Na Innocent Kansha - Mahakama
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es salaam, Mhe. Amir Mruma
amesema Mahakama ya Tanzania itahakikisha huduma zake zinamfuata mwanachi alipo
na si mwanachi afuate huduma hizo umbali mrefu, kwani kwa kufanya hivyo muda wa
uzalishaji mali utapungua na malengo ya taasisi ya kufikia mapinduzi ya nne
viwanda yataathirika.
Akifungua
rasmi jengo la Mahakama ya Mwanzo Chanika lililojengwa Kata ya Zingiziwa Wilaya
ya Ilala jana tarehe 01 Novemba, 2022, Jaji Mfawidhi huyo alisema Mahakama itaendelea
kushirikiana na Serikali na wadau wengine wote ili kufikia malengo yake ya
kikatiba ya utoaji haki. Amesema jitihada zilizofanyika kupatikana kwa huduma za
kimahakama Chanika hazitaishia hapo bali zitakuwa hata katika maeneo mengine.
“Mfano
Mahakama ya Mwanzo Ukonga iko katika jengo lisilokuwa la Mahakama na haina eneo
hapo. Niwaombe viongozi wenzangu mtupatie ushirikiano wa kupata eneo. Mahakama
ya Mwanzo Ukonga ni ya kwanza kwa wingi wa mashauri katika Wilaya yetu na inaweza
kuwa kati ya Mahakama za Mwanzo tatu zinazopokea mashauri mengi zaidi nchini.
Mahakama hii ina wastani wa Mashauri 4,153
kwa Mwaka”, alisema Jaji Mruma.
Jaji
Mfawidhi huyo aliongeza kuwa, Mahakama inatambua juhudi zinazofanywa na viongozi
wa Serikali na Mahakama kwa kushirikiana pamoja kusaidia upatikanaji wa maeneo
yatakayowezesha ujenzi wa majengo mazuri ya Mahakama za Mwanzo Buguruni na Ukonga.
Alisema Mahakama inatambua kuwa juhudi hizo bado hazijazaa matunda, hivyo akawaomba
viongozi kujitahidi kufanikisha upatikanaji wa maeneo hayo.
“Ninaamini
kwa juhudi za Jaji Mkuu wa Tanzania, ikiwa tutapata maeneo hayo tunaweza kupewa
kipaumbele cha kujengewa majengo hayo kupitia Mpango Mkakati wa Mahakama wa uboreshoji
wa Mahakama unaoendelea nchi nzima na kuifanya Mahakama ya Tanzania kwenda na
kasi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa na Serikali
mtandao”, alisema.
Jaji
Mfawidhi alisema ni faraja kwa Mahakama kuona kuwa, mwananchi atapata huduma za
kimahakama katika Mahakama hiyo ya Mwanzo Chanika ambapo uwepo kwa Mahakama
hiyo utasaidia kuepusha gharama na usumbufu kwa wananchi kufuata huduma hizo
kwa umbali mrefu. Amesema ni dhahiri kuwa wananchi wa Kata takribani sita ambazo
zinazozunguka eneo hilo, wataitumia Mahakama hiyo na uwepo wake utawasidia
wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, hivyo akawashauli waendelee kuilinda
na kuitunza ili iendelee kuwahudumia.
Mhe.
Mruma akawakumbusha wadau kuwa, Mahakama imepeleka sehemu ya nguvu kazi
iliyokuwepo katika Mahakama za Dar es Salaam kufanya kazi katika Mahakama hiyo,
akawaomba kuwapa ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na
uaminifu mkubwa.
“Msiwashawishi
kuingia katika vitendo vilivyo kinyume na maadili yao ya kazi. Na kwa watumishi
mliopangwa katika Mahakama hii, mnao wajibu mkubwa wa kulinda heshima ya Mahakama
ya Tanzania na kuwahudumia wananchi hawa kwa unyenyekevu na weledi mkubwa ili
wananchi waliosubiri huduma hii kwa muda mrefu, waifurahie”, alisisitiza Jaji
Mfawidhi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtendaji wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam (Kisutu), Bi. Athanasia Kabuyanja alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Chanika, ulianza
tarehe 18
Aprili, 2021 na kukamilika tarehe 01
Julai, 2022 ambapo mradi ulikabidhiwa ujenzi
huo umetekelezwa na Mkandarasi Becyma Quality Construction LTD na Msimamizi Mkuu wa mradi alikuwa ni Wakala wa MajengoTanzania (TBA).
Mtendaji Kabuyanja akaeleza kuwa, gharama ya utekelezaji wa mradi huo ni shilingi 438,938,294.42
ambazo
tayari zimekwishalipwa kwa Mkandarasi. Gharama
nyingine ni shilingi 8,513,000.00 zilizotumika
kuchimba kisima kirefu cha maji na shilingi
6,252,000.00 zilizotumika kujenga mnara wa kuwekea matanki ya maji
pamoja na kununua matanki. Hivyo thamani halisi ya utekelezaji wa mradi ni sawa
na shilingi 453,703,294.42
Mtendaji
huyo alisema jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo Chanika lina ukubwa wa mita za
mraba 364, likiwa na kumbi mbili (2) za Mahakama, ofisi mbili (2) za Hakimu,
Ofisi sita (6) za watumishi wengine na vyumba viwili (2) vya kuhifadhia nyaraka
na vielelezo. Vingine ni jiko na vyumba kwa ajili ya mahabusu ya wanaume na
wanawake. Ujenzi wa jengo hilo pia ulijumuisha kazi za ujenzi wa choo cha umma
cha nje, kuchimba kisima cha maji na ujenzi wa mnara wa kuwekea matanki ya maji.
Naye, Diwani wa kata ya Zingiziwa, Mhe. Maige Selemani Maganga
akitoa salama kwa niaba ya wananchi alisema, niwakumbushe wakuu wangu na
wajumbe kupeleka taarifa kwa wananchi kwamba Kata ya Zingiziwa imepata Mahakama
na kazi yake kubwa ni kutenda haki bila kujali hali ya mtu, lakini mjue kuwa Mahakama
ni chombo huru kinachofanya shughuli zake bila kuingiliwi katika maamuzi, jambo
hilo ni muhimu sana wananchi wa eneo hili wakafahamishwa na kulielewa kwa
ufasaha.
“Kwa maana kuna muda maamuzi yatatoka Mahakamani kuja kwa Diwani wakati sio sehemu sahihi ya kuyashughulikia, kwani hata Diwani mwenyewe anaogopa na kuheshimu maandishi mekundu, Mahakama inataratibu zake za kushughulikia mambo yote yaliyoamriwa kisheria”, alisema Mhe. Diwani huyo.
Mhe. Maganga akawaasa wananchi kuwa, Kutokana na changamoto ya panya rodi na mambo mengine ya kiuhalifu na uvunjifu wa amani unaolikumba eneo hilo ni wajibu wa viongozi kwenda kuwaambia vijana kuachana tabia zenye viashiria vya kiuhalifu, na pengine kutojihusisha na vitendo hivyo na kuacha kukaa sehemu zisizokuwa na usalama kwani sasa chombo cha haki kipo na kinatenda kazi.
PICHA NA : Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni