Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto
Mwanadiplomasia nguli nchini,
Balozi Charles Sanga amewasihi Makatibu Mahsusi na watumishi wengine wa
Mahakama ya Tanzania kuzingatia uzalendo na maadili mema wanapotekeleza
majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi ili kuonyesha dhamira ya kweli katika
kuitumikia Tanzania.
Akiwasilisha mada kwenye
mafunzo yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuhusu ‘Uzalendo,
Itifaki na Maadili’ ambayo yanajumuisha Makatibu Mahsusi 56 kutoka Mahakama
mbalimbali nchini, Mhe. Sanga amesema kuwa uzalendo ni njia pekee inayomwongoza
mtumishi katika njia zake sahihi.
“Nawasihi mjitoe nafsi
zenu kwa ajili ya nchi na watu wengine. Tumieni nafasi ambazo umepewa na Mungu
kwa faida ya watu wengine. Kuna mambo mengine huwa yanashangaza sana, utakuta
mtu anamwaga chakula! huu sio uzalendo hata kidogo. Kumwaga chakula siyo
uzalendo. Jifunze tabia ya kumaliza chakula,” Mhe. Sanga aliwaambia watumishi
hao wa Mahakama.
Amewaambia maana halisi
ya uzalendo ni kuwa na moyo uliotukuka upendo kwa nchi na wananchi wake,
kuheshimu
nembo za nchi kama Wimbo wa Taifa; Bendera ya Taifa; Ngao ya Taifa; Twiga, kuwa
na dhamira hai na kuipenda nchi yako kwa moyo wako wote, akili zako zote, kwa
nguvu zako zote na upendo kwa nchi kama unavyojipenda mwenyewe.
“Uzalendo unadai daima
kuwa mkweli hata kama utajenga maadui, woga ni adui wa maisha. Usifanye kazi
kwa woga wala usiwe mwoga kutetea ukweli. Ujasiri utakufanya uweze kufikia
malengo yako katika maisha. Fanyeni kazi kwa bidii, kila siku ni siku mpya;
usizoee kazi wala usimzoee mtu. Fedha ni matokeo ya kazi na siyo msingi wa
kufanya kazi,” amesema.
Balozi Sanga amewakumbusha
washiriki wa mafunzo hayo kuwa jamii isiyo na maadili mema na uadilifu ni jamii
iliyooza, hivyo akawashauri kujiepusha na ubinafsi, ulafi, uchoyo, chuki, ufisadi,
kiburi na majivuno pamoja na hasira na vitendo vyovyote vya rushwa kama rushwa
ya fedha, rushwa ya ngono na rushwa ya upendeleo kwa kutumia familia, ukabila,
ukanda na undugu.
“Mna wajibu wa kuwa
waaminifu kwa nchi; kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kuheshimu sheria, kanuni
na taratibu bila unafiki. Uaminifu wa kweli unakudai kusema ndiyo au hapana
kulingana na uhalisia wa mazingira bila woga au unafiki. Fanyakazi bila kuchoka
au kukataa tamaa ili kutekeleza malengo kwa wakati uliopangwa. Uwe na
unyenyekevu na upole kuyapokea mapungufu yanayotokea sehemu yako ya kazi bila
kutoa visingizio na kujitetea ili uweze kujisahihisha,” amesema.
Awali, Makatibu Mahsusi
hao walikutana na Afisa Utumishi Mwandamizi kutoka Utumishi, Bi. Getrude
Chiunga, ambaye aliwapitisha kwenye mada kuhusu ‘Maadili na Kanuni za Maadili
kwa Utumishi wa Umma’ na kusisitiza kuwa maadili ni msingi wa kila kitu katika
utumishi wa umma.
“Mnatakiwa kufanya kazi
kwa uadilifu na kuepuka matumizi mabaya ya madaraka. Wewe una wajibika pale
ulipo, siyo kiongozi wako. Makatibu Mahsusi tunasemwa sana huko nje kwa vitu
vidogo vidogo kama mavazi na tabia mbaya. Mavazi na utanashati katika kutoa
huduma unatusaidia kutuaminisha. Hivyo, nawasihi tubadilishe mienendo yetu nje
na ndani ya mahala pa kazi,” amesema.
Bi Chiunga akawasihi
kuzingatia kanuni za maadili ya utendaji wanapotekeleza majukumu yao kazini,
ikiwemo kutoa huduma bora, utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila
upendeleo, kufanya kazi kwa uadilifu, kuwajibika kwa umma, kuheshimu sheria na matumizi
sahihi ya taarifa.
“Katika matumizi sahihi
ya taarifa, watumishi wa Umma wanapaswa kuzingatia Sheria ya Nyaraka Na.3 ya
Mwaka 2002, kuzingatia Mwongozo wa
Matumizi Sahihi na Salama ya
TEHAMA Serikalini wa mwaka 2017, ikiwemo kuepuka matumizi ya anuani za barua
pepe katika mawasiliano ya Serikali na kuepuka matumizi ya mtandao kutuma
nyaraka zote za siri,” amesema.
Akawahimiza pia kujali
muda wa kazi na kufika kazini mapema na kwa wakati, kuondoka baada ya
kukamilisha kazi na siyo tu baada ya muda wa kazi kuisha, kutulia ofisini na
kufanya kazi, kuwa tayari kufanya kazi kwenye kituo chochote cha kazi unachopangiwa,
kufanya kazi kwa ufanisi na kukamilisha majukumu na kutumia utaalamu, ujuzi na
maarifa kuongeza tija kazini.
Hata hivyo, Bi Chiunga
amekemea uvujaji wa siri za Serikali kupitia vyombo vya habari na njia
nyingine, ukiritimba katika upatikanaji wa taarifa kwa vyombo vya habari,
wananchi na watumishi ambazo wanapaswa kuzijua na kuficha kwa makusudi taarifa
ambazo umma au watumishi wenzao wana haki ya kuzijua.
Sehemu nyingine ya Makatibu Mahsusi 56 (picha mbili chini) wanaohudhuria mafunzo IJA wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wawezeshaji.
Sehemu nyingine ya Makatibu Mahsusi 56 (picha mbili chini) wanaohudhuria mafunzo IJA wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wawezeshaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni