Jumanne, 20 Septemba 2022

JAJI NDUNGURU AZUNGUMZA NA WATUMISHI WA MAHAKAMA RUKWA; AKEMEA VITENDO VYA RUSHWA

Na Mayanga Someke, Mahakama-Sumbawanga

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru amewataka watumishi  wa Mahakama ya Mkoa Rukwa kutojihusisha na vitendo vya rushwa na badala yake wazingatie maadili ili waweze kufanya kazi bila bughudha.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama hiyo hivi karibuni katika kikao cha pamoja, Mhe. Ndunguru alisema kuwa, tuhuma za rushwa ni muhimu kuzifuta kwa kufuata maadili ya kazi, kupendana pamoja na kushirikiana huku akiwasihi watumishi hao kuepuka na kuacha vitendo vya utovu wa maadili ikiwemo rushwa.

“Rushwa mahakamani inamgusa kila mtumishi wa Mahakama kwa namna moja au nyingine, hivyo naomba suala hili liachwe maana linachafua taswira ya Mahakama, mtumishi yeyote atakaejihusisha na vitendo vya rushwa, Mahakama haitamvumilia,” alisisitiza.

Mbali na hilo, Jaji Ndunguru aliwakumbusha Viongozi wa Mahakama hiyo kuwa na desturi ya kufikisha taarifa muhimu kwa watumishi wa chini yao mara tu wanapozipata ili taarifa mbalimbali ziweze kufahamika katika ngazi zote za Mahakama.

“Nataka taarifa ziweze kumfikia kila mmoja wetu katika ngazi ya Mahakama ili ajue kinachoendelea kwenye Mhimili wa Mahakama, ikiwemo Mpango Mkakati wa Mahakama” alisema.

Kadhalika; Jaji Mfawidhi aligusia suala la watumishi kutambua na kuheshimu mipaka kwa kila ngazi ya Mahakama ili kuepuka migongano isiyo ya lazima.

Mhe. Ndunguru aliongeza kwa kuwasihi watumishi kujitokeza kwa wingi kwenye programu ya mazoezi ambayo hufanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa ya kila wiki katika viwanja vya mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga ili kuimarisha afya zao.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya Mkoa wa Rukwa (hawapo katika picha) katika kikao cha pamoja kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Maira Kasonde na kushoto ni Mtendaji wa Kanda hiyo, Bw. Emmanuel Munda.

Watumishi wa Mahakama ya Mkoa Rukwa wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao katika kikao kati yake na Watumishi hao.

Watumishi wa Mahakama ya Mkoa Rukwa wakimsikiliza kwa makini Jaji Mfawidhi, Mhe. Dunstan Ndunguru alipokuwa akizungumza nao.

Watumishi wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Mhe. Dunstan Ndunguru.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni