Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Mcheza wa Timu ya Mahakama
ya Tanzania (Mahakama Sports) Juster Tibendelana juzi alipokelewa kishujaa
alipowasili katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro anapofanyika kazi
baada ya kushiriki katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na
Idara za Serikali (SHIMIWI) yaliyofanyika huko jijini Tanga hivi karibuni na
kuibuka mshindi wa kwanza kwenye riadha wanawake mita 3,000.
Justa hakuamini macho
yake alipowasili katika Kituo hicho baada ya kulakiwa na umati mkubwa wa
wafanyakazi wenzake wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe na viongozi wengine waandamizi na kupewa
heshima zote za kishujaa, ikiwemo kukabidhiwa keki maalumu iliyokuwa
imeandaliwa kwa ajili ya kumpongeza kwa ushindi huo mkubwa alioupata.
Binti huyo mdogo mwenye
sifa ya MMM, yaani, Mpole, Mcheshi na Mwelevu ambaye ni Mwembamba wa wastani,
Mrefu wa wastani na Mweusi wa wastani, mwenye umbo fulani hivi na macho ya kuvutia, alibaki
akiwapungia mikono watumishi wenzake huku akimwaga tabasamu murua la karne ya
21, hatua iliyoibua furaha kila kona katika viunga vya Kituo hicho.
Akizungumza wakati wa
hafla hiyo, Mhe. Ngwembe ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa ni jambo la
kujivunia kwa mtumishi huyo mwaminifu kupata ushindi huo na kusisitiza kuwa
ushindi huo haukuwa wa Justa pekee bali ni wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
“Tunafurahia sana jinsi
alivyotuwakilisha mtumishi mwenzetu Justa kwa kuwa mshindi wa kwanza katika
mbio za mita 3,000 upande wa wanawake, hii pia imewezekana kutokana na juhudi alizozionyesha
pamoja na ushirikiano mkubwa toka kwa watumishi wenzake, hongera sana,” Jaji Mfawidhi
huyo alisema.
Mhe. Ngwembe alimvisha Justa
medali ya dhahabu aliyoipata katika mashindano hayo ya SHIMIWI yaliyoanza tarehe
1 Octoba 2022 na kuhitimishwa tarehe 15 Octoba 2022. Katika mashindano hayo, Mahakama
Sports iliwatimulia vumbi washiriki wengine kutoka taasisi mbalimbali kwa kuzoa
makombe saba, ambayo kati ya hayo ilikabidhiwa manne.
Naye Mtendaji wa Mahakama
wa Kanda, Ahamed Ng’eni alimpongeza shujaa huyo kwa mshindi mnono na kuwataka
watumishi wengine kujituma kufanya mazoezi na kujiandaa vyema ili wakati ujao,
Mahakama iweze kutoa washindi wengi zaidi.
Akipokea pongezi hizo, Justa
alionekana kuhemewa na furaha na kusema kuwa anashukuru kwa ushirikiano mkubwa
alioupata kwa viongozi wa Mahakama na watumishi wenzake ambao ulichagiza ushindi
wake. Vilevile alifikisha salamu za ushindi wake zilizotolewa na Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
Mapokezi hayo pia
yaliambatana na kumkaribisha Jaji mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Gabriel Malata ambaye amewasili katika Kituo hicho hivi karibuni kwa ajili ya
kuwahudumia wananchi katika Kanda hiyo ya Morogoro. Mhe. Malata aliahidi
kutekeleza majukumu yake ipasavyo huku akiomba ushirikiano wa dhati toka wa
watumishi na wadau wa Mahakama.
Justa Tibendelana (aliyeshika keki katikati) akifurahia zawadi hiyo katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro. Kulia kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Maua Hamduni.
Hongera sana kwa ushindi.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni