Na Mary Gwera, Mahakama
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick leo tarehe 02 Agosti, 2022 amefungua Mafunzo elekezi kwa Makatibu Mahsusi wapya wa Mahakama na kuwataka Watumishi hao kuwa tayari kufanya kazi katika vituo watakavyopangiwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel wilayani Lushoto, Bi. Beatrice amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya Watumishi kuwasilisha sababu au malalamiko mbalimbali kuomba uhamisho kutoka mahali walipopangiwa kwakuwa mhusika hajapenda eneo alilopangiwa.
“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya Watumishi mara wanapoona kuwa wamepangiwa vituo wasivyopenda, wanaleta sababu lukuki na nyingine za uongo ili tu aweze kupata uhamisho,” amesema.
Ameongeza kwa kuwataka Watumishi hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi ili kufanya kazi kwa amani.
Mafunzo hayo ya siku tano (5) yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto ambacho ndio kinaendesha mafunzo hayo, washiriki wa mafunzo ni Watumishi wa Kada za Afisa Utumishi/Tawala, Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani, Maafisa TEHAMA, Maafisa Ugavi pamoja na Madereva.
Aidha; mafunzo ya namna hii ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza ni mwendelezo wa Mafunzo yaliyotolewa kwa kundi la Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu wapya yaliyomalizika tarehe 29 Julai, 2022.
Mada zinazotarajiwa kutolewa katika Mafunzo hayo ni pamoja na Muundo na tamaduni za kimahakama, Mpango Mkakati wa Mahakama na Mpango wa Uboreshaji Huduma za Mahakama, Huduma kwa wateja, Maadili ya Utumishi wa Umma na wa Mahakama, Ubunifu katika kazi na nyingine.
MATUKIO KATIKA PICHA HAFLA YA UFUNGUZI WA MAFUNZO ELEKEZI KWA MAKATIBU MAHSUSI
Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo Elekezi wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo katika picha).
(Picha na Ibrahim Mdachi, IJA-Lushoto)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni