·Jaji Mkuu ahimiza Watanzania kushiriki sensa
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza
viongozi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kuchukua jitihada mahususi ili
kuifanya Mahakama hiyo kuwa ya mfano katika mabadiliko, hususani katika
matumizi ya teknolojia kwenye utoaji wa huduma za haki kwa wananchi.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 5 Agosti,
2022 alipokuwa akifunga Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani uliofanyika
katika Hoteli ya Nashera mjini hapa.
“Msajili na Mtendaji wa Mahakama mnao wajibu wa
kugeuza Mahakama ya Rufani kutoka kwenye matumizi makubwa ya karatasi na kuwa Mahakama
inayotumia vifaa vya kisasa kusikiliza mashauri yanayowasilishwa katika
Mahakama ya Tanzania,” amesema.
Jaji Mkuu aliwakumbusha viongozi hao pamoja na wajumbe
wa Mkutano kuwa katika mada yake aliyowasilisha, Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw.
Kalege Enock aliwaomba kuwa kama viongozi wanayo nafasi ya kuonyesha mifano kwa
wengine na vile vile kuwa sehemu ya kuangalia upya taratibu za kimahakama na
kuziweka kwenye mifumo ya kimtandao.
“Lazima mtafute majibu kwa nini usajili wa mashauri
umefika asilimia 98 kwa njia ya mtandao, lakini mara baada ya kupokelewa kwa
njia hiyo tunarudi tena kwenye makaratasi. Hilo ndiyo suala la ajabu kidogo. Haya
ni maeneo ambayo Mahakama ya Rufani tunaweza kuwa mfano
kwa mabadiliko,” alisema.
Mhe. Prof. Juma, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano
huo akahoji, “Kwa nini hatuna electronic files (majalada ya kielektroniki), nadhani
mada zilizotolewa zinatuhimiza kwamba tuanze kuhama kutoka matumizi ya karatasi
twende katika matumizi ya Mahakama mtandao.”
Amesema pia kuwa kama alivyoeleza katika hotuba yake ya
ufunguzi, Majaji wa Mahakama ya Rufani ni viongozi ambapo kiongozi mzuri huwa hasubiri
kuambiwa, bali anao wajibu wa kuuliza na kufuatilia popote pale penye
changamoto ya aina yoyote kwa kuzingatia viongozi wa sasa wa Mahakama wapo wazi
na wanapokea changamoto zote na pamoja na ushauri.
“Ni matarajio yangu kwenu pamoja na wajumbe wote wa
Mkutano kwamba ninyi kama viongozi hamtasubiri kuambiwa na sekretarieti kuwa
wamefanya nini bali ni wajibu wetu pia kufuatilia yote tuliyokubaliana kama
yote yanatekelezwa na sisi wenyewe au wengine wanaotakiwa kutekeleza,” alisema.
Amewaomba wajumbe kuwashirikisha watumishi wengine wa
Mahakama ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria Mkutano huo ambao umekuwa na
manufaa makubwa na kuwasihi wanapokumbana na changamoto ya kiutendaji
wajitahidi kuiwasilisha katika mamlaka husika haraka ili ipatiwe ufumbuzi.
Jaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wajumbe kuhusu
zoezi la sensa ambalo litafanyika terehe 23 Agosti, 2022 nchini kote. “Zoezi
hili ni muhimu sana kwetu sisi Mahakama kwa sababu mipango yetu mingi ya ujenzi
wa miundombinu kupeleka huduma kwa wananchi itategemea matokeo ya hiyo sensa,
hivyo tuwahimize watumishi, ndugu zetu na marafiki washiriki hilo zoezi,”
amesema.
Kadhalika, Mhe. Prof. Juma alisisitiza kuwa kwa Mahakama
zoezi la sensa linawakumbusha umuhimu wa kukusanya takwimu muhimu kama shughuli
zao za kila siku ambazo zinatakiwa kuwasaidia kufanya uamuzi wa kisera na ule
wa uboreshaji.
Amesema awamu ya pili ya mradi wa Benki ya Dunia
imetambua umuhimu wa kukusanya takwimu na inaunga mkono kuanzishwa kwa Kituo
cha Matukio cha Mahakama ya Tanzania ambacho kitakuwa kinapokea data na takwimu
kuhusu masuala mbalimbali yanayotokea mahakamani.
“Moja ya eneo ambalo mradi wa uboreshaji umeagiza kitengo
cha uboreshaji kufanya ni kuwezesha uwepo wa gender justice strategic framework. Kituo hiki ni muhifadhi wa
taarifa hizo muhimu ambazo zinatakiwa kutusaidia na wao wamesisitiza kwamba
tuanze kukusanya taarifa za haki jinsia,” alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, Mahakama ya Tanzania
inatakiwa kukusanya takwimu kuhusu gender justice (haki jinsia), gender violence
(ukatili wa kijinsia) ambapo Andiko linatakiwa kutayarishwa kusaidia ukusanyaji
wa takwimu, eneo ambalo mradi wa Benki ya Dunia utapimwa.
Jaji Mkuu amesema kuwa takwimu za haki jinsia kutoka
katika mashauri yanayopitia mahakamani, wananchi wanaohudhuria mahakamani na malalamiko
yanayopokelewa mahakamani zinatakiwa vile vile kukusanywa kwa kuzingatia haki
jinsia.
“Kwa mfano, katika kila Mahakama tuna vituo vya
madawati ya jinsia ambavyo vinakusanya taarifa kila siku, lakini hatujui hizo
taarifa zinakwenda wapi, zinashughulikiwaje na zinasaidia nini katika kuboresha
sera na mambo ya kiutawala ya Mahakama. Kwa hiyo, tuna kazi kubwa ya kuhakikisha
tunatumia hizo takwimu kuboresha hali ya haki jinsia,” amesema.
Mkutano huo ambao uliwaleta pamoja Majaji wote wa Mahakama
ya Rufani, Msajili wa Mahakama hiyo, Mhe. Kevin Mhina, ambaye ndiye alikuwa Katibu,
Naibu Wasajili na watumishi wote kutoka katika Mahakama hiyo ulifunguliwa jana
tarehe 4 Agosti, 2022 na Jaji Mkuu ambapo wajumbe walipata nafasi ya kupokea
taarifa kuhusu hali ya mashauri na utendaji.
Kadhalika wajumbe wa Mkutano huo ambao uliwashirikisha
viongozi wengine wa Mahakama kama waalikwa walipitishwa kwenye mada mbalimbali
zilizotolewa na wawezeshaji wabobezi, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani
mstaafu, Mhe. Edward Rutakangwa.
Miongoni mwa viongozi wa Mahakama walioalikwa kwenye
Mkutano huo ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni