Na Castilia Mwanossa- (SAUT)
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma amesema jitihada na
nguvu za Pamoja zinahitajika kutoka kwa wadau wa ndani na nje ya nchi ili
kuweza kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Ameyasema hayo leo 22 Septemba
jijini Dar es salaam alipokuwa kwenye kongamano lililowakutanisha
wadau mbalimbali kujadili namna bora ya kushughulikia kesi za ukatili wa
kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa kike ili kuwawezesha kupata haki.
Aidha, amesema kwamba Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na Madawa
ya Kulevya, Uhalifu na Makosa ya Jinai “United Nations on Drugs and Crime”
(UNODC) wamesaidia Mahakama na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) kuandaa kongamano
hilo ili kuwapa weledi wadau mbalimbali wa Haki Jinai dhidi ya
wanawake na watoto wenye jinsia ya kike, ambapo jitihada za pamoja zinahitajika
ili kukabiliana na tatizo hilo.
Ameongeza kuwa, katika
utekelezaji wa haki ya jinai kundi hili
ndilo limekuwa likipata matatizo makubwa ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji
kama vile kubakwa na kulawitiwa hivyo kumekuwa na shida katika uendeshaji wa
mashauri ya vitendo hivyo kulingana na sababu mbalimbali kama vile uwoga wa
watu walioathirika kujitokeza kutoa ushahidi,
ikiwemo tatizo la jamii kuona jambo hilo
ni la aibu na kutolitolea taarifa katika
vyombo husika.
“Kuna shida katika
upelelezi wa mashauri hayo namna gani wapelelezi waangalie ni vigezo gani ili
kuweza kuthibitisha kesi, katika kesi za jinai ili mtu atiwe hatiani lazima
shauri lake lithibitishwe bila kuacha kiwango chochote cha mashaka, kukiwa na
mashaka yoyote inawezekana labda hiki kinachosemwa si kweli inabidi mtuhumiwa
aachiwe.
“Unapokuja kwenye kesi ya
udhalilishaji kuna hoja nyingi kwenye upelelezi zinaachwa kwa mfano daktari
anaposema huyu mama au mtoto wa kike amebakwa amefikiaje hatima hiyo kuwa
amebakwa na kuwa pengine labda uchunguzi wa vina saba (DNA) iwe ni kigezo cha
watu waliofanya makosa hayo na kujua kwamba huyu mtu ni kweli aliingiliwa
kimwili na hivyo kwa hapa nchini kwetu ni changamoto,” alisema Jaji Mruma.
Aidha, ametoa takwimu kwa
mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Benki ya Dunia ambayo imeonyesha kwamba nchini
Tanzania asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa vitendo
vya ukatili wa kimwili lakini pia asilimia 17 wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji
wa kijinsia na pia alisema wanawake wenye umri kati ya miaka 15-49 ambao ni
asilimia 44 wameathiriwa na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.
Alibainisha kuwa,
asilimia 52 ya wanawake vijijini wanakabiliwa na ugomvi wa kifamilia na mjini
ni asilimia 45 na asilimia 30 ya watoto wa kike wanafanyiwa vitendo hivyo kabla
hawajafikisha miaka 18.
Kwa upande wake Dkt. Linda Naidoo kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa
inayopambana na madawa ya kulevya, uhalifu na makosa ya jinai “United Nations
on Drugs and Crime” (UNODC), amesema vipimo vya uchunguzi wa vina saba (DNA)
vinaweza kutumika kubaini mtu aliyetenda kosa la ubakaji hivyo ni vyema kutumia
njia hiyo ili kurahisisha uendeshaji wa mashauri hayo.
Naye Naibu Mkuu wa Chuo
Mipango Fedha na Utawala kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) - Lushoto
Prof. Fatihiya Massawe amesema wako kwenye kongamano hilo kwa ajili ya
kuwajengea uwezo watumishi wa Mahakama ya Tanzania ili kupata ujuzi wa
kushughulikia suala hilo na kuziba pengo lililopo kwa kufanya utafiti na
kuandaa mafunzo mahususi.
Kwa upande wake Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Zainab Mango amesema kuwa, Mahakama
inategemea utendaji kazi wa wadau wengine hasa wanaopeleleza makosa na wanaokuja kuthibitisha kwa kutoa ushahidi mahakamani,
hivyo kama mashauri hayatapelelezwa vizuri wasitegemee muujiza kutoka
mahakamani kwa sababu Mahakama inaangalia ushahidi na haiwezi kuibua ushahidi
kutoka sehemu nyingine ambazo siyo maalumu kwa ajili ya kutoa ushahidi, kama
upelelezi ni mzuri Mahakama haiwezi kumwachia mtu ambaye amepatikana na hatia
ya kutenda kosa hilo na itatoa hukumu kwa haki.
Naye
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Susan Kihawa amesema
kongamano hilo ni maalum kwaajili ya kuangalia namna nzuri ya kushughulika na Mashauri
ya ukatili wa kijinsia kwa sababu licha ya kuwepo kwa juhudi mbalimbali bado
suala hilo limezidi kuongezeka na kuwa changamoto ya dunia nzima hivyo
wameungana na wadau kutoka nje ya nchi ili kushirikiana kutatua tatizo hilo
nchini na dunia nzima.
Dkt.
Linda Naidoo kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na Madawa ya Kulevya,
Uhalifu na Makosa ya Jinai “United Nations on Drugs and Crime” (UNODC), akizungumza
jambo kwenye kongamano hilo.
Hakimu
Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Susan Kihawa akizungumza jambo wakati
wa kongamano hilo.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Amir Mruma (walioketi watatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya Pamoja na wadau wa kongamano hilo.
Baadhi
ya wadau wa kongamano hilo wakijadiliana jambo.
(Picha na Castilia Mwanossa)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni