·Mahakama haishikiki uboreshaji miundombinu
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Kasi ya kumalizika kwa mashauri (clearance rate) katika
Mahakama ya Rufani ya Tanzania imepanda kutoka asilimia 73 kwa Disemba 2021
mpaka kufikia asilimia 92.9 mpaka Juni 2022.
Hayo yamebainishwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Kevin Mhina alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mashauri katika Mahakama
hiyo kwenye Mkutano wa Nusu Mwaka ambao umefunguliwa leo tarehe Agosti, 2022 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma.
“Kiwango cha kumaliza mashauri kwa kipindi cha mwezi
Januari-Juni 2022 kilikuwa ni asilimia 92.9. Hivyo Mahakama ya Rufani kwa
kipindi cha Januari-Juni 2022 ilikuwa na uwezo wa kumaliza asilimia 92.9 ya
mashauri yanayosajiliwa. Iwapo kama katika kipindi hicho uamuzi wote ungetolewa
kiwango cha kumaliza mashauri kingekuwa asilimai 97. Katika kipindi cha mwaka
jana ilipofika Disemba 2021 kiwango cha
kumaliza mashauri ilikuwa ni asilimia 73. Hivyo kasi ya kumaliza mashauri
imepanda kwa asilimia 19.9,” amesema.
Mhe. Mhina ameueleza Mkutano huo unaofanyika katika
Hoteli ya Nashera mjini hapa kuwa Mahakama ya Rufani ilianza mwaka mpya wa 2022
ikiwa na jumla ya mashauri 5,054 ambayo yalibaki mwaka 2021. Amesema kuwa Januari
- Juni 2022, Mahakama hiyo ilisajili jumla ya mashauri 908 na kati ya hayo 237
ni yenye asili ya jinai na 671 yenye asili ya madai.
Kwa mujibu wa Mhe. Mhina, ambaye ni Katibu wa Mkutano
huo, mashauri yaliyosikilizwa yalikuwa 881 yanayojumuisha 313 ambayo ni ya
jinai na mengine 568 ya madai. “Kipindi cha nusu mwaka
kwa mwaka uliopita (Janauri-Juni 2021) jumla ya mashauri 734 yalisikilizwa
hivyo kuna ongezeko la mashauri 147 yaliyosikilizwa,” amesema.
Akizungumzia hali ya utoaji haki katika Mahakama hiyo
ya juu hapa nchini, Mhe. Mhina amebainisha kuwa katika kipindi cha nusu ya
kwanza ya mwaka 2022 kwa mujibu wa kalenda ya Mahakama ya Rufani, Mahakama
ilipanga kufanya vikao 16 katika kanda 12 ambazo ni Dar es Salaam, Mbeya,
Arusha, Mwanza, Iringa, Tabora, Mtwara, Dodoma, Tanga, Musoma, Kigoma na Zanzibar.
“Vikao vyote vilifanyika kwa asilimia 100 kama
vilivyokuwa vimepangwa. Katika kipindi husika Mahakama ya Rufani
ilikuwa na majopo saba (7). Majopo hayo yaliketi mara 28 katika vikao 16
vilivyokuwa vimepangawa. Majaji wa
Rufani 24 akiwemo na Jaji Mkuu walishiriki vikao hivyo. Jumla
ya mashauri yaliyopangwa yalikuwa 1,003, yaliyosikilizwa yalikuwa 881 na yaliyoahirishwa
ni 122,” amesema.
Amezitaja baadhi ya sababu zilizopelekea kuahirisha
kwa mashauri hayo kama Mawakili au warufani kuomba kuwasilisha
nyaraka za ziada au nyongeza (supplementary record(s), hati za kuchelewa au
kufungua rufaa au maombi nje ya muda (certificate of delay) kutokuwa sahihi, kutofika
mahakamani kwa warufani kutokana na sababu mbalimbali au kutopatikana, kufariki
kwa warufani na kuahirisha ili kupisha
msimamizi au wasimamizi wa mirathi wateuliwe na kuunganishwa kwenye rufaa.
Msajili huyo ametaja mafanikio kadhaa yaliyopatikana
katika kipindi husika ikiwemo kuendelea kupungua kwa mashauri ya
mlundikano kutoka mashauri 707 (14%) Disemba 2021 mpaka mashauri 611 (11%) Juni
2022 na kuongezeka kwa kiwango au kasi ya kumalizika kwa mashauri (clearance
rate) kutoka asilimia 73 Disemba 2021 mpaka kufikia asilimia 92.9 mpaka Juni
2022.
Amesema pia kuwa kumekuwepo na hali ya kupungua kwa
mzigo wa mashauri kwa jopo (workload) kutoka mashauri 917 kwa jopo Disemba 2021
mpaka kufikia mashauri 859, kufanya vikao vyote kwa asilimia 100 kama
ilivyopangwa katika kalenda ya Mahakama ya Rufani na kuendelea kupungua kwa
mashauri yanayo ahirishwa kutoka mashauri 150 kwa kipindi cha Jan-Juni 2021
mpaka kufikia mashauri 122 kwa kipindi cha Jan-Juni 2022.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama
ya Tanzania, Bw. Steven Magoha aliwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama ya Rufani
kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bw. Solanus Nyimbi ambayo imesheheni
mambo mengi, ikiwemo jitihada zinazofanywa na Mahakama ya Tanzania kuboresha na
kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi.
Bw. Magoha ameuambia Mkutano huo kuwa Mahakama ya
Tanzania imeendelea na utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26)
wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama, ambapo katika mwaka
2021/2022 jumla ya miradi 60 ilitekelezwa katika ngazi mbalimbali.
“Miradi ya Ujenzi iliyokamilika ni pamoja na Vituo
Jumuishi vya Utoaji Haki (6) katika Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Morogoro,
Mwanza na Dodoma, ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi tatu (3) za Njombe,
Katavi, Lindi, ujenzi wa Mahakama za Wilaya sita (6) za Bahi, Chemba, Rungwe,
Makete, Wanging’ombe na Bunda na ujenzi wa Jengo la Chuo cha Uongozi wa
Mahakama Lushoto,” amesema.
Ametaja miradi mingine kama ujenzi wa Mahakama za
Mwanzo sita(6) za Matiri-Mbinga, Hydom-Mbulu, Ngerengere-Morogoro,
Mtae-Lushoto, Kibaigwa-Kongwa na Lugarawa-Ludewa, ujenzi wa nyumba mbili (2) za
Mahakimu Loliondo-Arusha na ujenzi wa Jengo la kuhifadhi Kumbukumbu-Tanga.
Bw. Magoha ametaja miradi inayoendelea kwa sasa kuwa ujenzi
wa Mahakama za Hakimu Mkazi Songwe na Mahakama za Wilaya nane (8) za Nanyumbu,
Namtumbo, Same, Tandahimba, Kilindi, Sikonge, Mwanga na Ngara na ujenzi wa
Mahakama za Mwanzo sita (6) za Chanika (Ilala), Kabanga (Ngara), Kimbe
(Kilindi), Nyakibimbili (Bukoba), Mlimba na Mang’ula (Morogoro).
Amesema pia kuwa kuna ukarabati wa Jengo la Mahakama
Kuu Tabora na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ujenzi wa Mahakama za Wilaya 18
katika Wilaya za Kakonko, Buhingwe na Uvinza (Kigoma), Butiama na Rorya (Mara),
Itilima na Busega (Simiyu), Songwe (Songwe), Mbogwe na Nyang’wale (Geita),
Kyerwa na Misenyi (Kagera), Gairo, Mvomero na Kilombero (Morogoro), Mkinga
(Tanga), Tanganyika (Katavi) na Kaliua (Tabora) na Ujenzi wa Makao Makuu ya
Mahakama na Nyumba za Majaji Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni