·Wadau wafunguka,
hawaamini yanayotokea
Na. Mujaya Mujaya – IJC
Temeke
Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kilichopo
jijini Dar es Salaam hivi karibuni kilisherekea mwaka mmoja tangu kianze kutoa
huduma za utoaji haki kwa wananchi kwenye mashauri mbalimbali ya kifamilia
yanayohusu watoto, ndoa, talaka na mirathi kwa kuadhimisha wiki ya huduma kwa
mteja.
Maazimisho ya wiki hiyo yalianza tarehe 25 Oktoba 2022
ambayo ni mwaka mmoja kamili tangu Kituo hicho kilipoanza kutoa huduma zake
rasmi tarehe 25 Oktoba 2021 na kukamilika tarehe 28 Octoba, 2022, huku wananchi
wakipongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri, huduma bora na ushirikishwaji wa
wadau wa haki madai ya mirathi na ndoa.
Katika maadhimisho hayo, wananchi waliofika mahakamani
walipata fursa ya kupata huduma maalumu zilizolenga kuharakisha upatikanaji
haki kwa wakati ambapo viongozi wa ngazi za juu walihusika moja kwa moja katika
wiki nzima kuhudumia wateja kwenye dawati la mapokezi, kujibu simu za nje
kutoka kwa wateja wanaofuatilia mashauri yao na kutoa elimu kuhusu huduma
zinazotolewa.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, Kituo Jumuishi Temeke kimehudumia
watu 135,437, ambapo kati yao 71,915 ni wanawake, sawa na asilimia 53.1 na 63,522
ni wanaume ambao ni sawa na asilimia 46.9 ya watu wote walio hudumiwa.
Akizungumza kuhusu tukio hilo kwa niaba ya Jaji
Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe. Ilvin Mugeta, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Mhe. Modesta Opiyo, alisema, "Kila mahali huwa naitabulisha Mahakama hii kama
Mahakama ya wananchi. Asili ya watu tunaowahudumia wengi wanakuwa wameshaumia
kwa namna moja ama nyingine, kwa hiyo huduma zetu huanza kurudisha faraja kwao.
Utaona watu wameathirika kisaikolojia, tunajitahidi kuwarudishia tabasamu.”
Mhe. Opiyo aliendelea kufafanua, “Tungekuwa na urasimu
kwa wananchi hawa, machungu yangeongezeka mara mbili, lakini mtu akija na
kupata faraja anapata unafuu. Kwa mfano, katika Mahakama ya Mwanzo kwenye kituo
hiki mtu ana andikisha shauri na kuonana na Hakimu siku hiyo hiyo, hii ndiyo
dhana halisi ya haki sawa kwa wakati.”
Alisema kuwa Kituo hicho kitaendelea kuboresha huduma
ili kutatua changamoto ambazo zitabainika. Kwa mujibu wa Jaji Opiyo, wametumia
wiki hiyo ya huduma kwa mteja kujitafakari kila mmoja wao ili kuona wapi wanatakiwa
kuboresha kwenye utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Temeke,
Mhe. Martha Mpaze alizungumzia mashauri
yaliyosajiliwa na kuamuliwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja na kueleza
kuwa jumla ya mashauri 7,825 yanayohusu mirathi na ndoa yalifunguliwa katika
ngazi zote za Mahakama, yani Mahakama Kuu, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya
Mwanzo.
Alibainisha kuwa hadi kufikia tarehe 25 Oktoba 2022,
jumla ya mashauri 6,140 sawa na aslimia 78% ya mashauri yote yamemalizika na
mashauri 1,685 bado yanaendelea kusikilizwa.
Naye Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Mary Shirima aliwapongeza
watumishi wote kwa kufanya kazi wa kujituma na kutoa huduma bora zinazomlenga
mwananchi, hatua iliyochagiza mafanikio hayo.
"Kwa takwimu tulizokusanya kutoka kwa wateja 4,414
kuhusu huduma zetu, 4,397 ambao ni sawa na asilimia 99.62% walisema huduma ni
nzuri huku 17 pekee, sawa na asilimia 0.38% wakionesha kutokuridhiswa na huduma
zetu. Bado tunafanya mawasiliano na wateja hao ili kupata maoni yao, tujue
maeneo ya kuboresha," alisema.
Mama mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe alitoa
ushuhuda wa namna alivyohudumiwa baada ya kuwasilisha shauri lake katika Kituo
linalohusu masuala ya ndoa ambapo alionyesha kuridhika na huduma alizopata.
"Nilileta maombi ya talaka, jamaa akaitwa akaja,
tukapangiwa tarehe na kusikilizwa, leo alikuwa anajitetea, kesho tunaenda
kumaliza utetezi kisha hukumu. Yani ndani ya miezi miwili jambo linaisha. Sikutarajia
kupata huduma nzuri mahakamani kama ninavyoona hapa Temeke, hadi najiuliza hivi
Mahakama zote zipo hivyo?” alisema mteja huyo.
Naye Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania
(BAKWATA) Wilaya ya Temeke, Ustadhi Mudhihir Mchoye amepongeza kuanzishwa kwa Kituo
hicho kwani wamepata fursa ya kushirikiana na taasisi nyingine kama ustawi wa
jamii, watu wa msaada wa kisheria au dawati la jinsia ili kuwahudumia wananchi
kwa ukamilifu.
"Tunashukuru kwa uwepo wa taasisi mbalimbali
zinazosaidia watu kisheria bila gharama yoyote au kwa gharama nafuu. Uwepo wetu
umesaidia kuongeza uelewa katika mashauri yoyote ambayo yanahitaji ufafanuzi wa
sheria ya dini ya kiislamu,"alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa
Sheria kwa Wanawake (WLAC), Wakili Theodosia Nshala alieleza namna
anavyoshangazwa na kasi iliyopo katika Kituo hicho katika kushughulikia
mashauri yanayowasilishwa na wananchi.
“Mashauri huchukua muda mfupi hasa yale ambayo hayana
changamoto za kisheria kwani mteja anaweza kupata msaada au huduma anayohitaji
hapo hapo mahakamani bila kusafiri umbali mrefu. Pia mahusiano baina ya wadau
wa haki mirathi na ndoa yameimarika kutokana na kufanya kazi kwa pamoja. Hatua
hii inaharakisha upatikanaji wa haki na kumpunguzia gharama mwananchi,” alisema.
Kituo cha Masuala ya Familia Temeke kilianzishwa kupitia
Gazeti la Serikali Na. 640 la mwaka 2021 kikijumuisha ngazi tatu za Mahakama ambazo
ni Mahakama Kuu, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Mwanzo. Mahakama hizi zimepewa
mamlaka kupitia Gazeti la Serikali Na. 641 na 639 kusikiliza mashauri ya ndoa
na mirathi katika mkoa wa Dar es salaam.
Matangazo ya kuanzishwa Mahakama hiyo yalichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 27 Agosti 2021. Ngazi tatu za Mahakama tajwa na ofisi za wadau hutoa huduma ndani ya jengo moja, hivyo kuunda dhana ya Kituo Jumuishi cha Mahakama.
Watumishi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Kifamilia
Temeke wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kuhitimisha wiki ya kusherekea
mwaka mmoja tangu kuianzishwa kwa Kituo hicho.
(Picha na Mujaya Mujaya – IJC Temeke)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni