Na Stephen Kapiga- Mahakama, Mwanza
Rais wa Chama cha Majaji
na Mahakimu Tanzania (JMAT) Taifa, Mhe. John Kahyoza leo tarehe 4 Agosti amekutana
ofisini kwake katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini hapa na viongozi wapya
wa Chama hicho, tawi la Mkoa wa Mwanza waliochaguliwa hivi kwa ajili ya
kujitambulisha.
Viongozi hao ni Mhe
Monica Ndyekobora ambaye ni Mwenyekiti wa JMAT Mwanza pamoja na Mhe. Godfrey
Ndege ambaye ni Katibu wa JMAT Mwanza. Katika ziara hiyo, Rais wa JMAT Taifa,
ambaye pia ni mlezi wa Chama hicho Kanda ya Mwanza alipokea malengo ya viongozi
hao wapya katika kipindi cha uongozi wao.
Baadhi ya malengo
waliyowasilisha ni kuwawezesha wanachama wa JMAT, tawi la Mwanza kuielewa JMAT
kupitia vikao vyao, kutoa mada mbalimbali za kisheria wakati wa vikao, kutoa
elimu ya kisheria kwa wananchi na vikundi mbalimbali, kushiriki katika utalii
wa ndani na kuandaa miradi mbalimbali kwa ajili ya kutunisha mfuko wa Chama.
Akizungumza na viongozi
hao, Mhe. Kahyoza aliwashukuru kwa ujio wao na kwa mikakati mizuri waliojiwekea.
“Binafsi niwapongeze kwa kuchaguliwa kwenye nafasi hizo na niwapongeze kwa
mikakati na malengo ambayo mmejiwekea kama tawi ambayo naamini mnaweza
kuyatekeleza kwa ufanisi Zaidi,” alisema.
Amewashauri viongozi hao
kuunda kamati ya elimu itakayokuwa inaratibu zoezi zima la mada na nini
kitachoenda kufundishwa katika vikao vyao au kwa jamii. Alisema ni vizuri kuwepo
kwa kamati nyingine kama kamati ya maafa ili kuweza kuwasaidia wanachama pindi
wapatapo maafa.
Pia aliwashauri namna bora ya kuangalia michango ya wanachama katika tawi lao ili kuweza kukidhi malengo hayo waliojiwekea ikiwemo na hayo aliyowashauri.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni