·Awafunda kujikubali, kuwa waaminifu
Na
Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto
Mafunzo ya siku tano ambayo yamewaleta pamoja Makatibu
Mahsusi 56 kutoka Mahakama mbalimbali nchini yameingia siku ya tatu leo tarehe
11 Agosti, 2022 ambapo Mwanasaikolojia, Bi. Sadaka Gandi amewaasa kujikubali,
kujitambua na kujiona kuwa wao ndiyo sura ya Mahakama, hivyo wanapaswa
kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini na kuzigatia uaminifu wa hali ya juu.
Akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo yanayofanyika
katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuhusu ‘Uthabiti, uaminifu
na uvumilivu mahali pa kazi,’ Bi Gandi amewashauri
watumishi hao kujibeba wao wenyewe, kujikubali kwa namna gani ni muhimu katika
ofisi na kuacha kufanya uamuzi kwa hisia bila kupima matokeo yake kwa wale
wanaowahudumia katika mnyororo mzima wa utoaji haki mahakamani.
“Nyinyi ni sura ya Mahakama. Nawashauri msijichukulie rahisi rahisi, ni watu muhimu sana mahala pa kazi. Ikiwa mawasiliano yako ni
duni utakuwa una uwezo mdogo wa hisia. Wewe ndiye unayepeleka hisia ya ofisi
kwa watu. Hivyo, kama huna nguvu ya kujibeba utajiona umezaliwa na bahati
mbaya. Chukua
hatua na uhakikishe kuwa uko juu,” Mwanasaikolojia Ushauri Nasaha na Mtindo wa
Maisha amesema.
Amewaambia washiriki hao wa mafunzo kuwa changamoto
wanazokabiliana nazo wanapotekeleza majukumu yao ni za kawaida, hivyo wanapazwa
kisimama wao kama wao na kubeba thamani waliyonayo, kwani kwa kufanya hivyo
wanaweza kufanya kazi zao bila kuteteleka. Akawashauri pia kuzingatia uaminifu na
mara zote kumfikiria mwajiri wao kwanza badala ya nafsi zao.
“Kuna watu wengine wanapenda kuumiza wenzao ili wapate
nafuu. Ukikutana na watu wa aina hiyo ofisini kaa nao mbali. Ni muhimu
kuvumilia, lakini ni vizuri zaidi kujua kitu gani cha kuvumilia,” alisema.
Akawakumbusha watumishi hao kuwa hakuna mtu aliyeumbwa na Mungu na akili ya
kihisia, bali yote yanayotokea yanatokana na kujifunza kutoka kwa watu wengine.
Bi Gandi akasema, “Hakuna aliyezaliwa mmbea duniani,
tunajifunza. Thibiti hisia zako, utakuwa kwenye matatizo kama hutaweza. Ukiamua
kitu fulani kiwe kizuri, kitakuwa tu. Unavyoitazama dunia ndivyo
unavyochangamana nayo. Kama moyoni mwako kuna giza, ndivyo dunia utakavyoiona.
Jambo la msingi zingatia mipaka yako na mara zote jiulize kama unaridhika kuwa
kazini kwako.”
Amesema mfumo wa Mahakama unahitaji watu wenye mtazamo
wa watu wazima na waliokomaa kwa vile mtazamo wa mtu mmoja unaweza kuathiri
kila mtu katika taasisi na mfumo uliopo unaweza kuathiri utamaduni wa shirika na pia mitazamo ya wafanyakazi.
“Kuimarisha mitazamo chanya ya mahali pa kazi kutaleta
manufaa kwa mwajiri na mfanyakazi na jambo la msingi itaongeza tija, ustawi wa
wafanyakazi kwenye kilele chake na msisimko mzuri kwa ujumla ambao watu
hufurahia kuwa mahali pa kazi,” Bi Gandi amesema.
Jana jioni tarehe 10 Agosti, 2022, Makatibu Mahsusi
hao walipitishwa na Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Mahakama, Bw. Allan Machella
kwenye mada kuhusu matumizi ya teknolojia ya kisasa mahakamani, hatua ambayo ina
jukumu muhimu katika kuhakikisha dhamira, dira na mipango ya kimkakati inatekelezwa
vyema kupitia uboreshaji wa kisasa wa shughuli za kimahakama.
Aliwaambia washiriki kuwa teknolojia ya habari
hutengeneza fursa na changamoto kwa pamoja ambazo zinahitaji kueleweka
kikamilifu ikiwa Mahakama ya Tanzania italazimika kufaidika na kile ambacho
teknolojia ya habari inatoa.
Katika mafunzo yanayoendelea, mada zingine zilizowasilishwa leo zinahusu ‘Maadili
na Kanuni za Maadili kwa Utumishi wa Umma’ iliyowasilishwa na Afisa Utumishi
Mwandamizi kutoka Utumishi, Bi. Getrude Chiunga na ‘Uzalendo, Itifaki na
Maadili’ iliyowasilishwa na Balozi Charles Sanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni