Na Faustine Kapama-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 27 Septemba, 2022 amekutana na Jaji Mstaafu
wa Uingereza, Mhe. Nic Madge na kufanya naye mazungumzo mafupi kuhusu mambo mbalimbali
ya kimahakama, ikiwemo uwepo wa programu ya kujenga mfumo endelevu wa mapambano
dhidi ya rushwa nchini.
Jaji huyo ambaye aliongozana
na maafisa kutoka Ubalozi wa Uingereza, akiwemo Mshauri wa Utawala, Bw. Simon
Charters na Mtaalamu wa Mashtaka, Bi. Claire Harris alifika ofisini kwa Jaji Mkuu
katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kujitambulisha na kumweleza kuhusu programu hiyo.
Programu hiyo inayofadhiliwa
na Ubalozi wa Uingereza inahusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo kufanya mafunzo
ya kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu, matumizi sahihi ya adhabu kwa mujibu wa
mwongozo wa utoaji wa adhabu (Sentencing Mannual) na uendeshaji wa kongamano la
wadau wa sheria kuhusu mambo kadhaa ya haki jinai katika kipindi cha Wiki ya Sheria
(Law Week Symposium).
Hivyo, Jaji Nic
alijitambulisha kwa Jaji Mkuu kama mtaalamu ambaye amekuja kuomba kazi ya kutekeleza
pragramu hiyo kama ilivyopendekezwa na Ubalozi wa Uingereza kwa Mahakama ya Tanzania
kuingia naye mkataba aweze kutoa uzoefu wake katika maeneo hayo matatu, ikiwemo
hilo la kuwajengea uwezo Majaji na Mahakimu kusikiliza mashauri ya rushwa kubwa
(grant corruption cases).
Kwa upande wake, Jaji
Mkuu alifurahia ujio wa Jaji Mstaafu huyo na kumweleza kuwa Mahakama ya Tanzania
ipo tayari kushirikiana naye kwenye hayo maeneo. Akizungumzia kuhusu kongamano
alilolitaja Jaji Nic, Mhe. Prof. Juma alimweleza mgeni wake kuwa imekuwa utamaduni
kwa Wiki ya Sheria kukutanisha wadau mbalimbali wa Mahakama.
Aliwataja baadhi ya wadau
hao kama Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya
Wakili Mkuu na wengine wengi. Hivyo akaridhia mchakato huo ukamilike ili watumishi
wa Mahakama waweze kupata uzoefu kwenye maeneo hayo kwa lengo la kuboresha
utendaji wa kazi.
Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani
na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo,
ambaye ndiye Kiongozi wa Timu kwenye suala hilo alifika ofisini kwa Jaji Mkuu
akiogozana na wageni hao pamoja na watumishi wengine wawili wa Mahakama, akiwemo
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Stephen Magoha na Afisa
Utumishi, Bw. Nkuruma Katagira, na kueleza
lengo kuu la ujio wao.
Jaji Kihwelo kwa mara nyingi
amekuwa akiratibu ushirikiano wa kitaaluma kupitia IJA na kwenye mradi wa programu
ya kujenga mfumo endelevu wa mapambano dhidi ya rushwa nchini (BSAAT) amekuwa
kama kiunganishi muhimu katika kusimamia mafunzo ya Majaji na Mahakimu kwa
kushirikiana na taasisi zile ambazo zinatumia mradi huo.
Hivi karibuni, Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto kilichopo mkoani Tanga kiliendesha mafunzo yaliyowaleta
pamoja Mahakimu 43 kuhusu namna bora ya utoaji wa adhabu na utekezaji wa amri
za Mahakama.
Mafunzo hayo
yaliyoratibiwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo hicho kupitia
ufadhili wa Programu ya Kitaifa ya Kuzijengea Uwezo Taasisi za Umma Tanzania
zinazohusika na Kuzuia na Kupambana na Rushwa (BSAAT) yalilenga kuwajengea
uwezo Mahakimu hao kutekeza jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akimpokea mgeni wake,Jaji Mstaafu wa Uingereza, Mhe. Nic Madge alipowasili ofisini kwake leo tarehe 27 Septemba, 2022 kwa mazungumzo mafupi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akisalimiana na Mshauri wa Utawala, Bw. Simon Charters alipowasili ofisini kwake.
Mshauri wa Utawala kutoka Ubalozi wa Uingereza, Bw. Simon Charters akieleza jambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni