·Jaji Mfawidhi Kanda ya Musoma afunika kwenye soka
Na
Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza
Mahakama ya Tanzania katika Kanda ya Ziwa tarehe 29
Octoba, 2022 iliendesha bonanza maalumu la michezo lililowashirikisha watumishi
wa kada mbalimbali wakiwemo Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu na Watendaji kutoka
katika Mikoa ya Mwanza, Mara na Shinyanga.
Akifungua bonanza hilo lililofanyika katika Uwanja wa Nyamagana,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. John Kahyoza aliwapongeza
watendaji wote kutoka Mahakama zilizoshiriki kwa kutoa ushirikiano kufanikisha
jambo hilo.
“Kwanza niwapongeze watumishi wote mliosafiri na kuja Mwanza
kwa ajili ya bonanza hili. Bonanza hili lina baraka zote za viongozi wa Mahakama,
kwani ni sehemu ya mazoezi ambayo ni afya. Nawapongezeni wote kwa kuifanya siku
hii ya pekee kuwa ni yenye furaha kwa kila moja wetu aliyehudhuria na kushiriki,”
alisema.
Mhe. Kahyoza alielezea masikitiko yake kufuatia
watumishi wa Mahakama kutoka Kanda ya Bukoba kushindwa kuhudhuria bonanza hilo baada
ya kuchelewa kupata taarifa. “Niwasilishe salama za masikitiko kutoka kwa
wenzetu wa Kanda ya Bukoba ambao walipenda kuwepo katika bonanza hili lakini
walishindwa kufanya maandalizi kwa ajili ya safari ya kuja Mwanza kwa vile hawakupata
taarifa kwa wakati,” alisema.
Jaji Mfawidhi huyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba waratibu
wa bonanza hilo kuandaa ratiba mapema na kuiwasilish kwa wenzao wa Bukoba ili
waweze kujiandaa kwa ajili ya kushiriki.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Tutubi
Maganzini aliwashukuru viongozi wenzake kwa kuwawezesha watumishi kusafiri na
kupangilia kila jambo kwa jinsi inavyotakiwa.
“Nawapongeza watendaji wenzangu kwa kuweza kufanikisha
hili japo pamoja na maandalizi kuwa ya muda mfupi. Pamoja na faida za kiafya
kwa watumishi pia bonanza hili linawezesha kufahamiana baina yetu, kwani hata
mtumishi akihamishiwa Kanda nyingine kati ya hizi tatu tulizokutana hatakuwa mgeni,”
alisema.
Bonanza hilo lilihusisha michezo ya riadha, mpira wa
pete, kukimbiza kuku, kuvuta kamba, mpira wa miguu, mbio za magunia na mchezo
maalumu wa aina yake wa kunywa soda.
Katika mchezo wa riadha uliowashirikisha Majaji, Naibu
Wasajili na Watendaji, mshindi wa kwanza alikuwa Mtendaji Kanda ya Mwanza, Tutubi
Mangazini ambaye alifuatiwa na Mtendaji Kanda ya Musoma, Festo Chonya na
mshindi wa tatu alikuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya, huku mshindi wa nne akiwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
kutoka Kanda hiyo hiyo, Mhe. Frank Mahimbali.
Kwenye mpira wa pete, timu ya Mahakama Kanda ya Mwanza
iliigaragaza Kanda ya Musoma kwa vikapu 36-7. Katika shindano la kukimbiza kuku,
Mhe. Mahimbali aliibuka mshindi kwa upande wa wananume, huku Editha Haule
kutoka Kanda ya Shinyanga akichukua ushindi kwa upande wa wanawake. Mchezo huo
pia uliwashirikisha watumishi wenye umri wa kuanzia miaka 50 ambapo ushindi ulienda
kwa Michael Maduhu kutoka Kanda ya Shinyanga.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa upande wa wanaume, timu
kutoka Kanda ya Musoma iliwaburuza Mwanza na kwa upande wa wanawake timu ya Kanda
ya Mwanza ikawakamua Kanda ya Musoma.
Mahakama Kanda ya Musoma iliwachapa Mwanza magoli 2-1 katika
mchezo wa mpira wa miguu, huku goli la ushindi likifungwa kiufundi na Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya. Katika
mchezo huo, timu ya mpira wa miguu Kanda ya Shinyanga ilizifunga timu kutoka Kanza
za Musoma na Mwanza kwa goli 1-0 kila mmoja.
Kwenye shindano la kunywa soda pamoja na mkate kwa
upande wa wanaume, mshindi alikuwa Leopord Ngowi kutoka Kanda ya Shinyanga na
kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa Amina Mlasi kutoka Kanda ya Musoma.
Kwa upande wa mbio za magunia wanaume, Donald Sondo kutoka Kanda ya Musoma aliibuka kinara na kwa
upande wa wanawake mshindi alikuwa ni Rose
Daudi kutoka Kanda ya Shinyanga.
Baada ya michezo hiyo iliyonza saa tatu asubuhi hadi
saa kumi na moja jioni, watumishi wote wenyeji na wageni ambao walikuwa na
nafasi walijumuika pamoja katika “Get Together Party’’ iliyofanyika katika Hotel
ya Taiwan kwa lengo la kupongezena na kuondoa uchovu.
Timu ya Mpira wa Pete kutoka Kanda ya Mwanza kabla ya mpambano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni