Jumamosi, 24 Septemba 2022

MAHAKAMA SPORTS YATUMA SALAMU TANGA

·Yatangaza rasmi kushiriki mashindano SHIMIWI

·Yajichimbia kujifua kwenye michezo nane

Na Faustine Kapama-Mahakama

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 24 Septemba, 2022 imefanya Mkutano Mkuu wa mwaka kujadili mambo mbalimbali ya kiutendaji, ikiwemo kushiriki kikamilifu kwenye mashindano yajao ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kufanyika jijini Tanga kuanzia tarehe 1 Octoba, 2022.

Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi namba moja katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Wilson Dede amewahimiza wanamichezo wote kujiandaa kikamilifu ili kupata ushindi wa kishindo kwenye michezo yote nane watakayoshiriki kwenye mashindano ya SHIMIWI mwaka huu. Ameitaja michezo hiyo kuwa ni Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli.

“Mwaka jana kwenye mashindano haya tulishiriki kwenye michezo kadhaa na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza na kupata makombe mawili kwenye Kamba Wanaume na Kamba Wanawake. Mwaka huu tunataka ushindi na makombe kwenye michezo yote tunayoshiriki, uwezo wa kufanya hivyo tunao na upo mikononi mwetu,” aliwaambia wajumbe wa Mkutano huo.

Mwenyekiti Dede aliwasihi wanamichezo wenzake kuendeleza ushirikiano walionao na kudumisha nidhamu ya mchezo tangu wakiwa kwenye mazoezi, kambini na kwenye uwanja wa mashindano, kwani kwa kufanya hivyo nuru ya mafanikio itaweza kuwaangaza na hatimaye kutimiza matarajio ya Mwajiri, yaani, Mahakama ya Tanzania.

“Mwajiri wetu ana matarajio makubwa sana kutoka kwetu na ndiyo maana ametupa kibali cha kushiriki. Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel hataki tuishie kwenye mashindano ya SHIMIWI pekee, anataka twende mbali zaidi ya hapa. Azma yake ni kushiriki kwenye Ligi Kuu kwenye michezo yote. Kwa hiyo, ili tuweze kufikia matarajio haya hatuna budi kushikamana, kupendana na kuzingatia nidhamu wakati wote,” alisema.

Mwenyekiti huyo aliwatakia wanamichezo wote afya njema na maandalizi mema ya mazoezi na kuwasihi kuzingatia programmu zinazotolewa na walimu ili waweze kujiandaa vyema kushiriki kikamilifu kwenye mashindano hayo. Amewatangazia kuwa Timu ya Mahakama Sports itaondoka kuelekea Tanga kushiriki mashindano ya SHIMIWI muda wowote mara baada ya taratibu za kiutawala kukamilika.

Akizungumza kwa kifupi kwenye Mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Theodosia Mwangoka amewashukuru wanamichezo wenzake kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kwenye Mkutano huo na kuwaomba kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi. Amewasihi kutunza siri za kambi na masuala mengine nyeti ambayo hayafai kujadiliwa nje ya Mkutano.

Mbali na Mwenyekiti na Naibu Katibu Mkuu, viongozi wengine waliohudhuria Mkutano huo ni Wajumbe watatu wa Kamati Tendaji Mchawi Mwanamsolo, Judith Mwakyalabwe na Rhoida Makassy, Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole, Afisa Michezo kutoka Utawala Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Mhasibu Rajabu Diwa. Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka na Katibu Mkuu Robert Tende hawakuweza kuhudhuria Mkutano huo kwa vile walikuwa na Mkutano mwingine uliokuwa unafanyika jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Mahakama Sports, Wilson Dede akisisitiza jambo alipokuwa akiongea kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka leo tarehe 24 Septemba, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Theodosia Mwangoka na kushoto ni Meneja wa Timu Antony Mfaume.
Naibu Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Theodosia Mwangoka (katikati) akizungumza katika Mkutano huo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede na kushoto ni Mjumbe wa Kamati Tendaji Rhoida Makassy.
Meneja wa Timu Antony Mfaume akisisitiza masuala ya nidhamu alipokuwa akiongea kwenye Mkutano huo. Kulia ni Mwanyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede na kushoto ni  Afisa Michezo kutoka Utawala Nkuruma Katagira.

 Afisa Michezo kutoka Utawala Nkuruma Katagira akijibu baadhi ya hoja za kiutawala zilizoibuliwa kwenye Mkutano huo. Kulia ni Meneja wa Timu Antony Mfaume na kushoto ni Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Mahakama Sports Mchawi Mwanamsolo akeleza uzoefu wake katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wakiwa kambini.

Sehemu ya wajumbe (juu na chini) waliohudhuria Mkutano huo.

Sehemu nyingine ya wajumbe wa Mkutano (juu na chini) wakifuatilia matukio mbalimbali.


Sehemu nyingine (picha moja juu na mbili chini) wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye Mkutano huo.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni