Jumanne, 22 Novemba 2022

JAJI KIONGOZI ATAJA USULUHISHI KUWA NJIA SAHIHI YA UTATUZI WA MIGOGORO

 ·       Awataka Mawakili kutumia mifumo iliyopo kisheria kuwasilisha malalamiko yao

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Shinyanga

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amesema usuluhishi ni njia sahihi ya kutatua migogoro kwa kuwa inajenga na kukuza undugu na pia ni takwa la Katiba ya nchi.

Akizungumza na wadau wa utoaji haki katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Shinyanga, Jaji Siyani alisema njia hiyo ya utatuzi wa migogoro ina tija katika jamii kwa kuwa huwaacha watu wakiwa wamepatana badala ya kutekeleza amri zinazotolewa na Mahakama.

“Wakati mwingine ni bora hata pale unapofanyika vibaya lakini watu wamepatana ni bora zaidi kuliko amri zinazotolewa na Mahakama”, alisema Jaji Kiongozi.

Akitolea mfano wa nchi zilizoendelea, Jaji Siyani alisema kuwa katika nchi hizo, usuluhishi unamaliza kwa zaidi ya asilimia 90 migogoro inayofikishwa mahakamani. Aliongeza kuwa hali hiyo ni tofauti kwa nchi yetu licha ya kuwa zipo  njia mbalimbali za usuluhishi hata kabla nchi haijapata uhuru.

 Alisema ushahidi wa kwa nini Tanzania haitumii njia ya usuluhishi ni uwepo wa mashauri machache yaliyosikilizwa kwa njia hiyo. Alisema kati ya mwaka 2020 hadi 2021 Masjala za Mahakama Kuu ya Tanzania ziliamua mashauri 2,398 yenye asili ya madai na kati ya mashauri hayo, mashauri 182 tu ambayo ni sawa na asilimia nane ndiyo yaliyoamuliwa kwa njia ya usuluhishi.

Akizungumzia Mawakili, Jaji Kiongozi alisema wote wanao wajibu wa kuwaandaa wadaawa kushiriki kwenye hatua zote za usuluhishi na kuwa tayari kufikia uamuzi unaotokana na mapatano kwani kwa kufanya hivyo kutarahisisha kazi ya utoaji haki, kupunguza gharama na kuokoa muda.

 “Usuluhishi utafanikiwa tu endapo kuna dhamira ya kusuluhisha na kufikia muafaka, lakini ikichukuliwa kuwa ni hatua ya lazima kisheria hautaweza kufanikiwa na italeta dhana kuwa hatua za usuluhishi zinapoteza muda”, alisema Mhe. Siyani.

Aidha, Jaji Kiongozi amevitaka vyombo vya habari nchini kutenga nafasi ya kuelimisha Umma umuhimu wa usuluhishi ili wananchi waelewe faida zake na kuitumia njia hiyo. Alisema kutumika kwa njia hiyo si tu kuwa itaongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri bali pia mshikamano na undugu wa jamii utaimarika zaidi.

Ametoa wito kwa Maafisa wa Mahakama hususani Mawakili kushiriki katika maboresho ya Mahakama kwa kutumia mifumo na vyombo vilivyopo kisheria badala ya kulalamika na kukosoa kupitia mitandao ya kijamii huduma zinazotolewa na Mahakama pamoja na watumishi wake.

“Katika zama tulizonazo, Wakili hatarajiwi tu kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi wake bali pia anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maboresho ya mifumo mbalimbali kivitendo ili kufikia lengo la Mahakama la kutoa haki kwa wakati”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema Mawakili wanapaswa kufahamu kuwa kama suala linahusu maadili ya Jaji au Hakimu kuna kamati zilizoundwa kisheria zikiwemo Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama na nyinginezo hivyo wawasilishe malalamiko yao kwenye kamati hizo. 

“Kumekuwepo na ongezeko la Maafisa wa Mahakama kuwa wakosoaji wa huduma za Mahakama na watumishi kupitia mitandao ya kijamii pekee hivyo matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wananchi na Maafisa wa Mahakama wanashiriki katika juhudi za kuboresha huduma kupitia mifumo na vyombo vilivyopo kisheria na si kulalamika kupitia mitandao, kuijadili na kuishia huko”, alisema.

 Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara ya siku nne katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu yenye leo la kutangaza shughuli za Tume hiyo na pia kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja na wadau wa utoaji haki.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani akizungumza kuhusu matarajio ya Tume na Mahakama kwa wadau wakati wa Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji Haki jana mkoani Shinyanga.  
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Shinyanga wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati akifungua Mkutano wao na Tume.  
Viongozi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Tume na Wadau wa Utoaji Haki jana mkoani Shinyanga. Kushoto ni Naibu Katibu wa Tume (Ajira, Uteuzi na Upandishaji Vyeo) Bibi Enziel Mtei, katikati ni Naibu Katibu wa Tume (Nidhamu na Maadili) Bibi Alesia Mbuya na Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Mahakama ya Tanzania Bibi Beatrice Patrick.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwatt akijibu hoja katika Mkutano Tume na Wadau wa Utoaji Haki jana mkoani Shinyanga.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni