Na Faustine Kapama-Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewasihi viongozi wa Mahakama kutambua
nafasi walizonazo kwa jamii na ndani ya Mhimili huo wa utoaji haki na kufanya
uamuzi sahihi kwa usahihi ili kumsaidia Mtanzania kupata haki anayostahili kwa
wakati.
Prof. Ole Gabriel ametoa
wito huo leo tarehe 26 Septemba, 2022 alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tatu kuhusu
uongozi bora yanayotolewa kwa wajumbe wa menejimenti ya Mahakama ya Tanzania
inayojumuisha wakuu wa idara na vitengo mbalimbali yanayofanyika katika Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia Temeke jijini Dar es Salaam.
“Elewa hautakumbukwa kwa
sababu ya nafasi yako, utakumbukwa kwa mchango wako katika kuboresha uamuzi
unaofanywa. Hakikisha uamuzi unaofanya unamsaidia Mtanzania wa ngazi yoyote
ambaye anatafuta haki yake. Onyesha thamani yako, ndiyo utakayokufanya kukubukwa
na siyo rangi yako, sura yako wala hata vyeti vyako. Utakumbukwa kwa mchango
wako katika jamii,” alisema.
Amesema lengo kubwa la kuandaa
mafunzo hayo ni kuhakikisha viongozi hao wanaongea lugha moja, hasa katika
kuwatumikia wananchi kwa vile mchango wao katika mchakato mzima wa utoaji wa
uamuzi ni muhimu na wenye tija, kwani maendeleo yanayoonekana na yale
yanayotarajiwa ndani ya Mahakama hayawezi kupatikana bila wao.
“Haiwezekani Mtendaji
Mkuu, Msajili Mkuu hata Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi tukawa na mafanikio yoyote
bila kuhakikisha kuwa nyinyi ambao ni sehemu ya menejimenti tunaongea lugha
moja, tunakwenda kwenye kasi inayofanana na tunakwenda kwenye masafa na mwelekeo
unaofanana,” alisema.
Mtendaji Mkuu huyo
aliwaambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa mafanikio yote yanayoonekana ndani ya
Mahakama yanatokana na mchango wao mkubwa. Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel, kuzungumzia
uongozi bora katika taasisi yoyote ni kuona kwamba mambo yanafanyika kwa
usahihi unaotakiwa, hivyo ni matamanio yake kuona viongozi hao wanafanya mambo
sahihi kwa usahihi.
“Nyinyi sio bomba la
kupeleka mambo kwa viongozi wenu, bali ni watu wa kusaidia kuchakata na kuyapeleka
na maoni na mapendekezo ili kufanya uamuzi. Mfano, kama wewe ni mkuu wa idara
au mkuu wa kitengo, haitapendeza kuwa mtu wa kupokea mambo na kufikisha kwa
kiongozi bila wewe kuweka thamani yako kwenye mchakato wa kufanya uamuzi.
Usipoweka thamani yoyote hufai na huna thamani yoyote,” alisema.
Kadhalika, Prof. Ole
Gabriel aliwaomba viongozi hao kuzingatia Mpango Mkakati wa Mahakama na maelekezo
mazuri yanayotolewa na Jaji Mkuu Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma ili kuhakikisha haki yenye tija inapatikana kwa uwazi na kwa wakati.
“Hatuwezi kwenda vizuri
bila nyinyi, nyinyi hasa ndiyo mataili yaliyobeba mafanikio ya Mahakama. Kila
mtu kwenye idara yake afikirie hiyo, lazima ujiulize una thamani gani kwa ngazi
yoyote ile, Mkurugenzi Msaidizi, Mkuu wa Kitengo, hata mimi Mtendaji Mkuu
lazima nijiulize nina thamani gani ndani ya Mahakama,”alisema.
Akawashauri pia kuwa sehemu ya majibu na majawabu katika kufanya uamuzi na siyo kuwa sehemu ya matatizo. “Ndiyo maana wale Wachina wakasema haijalishi rangi ya Paka, mweusi, mwekundu, maadamu anakamata Panya ni Paka. Nasi tunaseme kwenye uongozi bora haijalishi kwamba upo kwenye nafasi gani, maadamu unatatua tatizo wewe ni kiongozi,” alisema Mtendaji Mkuu huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngungulu alisema mafunzo hayo ya siku tatu yanalengo la kuwajengea viongozi hao uwezo katika nyanja mbalimbali ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu. “Tunatarajia mafunzo haya yatawasaidia viongozi hawa kuleta mabadiliko ya kifikra na kuwapa weledi katika kutekeleza kazi zao,” alisema.
Katika mafunzo hayo, wajumbe hao wa menejimenti watapitishwa na wazeshaji mahiri akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. John Utamwa kwenye mada mbalimbali, ikiwemo kuelewa utamaduni wa Mahakama, fikra za kimkakati na usimamizi wa mabadiliko na jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni