Na Emmanuel Oguda – Shinyanga
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kutoka Mikoa
ya Shinyanga na Simiyu hivi karibuni walitembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kuhudhuria kipindi cha maswali na majibu na kujifunza shughuli
mbalimbali za kibunge.
Katika ziara hiyo, wanachama hao walifarijika kuona namna Bunge linavyoendeshwa.
Afisa Uhusiano wa Bunge, Bw. Deogratius Simba aliwapitisha katika maeneo mbalimbali
ikiwemo ukumbi wa zamani wa Bunge unaojulikana kwa jina la Ukumbi wa Pius
Msekwa pamoja na maeneo mengine na kutoa fursa kwa wanachama hao kuuliza
maswali kuhusiana na shughuli za uendeshaji wa Bunge.
Wakati huo huo, wanachama hao walipata fursa ya kutembelea Jengo la
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania linaloendelea kujengwa na kujionea ukubwa
wake ambapo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mhandisi Qeen Mduma aliwaeleza wanachama
hao kuwa jengo hilo linajumuisha Mahakama ya Juu (Supreme Court), Mahakama ya
Rufani, Mahakama Kuu (Masijala Kuu) pamoja na Ofisi za Utawala (Head Quarters).
Kadhalika, jengo hilo litakuwa na maeneo mbalimbali ikiwemo viwanja vya mpira.
Aliongeza kuwa ukubwa wa eneo ni ekari 45 na jengo hilo ni la sita (6) kwa ukubwa
duniani.
Nae Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe Dkt Adam
Mambi aliwapongeza wanachama hao kwa ziara yao ya kutembelea Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania pamoja na kupata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa
Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
“JMAT Dodoma tunalo la kujifunza kutoka kwenu, nina imani pia wanachama
wa JMAT Kanda ya Dodoma wataiga mfano huu kutoka kwa JMAT Shinyanga,” alisema.
Picha ya pamoja ya wanachama wa JMAT Shinyanga, Simiyu na Dodoma walipotembelea jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni