Jumanne, 27 Septemba 2022

JAJI MFAWIDHI BUKOBA UTAMPENDA

·Atoa ng’ombe kwa watumishi baada ya mashauri 400 kuondoshwa

Na Ahmed Mbilinyi – Mahakama, Bukoba

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga ametekeleza ahadi yake ya kutoa zawadi ya ng’ombe mmoja kwa watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo baada ya kufanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa mashauri yanayoendelea mahakamani.

Ng’ombe huyo alichinjwa katika Tamasha la Ngombe Day lilofanyika mwishoni wa wiki katika eneo la Kabuhara Beach iliyopo Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera. Mhe. Dkt. Kilekamajenga alitoa ahadi hiyo wakati ya kikao kazi kilichofanyika mwaka 2021 ambapo Mahakama Kuu Bukoba ilikuwa na mashauri zaidi ya 900 yaliyokuwa yanaendelea.

Jaji Mfawidhi huyo akaahidi kuwa kama mashauri hayo yakiPungua hadi kufikia 600 katika Mahakama hiyo atatoa zawadi ya ng’ombe mmoja. Baada ya kikao hicho timu ya Majaji, Naibu Msajili, Mtendaji wa Mahakama pamoja na watumishi wote wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba wakaandaa mkakati pamoja na mpango kazi wa kuwezesha kupunguzwa kwa mashauri hayo.

Katika mkakati huo, majalada asilia yaliitishwa toka Mahakama za chini, Mabaraza ya Ardhi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) na kisha vikao vya kuondosha mashauri vikaandaliwa na kuendeshwa na Majaji. Vikao hivyo vilikuwa na mafanikio makubwa ambapo asilimia 98 ya mashauri yaliyopangwa yalimalizika.

Mwanzoni mwa mwezi Juni 2022 moshi mweupe ukaanza kuonekana kwa kazi kubwa iliyofanyika, ambapo Mahakama Kuu Bukoba ikabaki na mashauri 600 yaliyokuwa yakiendelea. Ndipo Mhe. Dkt. Kilekamajenga akatoa tamko la kutoa ng’ombe kutimiza ahadi yake.

Kufuatia hatua hiyo, kamati ya maandalizi ikaundwa kuratibu tamasha, ambalo kushirikisha michezo mbalimbali, wakati huo huo kazi ya kushughulikia mashauri ikiwa inaendelea kufanyika na hadi kufikia mwanzoni mwa mwezi Septemba 2022, Mahakama Kuu Bukoba ilibaki na mashauri yanayoendelea 495 tu.

Hatimaye tamasha likafanyika huku watumishi wa Mahakama wakiburudika na nyama iliyochinjwa pamoja na michezo mbalimbali iliwemo mashindano ya kula nyama na kunywa soda, Mpira wa Miguu kwa Wanawake na Wanaume huku timu husika zikiganyika kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Kadhalika, kulikuwepo na mbio za mita mia (100), mbio za kupokezana vijiti, mashindano ya kuogelea pamoja na mchezo wa meza (pool table).


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga akitoa neno la ufunguzi wa Tamasha la Ng'ombe.

Watumishi wa Mahakama  Kanda ya Bukoba, ambao ni wachezaji wa Mpira wa Miguu wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza mchezo huo katika Tamasha la Ng'ombe. Picha ya juu ni wachezaji waliojiita Simba na chini ni wachezaji waliojiita Yanga.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Bukoba, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga (wa tisa kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya wanamichezo katika tamasha hilo.


Maoni 1 :