Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama ya Tanzania imefanya uboreshaji wa huduma
zake katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na
wananchi.
Akizungumza
na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo wakati wa ziara
ya Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani humo, Jaji Mkuu alisema maboresho ya huduma
za Mahakama yaliyofanywa na Mhimili huo ni mengi na siyo ujenzi wa majengo ya
Mahakama peke yake.
Jaji
Mkuu alitaja aina ya uboreshaji wa huduma za Mahakama uliofanyika kuwa ni pamoja
na mapinduzi makubwa ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
katika shughuli za Mahakama Pamoja na utoaji wa huduma za kimahakama kwa uwazi
na kwa ufanisi.
Alisema
uboreshaji mwingine wa huduma za Mahakama uliofanyika licha ya ujenzi wa
majengo ya Mahakama ni mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa
maadili kwa watumishi wa Mahakama.
“Hili
ni eneo ambalo tunajipima na kujitathmini sana, malalamiko katika eneo hili
yamepungua kwa kiasi kikubwa”, alisema Jaji Mkuu.
Aidha,
Jaji Mkuu amewataka watumishi wa Mahakama kuyafanya maboresho na mafanikio
yaliyopatikana kuwa endelevu kwa kusoma na kujifunza yale yanayoendelea ili
kukabiliana na changamoto kubwa ya nchi zinazoendelea ya kuanzisha mambo mazuri
lakini hayawi endelevu.
Kuhusu
matumizi ya Tehama ndani ya Mhimili wa Mahakama, Jaji Mkuu amewataka watumishi
kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya kidigitali katika utoaji wa huduma.
Alisema Mahakama ya Tanzania inaandaa mtaala mpya wa mafunzo ambapo watumishi
wake wote watapata mafunzo ya namna ya kutoa huduma kidigitali.
Naye
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka watumishi wa
Mahakama kutojivuta katika kuingia kwenye matumizi ya Tehama kwa kuwa tayari uwekezaji
mkubwa umefanywa na Mahakama ya Tanzania.
Kwa
upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akifafanua kuhusu
upungufu wa watumishi wa Mahakama alisema matumizi ya TEHAMA yatasaidia kwa
kiasi kikubwa kutatua tatizo la upungufu wa watumishi.
Aidha,
alitoa wito kwa kila Kanda ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuona namna ya kuangalia
ni maeneo yapi yatahitaji kutumia Tehama ili kurahisisha kazi za utoaji haki na
pia kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi.
Wajumbe
wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wako kwenye ziara ya siku nne katika mikoa ya
Shinyanga na Simiyu yenye leo la kutangaza shughuli za Tume hiyo na pia kukutana
na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja
na wadau wa utaoji haki.
Watumishi Mahakama kuu kanda ya Shinyanga wakimsikiliza Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipokuwa akizungumza nao leo mkoani humo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni