Ijumaa, 25 Novemba 2022

JAJI KIONGOZI AWATAKA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI KUHAKIKI TAARIFA ZA MAHAKAMA

 ·       Azitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama kuwasiliana

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Simiyu

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kauu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kuhariri na kuhakiki taarifa zinazohusu Mhimili wa Mahakama kabla hazijawafikia wananchi ili kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama.

Akizungumza na wadau wa utoaji haki jana mkoani Simiyu, Jaji Kionggozi amesema wahariri wana nafasi kubwa ya kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama lakini pia wanayo nafasi kubwa ya kuvunja au kubomoa imani hiyo kwa chombo chao.

“Matarajio ya Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mahakama ya Tanzania ni kuona wahariri wanatambua kuwa wao ni wadau muhimu hivyo watambue wajibu wao wa kuhakikisha habari zinazotolewa kuhusu Mahakama zinahaririwa na kuhakikiwa vizuri na habari hizo ni za kweli na siyo za upande moja”, alisema.  

Alisema hakuna mtu au chombo chochote kile kinachoweza kuaminika kutoa haki kama pande mbili za mgogoro hazina imani na mtu au chombo hicho”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema habari zikiandikwa kishabiki au zikatengenezewa vichwa vya habari vyenye kusudio la kuvuta watu wazisome au kuzisikiliza kwa makusudio yoyote yale zinaweza kuupotosha Umma na kuondoa imani iliyonayo kwa Mahakama.

“Endapo wananchi watakosa Imani na Mahakama hawataitumia kutafuta haki, na Imani kwa Mahakama ndiyo msingi wa haki hivyo uwezekano wa wananchi kujichukulia sheria mkononi utakuwa ni mkubwa”, alisisitiza.

Jaji Kiongozi alisema kila Mdau wa Mahakama anao wajibu wa kuhakikisha vyombo vya Serikali ikiwemo Mahakama vinafanya kazi iliyokusudiwa. Aliongeza kuwa Tume na Mahakama pia inatarajia kuwa wahariri watashiriki katika maboresho yanayoendelea yenye lengo la kujenga na kukuza Imani ya wananchi kwa Mahakama kupitia habari zinazotolewa na vyombo vyao bila kuathiri wajibu na msingi wa kazi ya uandishi wa habari wa kuelimisha, kuhabarisha, kukosoa, kufichua na hata kuburudisha.

Kuhusu Maafisa Ustawi wa Jamii, Jaji Kiongozi alisema wanayo nafasi kubwa katika kupunguza msongamano magerezani kwa kuwa wajibu wao ni kuandaa taarifa ya uchunguzi wa kijamii kwa mfungwa aliyependekezwa kupata adhabu mbadala na Mahakama hutumia taarifa hizo kufikia uamuzi wa kutoa au kutotoa adhabu mbadala.

Alisema uzoefu unaonesha kuwa Maafisa hawa ni wachache nchini hivyo husababisha wafungwa wanaostahili adhabu mbadala kutopata. Aliongeza kuwa matarajio ya Tume na Mahakama ni Serikali kuendelea kuwaajiri Maafisa hawa ili matakwa ya Sheria ya Huduma kwa jamii yatekelezwe.

Kwa upande wa Madalali wa Mahakama ambao wana wajibu wa kutekeleza tuzo mbalimbali zinazotolewa na Mahakama, Mhe. Siyani alisema Madalali ni Maafisa wa Mahakama hivyo utendaji wao ni muhimu kwa Mahakama kwa kuwa unaweza kuipa sifa au kuipaka matope.

Alisema matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona Madalali wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria na kwa uadilifu. Aidha aliwataka wananchi walioathiriwa na vitendo vya ukosefu wa maadili vilivyofanywa na Madalali kutoa taarifa kwenye kamati za uteuzi na nidhamu zilizoko kwenye kila mkoa na makao makuu ya Mahakama.    

 Aidha, Jaji Kiongozi amezitaka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama kuimarisha mawasiliano na ushirikiano hasa katika kupanga mashauri ili vikao vinavyopangwa vilete tija. Alifafanua kuwa Mahakama ndiyo yenye mashauri na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ndiyo yenye jukumu la kuwalipa mashahidi. Ameishauri Ofisi hiyo kufungua ofisi kwenye kila wilaya nchini kama Mahakama inafanya hivi sasa.

 Tume ya Utumishi wa Mahakama imemaliza ziara yake katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu iliyolenga kuitangaza Tume hiyo na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya mikoa na wilaya pamoja na Wadau wa Utoaji haki.  

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na Wadau wa Mahakama wakati wa Mkutano wa Tume jana mkoani Simiyu.
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Simiyu wakiwa kwenye Mkutano wa Tume jana mkoani Simiyu.
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Simiyu wakiwa kwenye Mkutano wa Tume jana mkoani Simiyu.
  
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni