Jumatano, 10 Agosti 2022

WITO MUHIMU KWA MAKATIBU MAHSUSI

Na Faustine Kapama – Mahakama, Lushoto

Mafunzo ya siku tano yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kuwaleta pamoja Makatibu Mahsusi 56 kutoka Mahakama mbalimbali nchini yameingia siku ya pili leo tarehe 10 Agosti, 2022 huku washiriki hao wakitakiwa kuwa na ‘vifua’ ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu katika mnyororo mzima wa utoaji haki kwa wananchi.

Akiwasilisha mada kuhusu ‘Ijue Mahakama Yako’ na “Tamaduni za Mahakama,’ Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Japhet Manyama amewaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa wao ni nguzo muhimu ya ofisi ya Mahakama kwa vile hakuna wasichokijua kinachofanywa na viongozi wao katika maeneo yao ya kazi.

“Nyinyi ndiyo mhimili wa Mahakama, watumishi wengine kama afisa utumishi, karani, mtendaji au mlinzi hawakai na viongozi wao katika ofisi moja. Mnatakiwa kutunza siri za viongozi wen una kutunza siri za ofisi. Najua kila mtu ana mapungufu yake, msiwe wepesi wa kuanika kila kitu kinachofanyika kwa mabosi wenu na ofisi mnazozihudumia kwa ujumla,” amesema.

Mwezeshaji huyo amesema kazi kubwa ya Mahakama ni kutoa haki kwa wananchi kwa wakati, hivyo kila mmoja wao anapaswa kutekeleza majukumu yake pale alipopangiwa, ikiwemo katika ngazi ya Ukatibu Mahsusi. “Nyinyi ni watu wakubwa sana mahakamani, ila hamjui tu. Ulishawahi kukuta ofisi ipi ina Makatibu Muhtasi wanne? Ulishawahi kujiuliza kwa nini upo peke yako?” alihoji.

Akawapitisha kwa ufupi kwenye dira na dhamira ya Mahakama ya Tanzania na kusisitiza kila mmoja kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili. Amewahimiza kujiepusha na vitendo vyote hasi, ikiwemo matumizi ya lugha mbaya kwa wananchi, jambo ambalo halikubaliki hata kidogo katika Mahakama ya sasa.

“Mahakama ya bora liende imeshapita, lazima tubadilike kwenda sambamba na mabadiliko na uboreshaji wa miundombinu unaoendelea kwa sasa,” amesema na kuwakumbusha pia kuwa kwa sasa Mahakama inachagiza matumizi teknolojia ya kisasa kwenye kila huduma ya kimahakama, hivyo wanapaswa kwenda na kasi hiyo ya mabadiliko.

Awali, akiwasilisha mada kuhusu ‘Utunzaji wa Majalada ya Watumishi na Mawasiliano ya Siri za Serikali’, Mkufunzi Msaidizi Masomo ya Uhazili kutoka Utumishi, Bi Juliana Mwalusamba amesema kuwa kila mtumishi katika sehemu ya kazi ana wajibu wa kutunza siri za Serikali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi, kwani kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kufanya kazi zake kwa utulivu na pia kulinda usalama wa Taifa.

“Katibu Mahsusi ni mmoja wa watumishi wanaoshiriki kazi nyingi zinazohusisha matumizi ya majalada ya watumishi. Ni wajibu wako kuhakikisha kuwa taarifa za watumishi zinashughulikiwa kwa usiri mkubwa hata kama hazijawekwa kwenye jalada la siri. Ni marufuku kabisa kwa mtumishi kushika au kuangalia kwa namna yoyote jalada lake binafsi au taarifa zilizo ndani ya jalada lake,” amesema.

Akawakumbusha washiriki hao wa mafunzo kuwa wakati wa kutekeleza majukumu katika osisi za umma kila mtumishi anapaswa kutunza siri za Serikali katika kutekeleza takwa la sharia na kanuni mbalimbali, kulinda amani na utulivu sehemu ya kazi au jamii, kuepuka mipango pingamizi, kulinda faragha za watu, kulinda usalama wa Taifa na kuepuka udhalilishaji.

“Watumishi wa umma na wananchi wote tunapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi katika kulinda siri za Serikali ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na kuvuja kwa taarifa hizo,” amesema.

Mada nyingine iliwasilishwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Bw. Sebastian Lacha ambayo ilihusu ‘uelewa wa mpango mkakati wa Mahakama kwa ajili ya utekelezaji mzuri wa shughuli za kila siku’ iliyowasilishwa.

Zingine ni ‘utawala, muundo na maendeleo ya mifumo; maendeleo ya ujuzi, ukaguzi na usimamizi wa utendaji; upatikanaji wa haki na uadilifu wa umma’ iliyowasilishwa na Naibu Msajili kutoka Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama, Mhe. Sekela Mwaiseje na ‘matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kimahakama’ iliyowasilishwa na Afisa TEHAMA Mwandamizi, Bw. Allan Machela.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Japhet Manyama akiwasilisha mada kwenye mafunzo ambayo yamewaleta pamoja Makatibu Mahsusi 56 yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto leo tarehe 10 Agosti, 2022.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Bw. Sebastian Lacha akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutoka Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama, Mhe. Sekela Mwaiseje akiwasilisja mada kwenye mafunzo hayo.

Afisa TEHAMA Mwandamizi, Bw. Allan Machela akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo ambayo yamewaleta pamoja Makatibu Mahsusi 56 kutoka Mahakama mbalimbali nchini.


Sehemu ya Makatibu Mahsusi 56 (picha mbili za juu na mbili za chini) wanaoshiriki kwenye mafunzo yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. 


Sehemu nyingine ya Makatibu Mahsusi 56 (picha tatu za chini) wanaoshiriki kwenye mafunzo yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.




Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro Mhe. Japhet Manyama (kulia) akiwa katika ukumbi wa mafunzo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni