Jumatano, 3 Agosti 2022

MKUTANO WA NUSU MWAKA MAHAKAMA YA RUFANI WAIVA

Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro

Maandalizi ya Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 4 Agosti, 2022 mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, yamekamilika.

Mwenyekiti wa maandalizi kuelekea kwenye Mkutano huo, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kevin Mhina amesema leo tarehe 3 Agosti, 2022 kuwa tayari viongozi wakuu wa Mahakama pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani wameshaanza kuwasili.

“Maandalizi ya Mkutano wetu yameshakamilika. Tayari tumeshampokea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani wameshaanza kuwasili kwenye eneo la Mkutano,” amesema Mhe. Mhina, ambaye ndiye Katibu wa Mkutano huo.

Amemtaja kiongozi mwingine ambaye ameshawasili katika eneo la Mkutano ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Mahakama ya Tanzania ambao wamealikwa kwenye Mkutano huo.

Viongozi wengine waalikwa ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, ambaye tayari yupo mjini hapa kwa ajili ya Mkutano huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili mbalimbali na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Bw. Steven Magoha.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo tarehe 3 Agosti, 2022, taarifa na mada mbalimbali zitawasilishwa katika Mkutano huo wa siku mbili unaotarajiwa kumalizika tarehe 5 Agosti, 2022. Katika siku ya kwanza, taarifa kadhaa zitawasilishwa, ikiwemo inayohusu mashauri kwa kipindi cha nusu mwaka (Januari-Juni, 2022) na ile kuhusu masuala ya kiutumishi na utawala.

Miongoni mwa taarifa zitakazowasilishwa siku ya pili ya Mkutano ni ile inayohusu uboreshaji, mpango mkakati wa awamu ya pili ya mradi wa Benki ya Dunia, hali ya mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na matumizi yake kuelekea Mahakama Mtandao. Pia kutakuwepo na uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji wabobezi, akiwemo Jaji wa Mahakama ya Rufani mstaafu, Mhe. Edward Rutakangwa.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili tayari kwa ajili ya Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 4 Agosti, 2022  mjini Morogoro.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasalimia watumishi wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro waliofika kumpokea leo tarehe 3 Agosti, 2022.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akikaribishwa na mwenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe baada ya kuwasili kwenye eneo la Mkutano.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akisalimiana na watumishi wa Mahakama waliofika kumpokea.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akibadilishana mawazo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe mara baada ya kuwasili kwenye eneo la Mkutano. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe, Mustapher Siyani.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustaher Siyani (katikati) akibadilishana mawazo na wenyeji wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (kushoto) na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda hiyo, Mhe. Messe Chaba.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akibadilishana mawazo na viongozi kadhaa waliokuja kumpokea. 
Sehemu ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania kutoka Makao Makuu Dar es Salaam na Kanda ya Morogoro waliofika kumpokea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Omar Makungu akikaribishwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Happiness Ndesamburo mara baada ya kuwasili kwenye eneo la Mkutano.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Stella Mugasha akiwasili katika eneo la Mkutano. Kulia ni Katibu wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Venance Mlingi.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sam Rumanyika akiwasili katika eneo la Mkutano.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Abrahaman Mwampashi akiwasili katika eneo la Mkutano hapa mjini Morogoro.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Ignas Kitusi akiwasili katika hoteli maarufu mjini Morogoro mahali ambapo Mkutano wa Nusu Mwaka wa Mahakama ya Rufani utakapofanyikia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni