Na Paul Mushi – Mahakama, Moshi
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 20 Septemba, 2022 amemkabidhi Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdnadri Kiwonde nyenzo za kufanyia
kazi mara baada ya kumteua kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo
jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo ambalo
lilishuhudiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani
lilifanyika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa kuwa Jaji Mkuu yuko mkoani
Kilimanjaro katika kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani kinachofanyika
katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo Moshi.
Akitoa nasaha na
maelekezo baada ya tukio hilo, Mhe. Prof. Juma alisema kukabidhiwa kwa nyenzo
hizo ambazo zinaonyesha mamlaka na majukumu ya kazi za Mfawidhi huyo ni matakwa
ya kisheria ili kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu katika Mahakama
yake na Mkoa kwa ujumla.
“Nataka usimamizi wa hali
ya juu katika mifumo yetu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yaani
JSDS II, E-filling, E-office kwenye kipindi hiki ambacho Mahakama ya Tanzania
inatoka katika matumizi ya karatasi kuelekea Mahakama mtandao. Hakikisha
unakagua na kusimamia suala hili ipasavyo,” Jaji Mkuu aliagiza.
Aidha, Mhe. Prof. Juma
alimtaka Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo kusimamia kikamilifu maadili kwa watumishi wenzake kwa
kuwa zoezi la utoaji haki linapaswa kufanywa kwa uadilifu wa hali ya juu. “Nakutakia kila kheri maana nina imani unajua
mifumo yetu yote ya kazi zetu,” alisema.
Naye Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania alimtakia Hakimu Mkazi Mfawidhi huyo utendaji mwema katika majukumu
yake mapya na kumtaka kuheshimu imani aliyopewa kuongoza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu ambayo ni moja ya Mahakama kubwa na yenye mashauri mengi hapa
nchini.
Naibu Msajili huyo aliyekuwa
anahudumu katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam ameteuliwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara baada ya mtangulizi wake, Mhe. Godfrey Isaya
kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Baada ya hafla hiyo fupi, Mhe. Siyani alitembelea maeneo ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali katika Mahakama hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni