikipa mahili wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe. Hadi timu zote zinaenda mapunziko, Mahakama
Sports ikatoka kifua mbele kwa ushindi huo wa bao moja.
Kipindi cha pili kilianza
kwa kasi kwa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu. Wachezaji wa timu zote
walishindwa kutumia vizuri nafasi walizokuwa wanazitengeneza na hadi dakika 90
zinaisha Mahakama Sports Club 1 na TBS 0.
Kikosi cha Mahakama Sports
kiliundwa na Spear Mbwembwe, Nasoro Mwampamba, Gisbert Chentro, Omari Mdakama,
Robert Tende Mwantimwa, Chilemba Hassan, Ghulam Katwila, Fidelis Choka, Charles
Mwakapimba na Joseph Nchimbi.
Katika hatua nyingine, Timu
ya Mahakama Sports ya Mpira wa Netiboli kutoka Kanda hiyo ilitoana jasho na TBS
na kupoteza kwa taaaabu kwa vikapu 17- kwa 28. Kikosi cha Mahakama Sports kiliundwa
Bahati Sultan, Agness Mwanyika, Tausi Mwambujhule, Rhoida Makasi, Edith Kanju,
Nyangi Kisagenta, Sophia Songolo, Flaviana Jackson, Jamila Kisusu, Jackline
Paul na Janevailler.
Michezo hiyo ya kirafiki
ni sehemu na mwendelezo wa maandalizi ya michezo ya SHIMIWI inayotarajiwa
kufanyika mkoani Tanga kuanzia tarehe 01 hadi tarehe 15 Octoba, 2022.
Akizungumza baada ya michezo
hiyo, Kocha mchezaji wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe amewapongeza
vijana wake kwa mchezo mzuri waliouonyesha katika vipindi vyote na ameridhishwa
na matokeo hayo. Hata hivyo amewahimiza kuendelea kufanya mazoezi kwa nguvu ili
kuweza kujiandaa vizuri na mashindano yajayo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Mahakama Sports Wilson Dede ameshukuru kwa timu za Mahakama kwa kupambana na
kwa kupata mechi hizo za kirafiki, ambazo ni kipimo sahihi kwao kuelekea
mashindano ya SHIMIWI.
“Tunawaomba wanamichezo wote na watumishi
wengine wa Mahakama Mikoa yote huko waliko kuendelea kufanya mazoezi ya pamoja.
Safari hii tupo makini sana kwa vile nia yetu ni kutengeneza timu imara zitakazoleta
ushindi kwa Mahakama kwenye michezo yote tunayoenda kushiriki,” amesema.
Golikipa wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe akidaka penati kutoka kwa mchezaji wa TBS kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa jana tarehe 11 Agosti, 2022 kwenye viwanja wa Law School. Mahakama Sports ilichomoza kwa bao 1-0.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni