Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo
tarehe 4 Agosti, 2022 amefungua Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania na kuwapongeza Majaji wote kwa mafanikio ya utekelezaji wa Mpango
Mkakati Wa Miaka Mitano (2016-2021) na Programu ya Uboreshaji, hatua ambayo
imechochea kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama.
Akizungumza na Majaji, wajumbe na wageni wengine
waalikwa katika siku ya kwanza ya Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika
Hoteli ya Nashera mjini hapa, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa kuna kazi kubwa ambayo
imefanyika katika kutoa huduma za haki kwa wananchi ambapo kiwango cha kuridhishwa
na huduma za Mahakama kimepanda kutoka Asilimia 61 (2015) hadi 78 (2019), kwa
mujibu wa Utafiti wa Kuridhika wa Watumiaji na Wateja wa Mahakama (Court Users
Surveys) za 2015 na 2019.
“Nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitachukua fursa
hii kuwapongeza Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa kazi yenu kubwa ambayo
imechangia utelezaji wa miaka mitano wa Mpango Mkakati wa Kwanza wa Mahakama na
mafanikio katika utekelezaji wa Programu ya Uboreshaji,” alisema Jaji Mkuu
ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo.
Amebainisha kuwa pamoja na viongozi wa Mahakama
kutopata nafasi ya kutafakari mafanikio makubwa waliyopata kutokana na huduma wanazotoa
kila siku, wapo wengine nje ya Mhimili wa Mahakama ambao wameyaona mafanikio
hayo ambayo yametajwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye Andiko la Benki
ya Dunia lililozaa nyongeza ya mradi wa uboreshaji.
“Benki ya Dunia wametambua mafanikio yetu. Chini ya
Vigezo vya Ufanisi (Efficiency Indicators), vigezo hivi vimeonyesha kuwa uboreshaji
umeleta usimamizi bora wa mashauri ambao unatoa huduma kwa haraka kwa watumiaji
wa Mahakama. Kwa kurahisisha kanuni za uendeshaji wa mashauri, Mahakama
imefanikiwa kupunguza hatua nyingi ambazo mashauri hupitia kabla ya
kukamilika. Hatua katika taratibu za kimahakama zimepungua kutoka 38 hadi 21,”
amesema.
Amesema kuwa kuanzishwa kwa mfumo wa usimamizi wa
mashauri kwa njia ya kielektroniki (JSDS2) umetajwa kuwa ni mafanikio yanayoonekana
ambapo matumizi ya Video Conference (Mkutano Mtandao) ambayo yamesaidia
kusikiliza mashauri ya Wafungwa na Mahabusu na pia kupokea ushahidi wa
Mashahidi kutoka nje ya nchi ni mafanikio makubwa. Kadhalika, Jaji Mkuu amesema
kuwa kumekuwepo na mfumo imara wa mafunzo na mfumo wa upimaji utendaji kazi
ambapo Majaji na Mahakimu wamejipangia idadi ya mashauri ya kusikiliza kila mwaka.
“Vigezo vya kupunguza mlundikano vililenga kushusha mlundikano
hadi asilimia 0.05. Ni mafanikio kwa Mahakama kuweza kushusha asilimia hii hadi
0.15. Lengo liliwekwa la kuhakikisha idadi ya siku ambazo shauri linakuwa
mahakamani kabla ya kukamilika ishuke hadi siku 350. Lengo hili limefanikiwa
kwa vile shauri linadumu mahakamani kwa siku 338, ambazo ni bora zaidi ya lengo
la siku 350,” aliwaambia wajumbe wa Mkutano huo.
Jaji Mkuu amesema pia kuwa kuelekea Mahakama Mtandao, Mahakama
ya Tanzania imeendelea kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi kwa kuimarisha
mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), huku akibainisha lengo
la msingi ni kufikia Mahakama isiyotumia karatasi (paperless court), hivyo ili
kufikia lengo hilo hawana budi kuendelea na maandalizi bila kurudi nyuma licha
ya changamoto zinazoweza kujitokeza.
Katika Mkutano huo, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Majaji
hao kuwa kwa nafasi zao mmoja mmoja, au kwa ujumla wao wapo katika kilele
(APEX) cha utoaji wa haki ambapo uamuzi wanaotoa una nguvu katika nchi, hivyo akabainisha
kila Jaji wa Rufani ni Kiongozi. “Jaji wa Rufani Mstaafu wa Uingereza aliwahi
kutoa mada nchini Bahrain kuhusu Judicial Leadership and Reform (Uongozi wa
Mahakama na Uboreshaji). Aliyoyasema, yanafafanua nafasi za Majaji katika nafasi
za Kiuongozi,” alisema.
Akimnukuu Jaji huyo wa Uingereza, Jaji Mkuu amesema
kuwa kazi za Majaji wa Rufani za utoaji haki amezitaja kuwa zinawapa uongozi
(leadership) katika kuendeleza sheria, kufafanua sheria, kuongoza katika
tafsiri na kuweka ukomo wa mabishano kuhusu tafsiri sahihi ya sheria na pia Majaji
wanapojizuia kuingilia kazi za Kibunge ya utungaji wa sheria, wanakuwa wakidhihirisha
uongozi.
“Jaji huonyesha uongozi anapotoa tafsiri ambayo
inafungua mipaka mipya katika ufahamu wa sheria. Majaji huonyesha Leadership
kila wakati wanapoheshimu mamlaka ambayo Katiba na Sheria zimetoa kwa Bunge,
Serikali, kwa Taasisi nyingine na hata kwa watumishi wa umma. Kila siku Jaji unaonyesha
leadership unaposimamia jalada la shauri ulilopangiwa na unaonyesha leadership
ukiwa mahakamani unaposimamia rufani au maombi,” amesema.
Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wamealikwa
katika Mkutano huo. Miongoni mwa viongozi hao ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Mustapher Siyani, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt, Jaji wa Mahakama ya Rufani
Mstaafu, Mhe. Edward Rutakangwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Bw. Steven
Magoha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni