·Mahakama ya Tanzania haina mpinzani ufuatiliaji hukumu kwenye mtandao
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Mahakama ya Tanzania imeanzisha mifumo mbalimbali
inayosaidia kurahisisha huduma za utoaji wa haki, ikiwemo ule unaothibiti
upotevu wa majalada na nyaraka mahakamani, hatua inayoodoa kabisa malalamiko
kutoka kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha TEHAMA cha Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock alipokuwa
akiwasilisha mada kuhusu Hali ya Mifumo ya TEHAMA na Matumizi ya TEHAMA kuelekea
Mahakama Mtandao katika siku ya pili ya Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya
Rufani unaofanyika mjini hapa.
Amewaambia wajumbe wa Mkutano huo chini ya Mwenyekiti wake,
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa mfumo mpya wa
Mahakama umejengwa kwa kuzingatia viwango vya kiusalama vilivyowekwa kwa
mamlaka ya Serikali Mtandao nchini Tanzania na kwa kuzingatia viwango vya
kimataifa na miongozo mbalimbali katika ujenzi wa mifumo.
“Mfumo huu utakuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu za
namna ambazo watumiaji wake wameingia na kufanya nini. Hivyo taarifa zote
zitahifadhiwa zikionyesha kila mtumiaji aliyeingia kwenye mfumo amefanya kitu
gani,” amesema.
Akijibu moja ya hoja iliyoibuliwa na Majaji wa
Mahakama ya Rufani waliokuwa wanatoa hoja mbalimbali kwenye Mkutano huo, Bw.
Enock alifafanua kuwa watu wote ambao watakuwa wanaingia kwenye mfumo ni wale
ambao watakuwa wameruhusiwa kwa mujibu wa nafasi za vyeo vyao ama kazi zao
mahakamani.
“Watajaza fomu maalumu ambayo itahifadhiwa kwenye
majalada yao, lengo ni kuongeza uwajibikaji ili kila mtumiaji awajibike namna anavyotumia mfumo kwa ajili ya kuepusha
matumizi mabaya ya mtandao na pia upotevu wa nyaraka na mambo mengine
yanayofanana na hayo. Kwa hiyo kutakuwepo na uwajibikaji mkubwa sana,” amesema.
Bw. Enock amewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa Mahakama
ya Tanzania ni kati ya Taasisi chache za umma ambazo zimefungamanisha TEHAMA na
shughuli zake za utendaji (business operations).
Mkurugenzi huyo amesema kuwa Mpango Mkakati wa
Mahakama wa kwanza (2015/16 - 2019/20 uliweka dira na mikakati inayolenga
kuongeza ufanisi kwa kutumia TEHAMA na uliainisha vipaumbele vya TEHAMA; miundombinu
ya mawasiliano, kusimika vifaa vya kuendeshea mashauri na kuimarisha Masijala
“Mahakama ya Tanzania imekamilisha kufanya mapitio ya
mtiririko wa utendaji kazi (business process re-engineering) ya huduma za Mahakama
(Court Services) ambapo utendaji kazi uliopo sasa una jumla ya hatua 703 na baada
ya zoezi la mapitio zitabaki hatua 320 ambayo ni sawa na asimilia 46 ya
ongezeko la ufanisi,” amesema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Uboreshaji cha Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amewaambia wajumbe wa Mkutano huo alipokuwa
akiwasilisha taarifa ya uboreshaji, mpango mkakati na awamu ya pili ya mradi wa
Benki ya Dunia kuwa Mahakama ya Tanzania
haina mpinzani kwenye ufuatiliaji wa hukumu zilizopandishwa kwenye mtandao.
Mhe. Dkt. Rumisha amesema kwa sasa Mahakama ya
Tanzania inashindana na nchi ya Marekani ambapo asilimia 85 ya uamuzi
unaotolewa na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu unapandishwa kwenye mtandao,
hivyo kuvuka lengo lililopo.
“Asilimia 82.8 ya uamuzi uliopandishwa kwenye mtandao
kutoka Tanzania unafuatiliwa ikifuatiwa na Marekani yenye asilimia 2.7 tu.
Majirani zetu hawaelewi kabisa tunafanyaje, sio Kenya wala hata Afrika ya
Kusini,” amesema.
Mkuu huyo wa Kitengo cha Uboreshaji amebainisha pia kuwa
Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza mlundikano wa
mashauri mahakamani kutokana na kasi ya usikilizaji wa mashauri mbalimbali.
Ametolea mfano muda wa kusikiliza mashauri, kwa mwaka
2015 ilikuwa siku 515, lakini kwa mwaka 2021 umepungua hadi siku 119 tu. Amesema
Mahakama inayotembea ndiyo kabisa, imefanya miujiza ambapo mashauri
yanamalizika kwa siku 30 tu badala ya siku 120 kwa Mahakama za kawaida.
“Kwa sasa tupo kwenye tarakimu moja tofauti na nchi
zingine zinazotuzunguka. Mrundikano ulipungua hadi asilimia 8.4 ilipofika mwaka
2021. Uboreshaji wa data uliwezesha ufuatiliaji bora na afua za kimkakati na
tumevuka malengo kwenye mashauri ya kibiashara na trafiki,” amesema.
Mada zingine zilizowasilishwa katika siku hiyo ya pili
kabla ya Mwenyekiti kufunga Mkutano huo zilihusu maandalizi ya kustaafu utumishi
wa umma, maelezo na ufafanuzi kuhusu kanuni mpya za ukokotozi wa pensheni kwa
watumishi wanaostaafu na dondoo za afya na ugonjwa wa UVIKO-19.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Stella Mugasha akisisitiza jambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni