Na Arapha Rusheke-Mahakama, Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe.
Gerson Mdemu amesisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa kwa Mahakimu kuhusu
utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa magaidi, biashara haramu ya
wanyamapori kutokana na athari zake katika uchumi wa Taifa ili waweze kutoa
uamuzi sahihi kukomesha uhalifu huo wa kimataifa.
Mhe. Mdemu alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anafungua
mafunzo kwa Mahakimu Wakazi wa Tanzania Bara kuhusu makosa hayo. Jaji Mdemu
alibainisha kuwa ongezeko la kasi la utandawazi na mwingiliano wa shughuli za
kifedha umefanya utakatishaji fedha kuwa miongoni mwa matatizo ya kimataifa.
"Kwa hiyo, hali hii inachagiza hitaji muhimu la kuwepo mikakati
na juhudi za pamoja kupambana na makosa haya ya utakatishaji fedha. Nchi lazima
zishiriki katika vita hivi,” alisisitiza.
Amesema ni kwa kutambua ukweli huo kwamba mashirika kadhaa
ya kimataifa yameandaa mapendekezo na mbinu bora kusaidia nchi zote kuimarisha
juhudi zao za kupambana na makosa ya utakatishaji fedha.
"Nyinyi mkiwa miongoni mwa maofisa wa Mahakama, ufahamu
wa maarifa na ujuzi kuhusu makossa haya, kwa hakika, utaboresha uamuzi wenu kwa
kutumia maarifa na ujuzi huo," Jaji Mdemu aliwaambia washiriki wa mafunzo
hayo.
Alisema mafunzo hayo yamefanyika kutokana na changamoto na
athari mbaya zinazotokana na utakatishaji fedha, biashara haramu ya wanyamapori
na ufadhili wa ugaidi.
"Mnafahamu kwamba, athari za utakatishaji fedha kama
uhalifu katika uchumi wa taifa haziwezi kupuuzwa. Kwa hiyo, haja ya kuongeza
kiwango cha uelewa cha kutosha miongoni mwa Mahakimu inapaswa kutiliwa mkazo,”
alisema.
Jaji Mdemu aliendelea kubainisha kuwa ni kwa njia ya
utakatishaji fedha ambapo shughuli haramu za fedha zinahalalishwa na kuchangia
kwa kiasi kikubwa kufanya uhalifu ulipe. Alisema utakatishaji wa fedha pia
unachangia kudhoofisha uadilifu wa mfumo wa fedha, taratibu za soko na uchumi
wa taifa zima.
"Utakatishaji fedha, biashara haramu ya wanyamapori na
kufadhili ugaidi ni matokeo mabaya ya uchumi, haswa kwa nchi zinazoendelea kama
uchumi wetu. Athari hizi kwa kawaida ni pamoja na ongezeko lisiloelezeka la
mahitaji ya bidhaa na huduma ambazo zinaweza kutumika kuhalalisha kiasi kikubwa
cha fedha zinazotokana na uhalifu,” alisema.
Ni matumaini yake kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki
kuboresha ujuzi wao juu ya utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi na mbinu
haramu za biashara ya wanyamapori, mbinu zinazoweza kubuniwa na kutumiwa
kushughulikia vitendo hivyo na namna bora ya kushughulikia mashauri yanayohusu makosa
hayo watatu.
Washiriki wa mafunzo hayo ya siku tano yamewakutanisha
Mahakimu Wakazi kutoka Mahakama Kuu Kanda za Dar es Salaam, Bukoba, Dodoma,
Iringa, Mbeya, Moshi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Songea, Morogoro na Sumbawanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni