Jumanne, 20 Septemba 2022

JAJI MKUU AZINDUA VIKAO VYA MAHAKAMA YA RUFANI MOSHI

Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 19 Septemba, 2022 alizindua vikao vya Mahakama ya Rufani katika Masjala ndogo Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, hatua ambayo imelenga kusogeza huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa ngazi hiyo ya Mahakama ya juu hapa nchini.

Akizungumza katika uzinduzi huo ulioashiria kuanza kwa vikao vya Mahakama hiyo, Mhe. Prof. Juma alibainisha faida lukuki kufuatia kuanzishwa kwa Masjala ya Moshi, ikiwemo kutatua changamoto za Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani ya Arusha, kutatua changamoto za wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro na kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama wa kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro sasa watakuwa na huduma (za kimahakama) kuanzia Mahakama za Mwanzo mpaka Mahakama ya Rufani ndani ya Mkoa na Kanda yao. (Kuanzishwa kwa Masjala hii) kutawapunguzia gharama na umbali wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro,” alisema.

Mhe. Prof. Juma alisema kuwa Masjala hiyo itatatua changamoto ya mlundikano wa mashauri katika Masjala ya Arusha. Alisema moja ya changamoto za Moshi ni uwepo wa mashauri mengi ya madawa ya kulevya ya washtakiwa wanaokamatwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro yanayowahusu raia wa kigeni na Watanzania.

Alibainisha kuwa baada ya mashauri hayo kumalizika katika ngazi ya Mahakama Kuu Moshi huwa yanaingia katika foleni ndefu ya kusubiri kusikilizwa katika Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani Arusha. “Jambo hili lilizua malalamiko mengi na ya mara kwa mara kutoka kwa wahusika (wafungwa). Kuanzishwa kwa vikao Moshi kutafanya mashauri hayo pamoja na mengine yote yasikilizwe kwa haraka,” Mhe. Prof. Juma alisema.

Jaji Mkuu aliongeza, “Kuanza kwa vikao vya Mahakama ya Rufani Moshi kutasaidia sana kutatua changamoto kubwa ya mlundikano wa mashauri yanayosubiri kusikilizwa Arusha. Ni hatua kubwa, idadi ya mashauri yanayosikilizwa Arusha itaongezeka kwa sababu sasa mashauri ya Moshi yatakuwa yanasikiliziwa Moshi.”

Aidha, Mhe. Prof. Juma alieleza kuwa kuanzishwa kwa Masjala hiyo kutawapa fursa wananchi wa Kilimanjaro kupata taarifa muhimu za kimahakama na kisheria kupitia tovuti ya Mahakama, ikiwemo upatikanaji wa uamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kwenye TANZLII.

Kadhalika, Jaji Mkuu alibainisha kuwa uanzishwaji wa Masjala hiyo utapeleka uzoefu wa Mahakama ya Rufani kwa Mawakili na wadau wa sheria katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kusaidia katika uimarishaji wa ujuzi na ukuzaji wa falsafa ya sheria kwa wadau.

Akizungumza katika halfa hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Emmanuel Mrangu alisema kuwa Moshi ilitangazwa kama Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani na Gazeti la Serikali 579 la Mwaka 2020 mnamo tarehe 24 Julai, 2020 na baadae Gazeti la Serikali Na. 520 la Mwaka 2022 la tarehe 12 Agosti, 2022.

Alisema hadi kufikia Septemba, Masjala ndogo ya Moshi ilikuwa na jumla ya mashauri 295 yanayoendelea na kati ya hayo, mashauri saba ndiyo mashauri yenye umri mrefu zaidi unaofikia miaka mitano tangu yaliposajiliwa. Mhe. Mrangu alieleza kuwa kati ya hayo saba, mashauri ya jinai ni sita na shauri moja ni la madai.

“Kwa kipindi cha mwezi Januari mpaka Septemba 2022, Masjala ndogo ya Moshi imesajili jumla ya mashauri 51 na kati ya hayo, mashauri 30 ni ya madai na mashauri 21,” Naibu Msajili huyo alisema.

Kuhusu mashauri ya mlundikano, Mhe. Mrangu alisema kuwa hadi kufikia mwezi Septemba 2022, Masjala ndogo ya Moshi ilikuwa na jumla ya mashauri ya aina hiyo 62 na kati ya hayo, mashauri ya madai yalikuwa 16 na mashauri ya jinai yalikuwa 46.

“Kwa idadi ya mashauri 62 ya mlundikano na kwa wastani wa mashauri 33 ambayo hupangwa kwa kikao kimoja, tutahitaji vikao viwili kumaliza mzigo huo wa mlundikano,” alisema.

Safari ya kusogeza huduma za Mahakama Kuu Moshi ilianzia Mwaka 1921 wakati utawala wa Wakoloni walipotunga Kanuni za Masjala ya Mahakama Kuu— High Court Registries Rules, 1921 [GN No. 27/1920]. Kanuni hizi zilianzisha Masjala ya Mahakama Kuu Dar es Salaam na Masjala za Mahakama Kuu Tanga, Tabora na Mwanza. Masjala ya Tanga ilihudumia Wilaya za Pangani, Usambara, Moshi na Arusha.

Mpaka kufika mwaka 1993, wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro walikuwa wakipata huduma za Mahakama Kuu jijini Arusha. Ilipofika mwaka 1993 ndipo Mahakama Kuu Moshi ilianzishwa ili kuwasogezea huduma wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa upande wa Mahakama ya Rufani tokea ilipoanzishwa mwaka 1979, wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamekuwa wakipata huduma za Mahakama hiyo katika Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani ya Arusha. Katika kalenda ya Mahakama ya Rufani ya 2022 iliyotolewa Septemba 2021, kikao cha kwanza cha Mahakama ya Rufani Moshi kilipangwa kuanza tarehe 19 Septemba  hadi tarehe 7 Oktoba, 2022.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (picha ya juu na chini) akizindua Vikao vya Mahakama ya Rufani katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo Moshi Mkoa wa Kilimanjaro. Uzinduzi huo ulifanyika jana tarehe 19 Septemba, 2022.

Kiongozi wa gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi (katikati aliyesimama kwa ukakamavu) akimkaribisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kufanya ukaguzi kama ishara ya uzinduzi wa Vikao vya Mahakama ya Rufani katika Masjala ndogo ya Mahakama hiyo Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, huku askali wengine wakichukua nafasi zao kabla ya zoezi hilo. 
Askali kutoka Jeshi la Polisi wakiwa tayari kwa ukaguzi wa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) kuashiria uzinduzi wa Vikao vya Mahakama ya Rufani Moshi.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikagua gwaride hilo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea salamu za heshima kutoka kwa kiongozi wa gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Polisi katika uzinduzi huo baada ya kufanya ukaguzi.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni