Na Faustine Kapama-Mahakama
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) jana tarehe
27 Septemba, 2022 imeanza mazoezi ya pamoja kwa kujumuisha wachezaji kutoka Mikoa
mbalimbali nchini kujiandaa na mashindano yajao ya Shirikisho la Michezo ya
Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika jijini Tanga
kuanzia tarehe 1 Octoba, 2022.
Akizungumza katika Viwanja vya Shule ya Sheria kwa
Vitendo (Law School) jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Robert
Tende amesema wanamichezo wote walioitwa kutoka mikoani wameanza mazoezi ili kuwawezesha
walimu kuchagua majina ya wale watakaoshiriki kwenye michezo mbalimbali katika mashindandano
hayo.
Tende amekiri kuwa walimu watakuwa na kazi kubwa ya kuchagua
wachezaji watakaoshiriki kwenye mashindano hayo kwa vile vijana wote mwaka huu wapo
vizuri, wana ari kubwa na wote wanajituma katika mazoezi.
“Safari hii tunawachezaji wazuri sana kwenye kila
mchezo, wote wanajituma na wanafanya vizuri kwenye mazoezi. Walimu wana kazi
kubwa kupata wachezaji watakaopeperusha bendera ya Mahakama kwenye mashindano haya
mwaka huu,” alisema.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza Mahakama Sports imedhamilia
kuchukua vikombe vyote vya mshindi wa kwanza kwenye michezo yote watakayoshiriki,
hivyo amewahimiza wanamichezo wote kuzingatia programu zinazotolewa na walimu
ili waweze kujiandaa vyema kushiriki kikamilifu kwenye mashindano hayo.
Amewakumbusha wanamichezo wote kuwa kwa mujibu wa kanuni
za mashindano kila mshiriki anatakiwa kuwepo kwa kipindi chote kilichopangwa,
hivyo akawatahadhalisha kujipanga vyema ili wasitolewe kwenye hatua za mwanzo na
kuwafanya kuwa wasindikizaji wawashiriki wengine.
“Kanuni za mashindano SHIMIWI zinamtaka kila mshiriki
kubaki kwenye kituo tangu siku ya kwanza hadi ya mwisho, hata kama umetolewa
kwenye hatua za awali. Kwa hiyo, nawaomba wanamichezo wenzangu kujiandaa
kikamilifu. Mwaka huu hatutaki kupoteza kitu,” alisema.
Michezo ambayo Mahakama Sports inatarajia kushiriki ni
Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe,
Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni