Na Tiganya Vincent-Mahakama
Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg ametoa
wito kwa maafisa wa Mahakama nchini kutumia kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa
Majaji na Mahakimu kinachohusu ukatili wa kijinsia ili kuwawezesha wanawake na
wasichana kupata haki zao wanapokuwa katika matatizo.
Mhe. Sjoberg ametoa kauli jana tarehe 3 Agisti, 2022 jijini
Dar es Salaam alipokuwa akitoa salamu za kuwaaga wanachama wa Chama cha Majaji
na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na viongozi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women ) mara baada ya
kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini wakati wa kikao cha siku
moja cha wadau hao.
Amesema Kitabu hicho kinatoa fursa na mbinu bora za
kushughulikia masuala yanasababisha ukosefu wa haki na ukatili wa kijinsia kwa
wanawake na wasichana nchini Tanzania.
Aidha, Mhe. Sjoberg ameongeza kuwa nchi ya Sweden
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau
wengine katika kusaidia mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kutetea usawa
wa kijinsia.
“Upatikanaji wa haki ni haki ya msingi ya binadamu na
kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha upatikanaji haki sawa kwa wote bila kumuacha
mtu nyuma,” amesisitiza.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake
nchini(TAWJA) Mhe. Joaquine De-Mello amesema Kitabu hicho kinatoa mwanga juu ya
ukubwa na tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na wasichana na uhusiano wa mfumo
dume unavyochangia tatizo hilo.
Amesema Kitabu kitawasaidia maofisa wa Mahakama
kufanya rejea thabiti wakati wa matumizi ya sheria na kuwaongoza katika masuala
ya kiutendaji wa kukabiliana na dhana potofu zinazokwamisha upatikanaji kwa
wanawake Mahakamani.
Mhe. De-Mello ameishukuru Sweden kwa kuendelea
kusaidia katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya mapambano dhidi ya ukatili wa
kijinsia na maeneo mengine hapa nchini.
“Kwa kheri mpendwa wetu Anders Sjoberg Balozi wa
Sweden nchini Tanzania unayemaliza muda wako!”amesema.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha
na masuala wanawake (UN Women) Hodan Addou amesema Serikali kwa kushirikiana na
Mahakama na wadau wengine wanaweza kuhakikisha vikwazo vinavyowakabili wanawake
na wasichana katika kupata haki vinaondolewa.
Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama mara baada ya kutoa salamu zake jana Jijini Dar es salaam za kuwaaga wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake (UN Women ) mara baada ya kumaliza muda wake kufanya kazi ya Ubalozi hapa nchini.
(Picha na Tiganya Vincent-Mahakama).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni